Mwalwisi arejesha majeshi Mbeya Kwanza

ALIYEKUWA Kocha Mkuu wa TMA, Maka Mwalwisi amerejea kukifundisha kikosi cha Mbeya Kwanza katika michezo iliyobakia, akichukua nafasi iliyoachwa na Emmanuel Masawe aliyeanza nacho msimu huu wa Ligi ya Championship.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwalwisi alisema anajisikia furaha kurejea ndani ya kikosi hicho alichowahi kukifundisha miaka ya nyuma, huku akiwataka viongozi na mashabiki kuendelea kumuunga mkono katika michezo hii ya mwishoni wa msimu.

“Malengo yetu ni kuendelea kupigania nafasi mbili za juu na hilo linawezekana kwa sababu hatujapishana pointi nyingi na waliokuwa juu yetu, ikishindikana kabisa angalau tumalize katika miongoni mwa timu nne na hilo naamini linawezekana.”

Mwalwisi aliyejiunga na TMA Januari Mosi 2023 akitokea pia Mbeya Kwanza, msimu huu ameiongoza katika michezo 15, kati ya hiyo alishinda minane, sare mitatu na kupoteza minne, akiiacha nafasi ya tano kwenye msimamo na pointi zake 27.

Kwa upande wa Masawe aliiongoza Mbeya Kwanza katika michezo 22 ya Ligi ya Championship na kati ya hiyo alishinda 11, sare sita na kupoteza mitano, akifunga mabao 32 na kuruhusu 19, akiiacha ikishika nafasi yake ya sita na pointi zake 39.

Related Posts