KONA YA MZAZI: Naafiki mzazi kumchagulia mtoto wake mwenza

Katika jamii nyingi, wazazi wamekuwa na ushawishi mkubwa katika maisha ya watoto wao, ikiwemo suala la ndoa.

Ingawa ulimwengu wa sasa unahimiza uhuru wa mtu binafsi katika kuchagua mwenza wa ndoa, bado kuna jamii na familia zinazoshikilia mila ya mzazi kumchagulia mtoto wake mume au mke. Swali linalojitokeza ni: Je, hatua hii ina faida au hasara kwa mtoto na ndoa yenyewe?

Niliwahi kumuuliza shangazi yangu juu ya hili, na nikamgusi kuwa jambo hili lilikuwa likifanyika sana miaka hiyo na sasa lipo ila si kwa kiwango kikubwa.

Akaniambia siyo zamani tu, hata sasa linaendelea. Akasema mara nyingi wazazi huangalia ustawi wa kifamilia na wa kifedha wa mtoto wao pale wanpoamua kumchagulia mwenza.

Anasema wengine hutaka kuona mtoto wao anaolewa au anaoa katika familia yenye maadili, kipato kinachoelewe lakini fmilia ambayo inachangamana na watu kwa lengo la kuleta umoja na mshikamano n jamii inyowazunguka, jambo ambalo linaweza kusaidia ustawi wa ndoa yao kwa muda mrefu.

Lakini akasema watu wengi huamini wazazi wana uzoefu mkubwa wa maisha na uhusiano kuliko watoto wao. Kwa sababu hiyo, wanaweza kuona mambo ambayo vijana hawayatambui kutokana na hisia au mapenzi ya muda mfupi. Hivyo, wanaona uchaguzi wao unaweza kuwa wa busara zaidi kwa sababu utazingatia tabia, malezi na maadili ya mwenza anayechaguliwa.

Hivyo hata mimi nikamuelewa kwamba katika jamii nyingi, ndoa sio muunganiko wa watu wawili pekee, bali ni muunganiko wa familia mbili.

Wazazi wanaposhiriki katika kuchagua mwenza, wanaweza kuhakikisha kuwa familia zinapatana na zina uhusiano mzuri, jambo ambalo linapunguza migogoro ya kifamilia katika ndoa.

Katika zama tulizonazo sasa, vijana wengi hivi sasa wanaathiriwa na dhana za kimapenzi zinazoonyeshwa kwenye filamu, tamthilia na mitandao ya kijamii, ambazo si za uhalisia wa maisha halisi.

Sasa wazazi wanapochagua mwenza, mara nyingi wanaangalia mambo ya msingi kama maadili, utulivu wa maisha na heshima badala ya mapenzi ya muda mfupi.

Nasema hivi kwa sababu tangu enzi na enzi, jamii nyingi, ndoa hupewa umuhimu mkubwa wa kiutamaduni na kidini. Wazazi wanapochagua au kukubaliana na chaguo la mtoto wao, ni kwamba wanataka kuhakikisha ndoa hiyo inakwenda kudumishwa kwa kuzingatia mila na desturi za kifamilia, jambo ambalo linaweza kusaidia mshikamano nadnia ya familia.

Japo kila mzazi anatambua kuwa watoto wake wanapolelewa, wanapewa nafasi ya kufanya uamuzi wao wenyewe kuhusu masuala mbalimbali ya maisha.

Hivyo baadhi wanaona kumchagulia mwenza wa ndoa kunaweza kuwanyima uhuru wa kufanya uamuzi kuhusu mtu anayempenda na anayetamani kushirikiana naye katika maisha yake yote.

Mara nyingi, tunaambiwa na wataalamu wa taasisi ya ndoa wanagusia kwamba ndoa zinazopangwa na wazazi, zinaweza kukosa mapenzi ya dhati kati ya wanandoa.

Wanasema kama kijana au binti hajampenda mwenza wake kwa dhati, kuna uwezekano wa kutokuwepo kwa uhusiano wa kihisia wa kweli, jambo ambalo linaweza kusababisha mtafuruku mkubwa na ndoa inaweza kuvunjika.

Ingawa wazazi wanaweza kuzingatia vigezo muhimu, haimaanishi kuwa ndoa itakuwa yenye mafanikio kama wawili hao hawana maelewano na haiba zao hazipatani.

Katika baadhi ya matukio, wazazi wanaweza kuwa na matarajio makubwa kutoka kwa ndoa wanayoipanga kwa mtoto wao, lakini kama itakuwa na changamoto, inaweza kusababisha migogoro kati ya mtoto na wazazi wake, hasa ikiwa hakuwa na uhuru wa kuchagua mwenza wake mwenyewe.

Tukumbuke kuwa dunia inabadilika kwa kasi na vijana wanazidi kuwa na vipaumbele tofauti kuhusu ndoa na maisha yao kwa ujumla.

Mila ya mzazi kumchagulia mtoto mwenza inaweza kuwa kikwazo hasa kwa kizazi kipya ambacho kinathamini uhuru wa uamuzi na mapenzi ya kweli.

Hivyo mzazi kumchagulia mtoto wake mwenza wa ndoa ni jambo lenye pande mbili; lina faida na hasara zake.

Ingawa wazazi wanaweza kuwa na nia njema, ni muhimu pia kuwapa watoto wao uhuru wa kuchagua wenza wao kwa kuzingatia mapenzi na maelewano.

Njia bora ni kushauriana, badala ya kulazimisha, ili kuhakikisha ndoa inakuwa yenye furaha, heshima na mafanikio kwa wote wawili.

Related Posts