Tarehe 8 Machi ilikuwa ni wakati wa dunia kusherehekea Siku ya Wanawake Duniani. Ni siku ya kutafakari maendeleo, kusherehekea mafanikio, na bila shaka, kupiga kelele kuhusu changamoto zinazowakabili wanawake.
Kwa sababu kusema ukweli, ingawa tumepiga hatua kwa kiasi kikubwa lakini bado wanawake wanapitia changamoto nyingi sana ambazo sio za ulazima. Kwa mfano, kwanini mpaka leo mtu kuna mabinti wananyima fursa ya kwenda shule eti kwa sababu tu ya jinsia yao? Kwanini mpaka leo kuna wanawake wanakosa fursa kwenye siasa na nafasi za uongozi mbalimbali kwa sababu tu ya jinsia zao.
Tumeona mijadala mingi ikijikita kwa wanawake pekee, wanawake wakizungumza na wanawake kuhusu changamoto zao, wakitafakari suluhisho wao wenyewe. Lakini hebu tuwe wakweli: matatizo mengi yanayowakumba wanawake hayajaibuka ghafla kama chafya. Kwa kiasi kikubwa, mfumo dume, mila potofu, na hata ukimya wa baadhi ya wanaume vimechangia hali hii. Na hapa ndipo wanawake na wanaondaa mijadala huu wanatakiwa kukumbuka kutuita mezani pindi wanapojadili mada hizi kuhusu wanawake.
Wanaume kwa muda mrefu tumekuwa na fursa nyingi zaidi—katika siasa, uchumi, hata ndani ya familia. Hii haimaanishi kuwa wanaume wote wanakandamiza wanawake, lakini ukweli ni kwamba mifumo mingi ya kijamii imetuweka sisi katika nafasi ya mamlaka. Hivyo basi, ili kubadilisha mambo, inaependeza tukijumuishwa.
Tuseme tunapinga ukatili wa kijinsia, lakini hatumshirikishi baba wa familia katika mazungumzo. Tunasema tunataka usawa kazini, lakini hatujaeleza kwa mabosi wa kiume jinsi wanavyoweza kusaidia. Tunazungumzia usawa wa kijinsia mashuleni, lakini hatuwapi walimu wa kiume nafasi ya kuelewa na kushiriki kubadilisha mitazamo ya wanafunzi wao. Je, tunategemea suluhisho lijitokeze lenyewe?
Kushirikisha wanaume hakumaanishi kuwaachia maamuzi yote. Hapana! Inamaanisha kuwapa nafasi ya kuelewa na kushiriki katika mabadiliko. Ikiwa baba anaelewa kuwa binti yake ana haki ya kusoma sawa na kaka yake, basi atapigania hilo nyumbani. Ikiwa kaka anaelewa kuwa dada yake hastahili kuolewa kwa lazima, atakuwa ngao yake. Ikiwa mume anajua kuwa mkewe ana haki ya kujiendeleza kitaaluma, hatakuwa mzigo wa ndoto zake.
Mabadiliko hayaji kwa amri au kwa lawama pekee. Yanakuja kwa majadiliano, elimu, na ushirikiano. Na kwa hilo, hatuwezi kujadili bila kiti cha mwanaume kuwepo kwenye meza ya mazungumzo.
Tupewe nafasi nafasi ili tujihisi kuwa sehemu ya suluhisho badala ya kuwa sehemu ya lawama pekee. Kwenye mijadala ya haki za wanawake, wanaume tuwepo pia. Tusisahau kwamba kuna wanaume wanaotamani kuona mabinti zao wakifanikiwa, lakini hawajui jinsi ya kuvunja mila kandamizi. Kuna vijana wanaotaka kuwa ‘ma-gentleman’, lakini wamelelewa na mifumo isiyowafundisha hilo.
Kwa hiyo, mwaka huu wa 2025, tunaposherehekea Siku ya Wanawake Duniani, tusisahau kiti cha mwanaume kwenye meza ya mazungumzo. Tuwashirikishe wanaume katika mazungumzo, kwa sababu wanapobadilika, jamii nzima inabadilika.