MSHAMBULIAJI wa Songea United, Cyprian Kipenye amesema anajisikia vibaya kutokana na ukame wa mabao unaomwandama katika kikosi hicho, licha ya kushukuru benchi la ufundi kwa kuendelea kumuamini, kumpa nafasi na kumjenga kisaikolojia.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kipenye alisema kama mshambuliaji huwa inamuumiza anapopitia kipindi kigumu cha kutokufunga mabao, japo anashukuru benchi la ufundi chini ya Kocha Mkuu, Meja Abdul Mingange kwa kuendelea kumwamini.
“Wakati wa dirisha dogo la Januari mwaka huu nilitaka kuondoka kutokana na changamoto nilizopitia ambazo nisingependa kuziweka wazi, ila nashukuru viongozi na kocha wamenijenga vizuri kisaikolojia baada ya kukosa takribani michezo sita.”
Kipenye aliyewahi kuzichezea timu mbalimbali zikiwemo, Biashara United, Simba na Ihefu ambayo kwa sasa ni Singida Black Stars, alisema licha tu ya ushindani uliopo ila bado hawajakata tamaa ya kuipambania Songea United ipande Ligi Kuu Bara.
Nyota huyo aliyejiunga na timu hiyo msimu huu akitokea Dodoma Jiji, amefunga mabao manne ya Ligi ya Championship huku mara ya mwisho kufunga ilikuwa sare ya kikosi hicho ya bao 1-1, dhidi ya Mbuni, mechi iliyopigwa Ruvuma, Oktoba 18, 2024.