Dar es Salaam. Waombolezaji wameendelea kufika nyumbani kwa Profesa Philemon Sarungi kutoa pole akiwemo Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku, ambaye amesema Profesa Sarungi, alikuwa mtu mwadilifu na aliyependa nchi yake.
Profesa Sarungi ambaye amewahi kuhudumu kama waziri wa wizara mbalimbali na mbunge wa zamani wa jimbo la Rorya alifariki Machi 5, 2025 akiwa nyumbani kwake Oysterbay, ambapo alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya moyo.
Butiku amesema sifa nyingine Sarungi alikuwa hapendi mtu anayetumia uongozi kujilimbikizia mali, na ndio maana hata waliofika nyumbani kwake wataona namna gani aliishi maisha ya kawaida licha ya nyadhifa mbalimbali alizowahi kushika serikalini.

“Viongozi walioko madarakani wana la kujifunza kwa Profesa Sarungi, hakupenda kujilimbikizia mali, alikuwa mwadilifu aliyejitoa kwa nchi yake naomba wengine kupitia kwake wajifunze namna gani ya kuwa kiongozi bora,” amesema Mwenyekiti huyo.
Aidha Mwenyekiti huyo amesema mara ya mwisho kukutana na Profesa Sarungi ilikuwa miaka mitatu iliyopita na baada ya hapo walikuwa wakiwasiliana kwa njia ya simu, na wala hajawahi kumwambia kuwa alikuwa anaumwa.
“Pia kinachoniuma zaidi siku tatu zilizopita nilipita hapa nje kwake, nikawa namwambia dereva wangu kuwa kuna rafiki yangu anaishi hapa anaitwa Sarungi, sijui atakuwepo kwa kuwa wakati wote geti lilikuwa linafungwa, hivyo leo naumia kuwa amefariki na sikuweza kuja kumuona,” amesema Butiku.
Kwa upande wa taaluma yake ya udaktari, amesema alikuwa daktari wa kwanza kuonyesha uwezo kwa madaktari waliosoma nje ya nchi, ambapo kipindi cha miaka ya 70 walikuwa hawaamini elimu yao zaidi ya waliosoma nchini na nchi za Afrika Mashariki.
“Profesa Sarungi alikata mzizi wa kutoaminiwa kwa madaktari waliosoma nje kwani alifanya kazi yake vilivyo, ninakumbuka alipoteuliwa kuwa Mkurugenzi Hospitali ya Taifa Muhimbili, alionyesha uchapakazi wake ikiwemo uwekaji wa bustani katika eneo lile,” amesema Butiku.
Moja ya kitu anachokumbuka alichoongea naye mara ya mwisho, amesema alimwambia kuwa anaandaa kitabu cha maisha yake na alimuonyesha ila kilikuwa bado hakijakamilika.

Aliyewahi kuwa Msemaji Mkuu wa Serikali, Balozi Mobhare Matinyi akisaini kitabu cha maombelezo katika msiba wa aliyekuwa Waziri wa zamani na Mbunge wa Rorya, mkoani Mara, Profesa Philemon Sarungi nyumbani kwake Oysterbay jijini Dar es Salaam.
Butiku ametoa wito kwa familia ya Sarungi, kuhakikisha wanakimalizia kitabu hicho ambacho anaamini watakaokisoma watajifunza mengi kutoka kwake.
Kwa upande wake aliyewahi kuwa msemaji mkuu wa Serikali, Balozi Mobhare Matinyi amesema watamkumbuka Profesa Sarungi kwa uzalendo wake wa kweli.
“Profesa Sarungi alilitumikia Taifa katika nafasi mbalimbali ikiwemo ya taaluma yake ya udaktari na upasuaji bingwa na pia kwenye siasa ,”amesema Balozi Matinyi.
Mwili wa Sarungi (89) unatarajiwa kuagwa Machi 10,2025 katika viwanja vya Karimjee jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Mwananchi Digital leo Jumamosi Machi 8,2025, msemaji wa familia ya Sarungi, Martin Sarungi amesema shughuli za kuaga zitafanyika katika viwanja vya Karimjee kabla ya kufanyika kwa maziko makaburi ya Kondo jijini humo.
“Kama ambavyo nilisema jana (Ijumaa Machi 7,2025) tunatarajia kumzika mpendwa wetu Jumatatu (Machi 10,2025) na ratiba ndio ipo hivyohivyo, ila shughuli za kumuaga zitafanyika viwanja vya Karimjee ili kuwapa nafasi na watu wengine kushiriki shughuli hiyo,” amesema Martin.