Tanzania mwenyeji mkutano wa Fiata Rame 2025, mageuzi ya kidijitali kuangaziwa

Unguja. Wakati mkutano wa kimataifa wa Shirikisho la Vyama vya Mawakala wa Ushuru na Forodha Afrika Mashariki na Kati (Fiata Rame) ukitarajiwa kufanyika Zanzibar, uimarishaji ujuzi katika usafirishaji ni miongoni mwa mambo yanayotarajiwa kujadili kwa kina.

Malengo mengine yatakayofikiwa ni kuchunguza mageuzi ya kidijitali, teknolojia mpya na suluhisho za ubunifu katika sekta ya vifaa ili kupunguza athari za kimazingira.

Akitoa taarifa kwa waandishi wa habari leo Machi 8, 2025 mjini Unguja, Waziri wa Uchukuzi, Professa Makame Mbarawa amesema Tanzania imechaguliwa kuwa mwenyeji wa mkutano huo.

Ametaja eneo lingine litakaloangaziwa katika mkutano huo ni kuwezesha majadiliano juu ya mbinu bora na utafiti wa kisasa kuhusu vifaa endelevu.

“Kukuza mazingira ya kisheria yanayounga mkono sekta bora na endelevu ya vifaa na kutoa jukwaa la washiriki kuungana na wateja, wawekezaji na washirika wapya,” amesema Profesa Mbarawa.

Amesema mkutano huo unaotarajiwa kufanyika Aprili 30 hadi Mei Mosi na kufunguliwa na Rais Samia Suluhu Hassan, pia, utajadili masuala ya urahisishaji biashara, ufadhili, bima, teknolojia na uboreshaji wa taaluma ndani ya tasnia ya usafiri na usafirishaji

“Washiriki watapata nafasi ya kufahamu fursa zinazotokana na mpango wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) na mchango wa tasnia ya usafiri na usafirishaji katika kusaidia ukuaji wa uchumi endelevu barani Afrika, mashariki ya kati na ulimwenguni,” amesema.

Amefafanua kuwa mkutano huo utakuwa na mambo mengine tofauti ikiwemo maonyesho ya bidhaa na huduma, majadiliano ya wataalamu, vikao vya biashara kati ya kampuni na biashara za Serikali na safari za utalii. 

Alitumia nafasi hiyo kutoa rai kwa wadau wa sekta ya uchukuzi kutoka Tanzania, Afrika Mashariki, Barani Afrika na ulimwenguni kutumia fursa hiyo kwa kushiriki kwenye mkutano huo muhimu.

Rais wa Chama cha Wakala wa Ushuru na Forodha Tanzania (Taffa), Edward Urio amesema mkutano huo utawanufaisha Watanzania kwa kuzitambua fursa za kiuchumi ambazo wataweza kujiongezea kipato.

Naye Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Makame Machano Haji, amesema

Serikali imejipanga vizuri kufanikisha mkutano huo wenye lengo la kuimarisha uchumi endelevu kupitia sekta ya usafirishaji.

“Hii ni fursa muhimu na kubwa kwa Zanzibar katika masuala ya usafiri wa bahari, kwa hiyo ipo haja kuchangamkia fursa hii,’ amesema

Naye Rais wa Chama cha Mawakala wa Ushuru na Forodha Zanzibar (ZFB), Omar Said Mussa amesema bila ya miundombinu mizuri sekta ya usafiri na usafirishaji haiwezi kufanya vizuri.

Related Posts