Dar es Salaam. Papa Francis Machi 7, 2025 aliunda Jimbo Katoliki la Bagamoyo, nchini Tanzania, akimteua Askofu Stephano Musomba kuwa wa kwanza kuliongoza.
Kabla ya uteuzi huo, Musomba alikuwa Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, uteuzi uliofanywa na Papa Francis Julai 7, 2021 na aliwekwa wakfu kuwa askofu Septemba 21, 2021.
Padri Richard Mjigwa, katika taarifa aliyoandika kwenye tovuti ya Vatican News Machi 7, 2025 alisema jimbo jipya la Bagamoyo limeundwa kwa kuligawa Jimbo Kuu la Dar es Salaam na Jimbo la Morogoro.
Kanisa kuu la Jimbo Katoliki la Bagamoyo amesema ni Kanisa la Moyo Safi wa Bikira Maria, lililoko mjini Bagamoyo.
Padri Mjigwa ameandika, Jimbo Katoliki la Bagamoyo linakuwa na parokia 22, mapadri wa Jimbo wanane, mapadri watawa 37 na watawa wanane.
Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Jude Thadaeus Ruwa’ichi jana Machi 7, alitaja parokia zilizomegwa kutoka jimbo hilo kwenda Bagamoyo kuwa ni Bahari Beach, Boko, Bunju, Kinondo, Madale, Mbopo, Mbweni Mpiji, Mbweni Teta, Mbweni, Mivumoni, Muungano, Nyakasangwe, Tegeta Kibaoni, Tegeta, Ununio, Wazo na Mbweni JKT (Parokia Teule).
Alisema mapadri waliopo kwenye parokia hizo na waumini wake watakuwa Jimbo la Bagamoyo chini ya uongozi mpya wa jimbo hilo na si kwake tena.
Kwa mujibu wa Padri Mjigwa, Askofu Musomba ambaye kaulimbiu yake ya kiaskofu ni “Nena Bwana kwa maana mtumishi wako anasikia” alizaliwa Septemba 25, 1969 katika Kijiji cha Malonji wilayani Mbozi mkoani Songwe.
Safari yake kielimu inaanzia katika Shule ya Msingi Malonji kuanzia mwaka 1979 hadi mwaka 1985 alipohitimu darasa la saba, akajiunga na seminari ndogo ya Maua wilayani Moshi, mkoani Kilimanjaro kwa kidato cha kwanza hadi cha sita kuanzia mwaka 1989 hadi mwaka 1995.
Baadaye alijiunga na taasisi ya Wasalvatoriani iliyoko Kola, Morogoro kwa masomo ya falsafa na taalimungu kuanzia 1995 hadi mwaka 2003 akatunukiwa shahada za awali za falsafa na Taalimungu.
Katika safari ya wito alianza kuvutiwa na wito wa kitawa mwaka 1988, akaenda kupata uzoefu na mang’amuzi ya maisha ya kitawa katika Shirika la Waagustiniani (OSA), Mahanje, Jimbo Kuu la Songea.
Alijiunga na upostolanti mwaka 1993 hadi 1998, Mahanje na baadaye Morogoro.
Kuanzia mwaka 1998 hadi 1999 alipokea malezi ya unovisi Jimbo Kuu la Manila, nchini Ufilipino. Septemba 25, 2002 aliweka nadhiri za daima katika shirika la kitawa la Waagustiniani (OSA) na Desemba 9, 2002 alipata daraja ya ushemasi katika taasisi ya Wasalvatoriani ambayo kwa sasa ni Chuo Kikuu cha Jordan, Morogoro.
Alipewa daraja takatifu ya upadri Julai 24, 2003 Mahanje, Jimbo Kuu la Songea, kisha aliteuliwa kuwa paroko msaidizi wa Parokia ya Mavurunza kuanzia mwaka 2003 hadi 2004.
Alitumwa kwenda kusomea Elimu ya Mababa wa Kanisa (Patrology) mwaka 2004 hadi 2008 mjini Roma, Italia akatunukiwa Shahada ya Uzamili katika masomo ya Taalimungu akibobea katika Elimu ya Mababa wa Kanisa
Mwaka 2008 hadi 2009 alikuwa mlezi katika nyumba ya Shirika la Waaugustiani na Mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Jordan, Morogoro.
Mwaka 2009 alitumwa na shirika kwenda Jimbo Kuu la Manila, nchini Ufilipino kutoa semina kwa wanovisi, waprofesi na wapostulanti.
Kuanzia mwaka 2009 hadi 2015 aliteuliwa kuwa paroko wa kwanza katika Parokia ya Temboni, Jimbo Kuu la Dar es Salaam na wakati huohuo akiwa mkufunzi katika Chuo Kikuu cha Jordan, Morogoro.
Mwaka 2015 aliteuliwa tena kuwa wakili paroko wa Parokia ya Mavurunza na Msimamizi wa Jumuiya ya Mtakatifu Monika Mavurunza.
Mwaka huohuo aliteuliwa kuwa paroko wa muda wa Parokia ya Mtakatifu Ambrose Tagaste, Jimbo Kuu la Dar es Salaam hadi mwaka 2016. Kuanzia 2016 hadi 2019 aliteuliwa kuwa Mlezi na gambera wa nyumba ya malezi ya Mtakatifu Agostino iliyopo Morogoro.
Kuanzia mwaka 2019 hadi kuteuliwa kwake kuwa askofu msaidizi amekuwa ni paroko na msimamizi wa Jumuiya ya Mtakatifu Monika Mavurunza, Temboni na Mtakatifu Rita wa Kashia.
Mwaka 2008 hadi 2021 alihudumu kama katibu mwakilishi wa Shirika la Waagustiniani nchini Tanzania.
Padri Mjigwa anaandika kuwa, Askofu Musomba ni mzoefu wa kuongea lugha mbalimbali zikiwemo, Kiswahili, Kiingereza na Kiitaliano. Anasoma Kihispania, Kifaransa, Kigiriki, na Kilatini.