KOCHA Mkuu wa Singida Black Stars, David Ouma amezitaja Azam na Tabora United kuwa ndizo timu zinazompa presha kwa sasa kutokana na ushindani uliopo wakiwania nafasi ya tatu ili kupata nafasi ya kushiriki michuano ya kimataifa.
Ouma amesema hayo baada ya kuifunga Namungo bao 1-0 ugenini na kuifanya timu yake iendelee kusalia nafasi ya nne kwenye msimamo wa Ligi Kuu ikiwa imekusanya pointi 44 kwenye mechi 23 walizocheza ikiachwa pointi nne na mshindani wake Azam ambayo ipo nafasi ya tatu na pointi 48 na ikiiacha Tabora United pointi nane.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ouma alisema licha ya kuwa katika nafasi nzuri na kukusanya pointi nyingi bado wapo kwenye presha ya ushindani kwani bado hawana uhakika wa kushiriki nafasi ya kimataifa hivyo wanaendelea kutafuta nafasi hiyo huku wakizitizama timu mbili tishio kwao.
“Pointi nne zaidi kwetu walizo nazo Azam sisi tukichanga vizuri karata zetu tunaweza kufikia lakini hivyo hivyo kwao wakichanga vyema karata wanauwezo wa kutukimbia na kutuacha mbali zaidi, hivyo hivyo kwa Tabora United ambayo imekuwa ikionyesha ubora kwenye michezo yao,” alisema na kuongeza;
“Huu ni mzunguko wa lala salama tuna kikosi bora na kipana ni wakati wa kuonyesha bila kujali mazingira yaliyopo na wachezaji wanatambua malengo ya Singida Black Stars tutapambana hadi tone la mwiosho ili kuhakikisha tunapata kile tunachokitaka.”
Akizungumzia ligi kwa ujumla Ouma alisema bado anakibarua kigumu cha kufanya kuhakikisha anaipambania timu hiyo kufikia malengo yake mwisho wa msimu na kila mchezo ulio mbele yao wanauchukulia na kama fainali wanapambania kombe.
“Hakuna mchezo mwepesi hata KenGold ambayo ni ya mwisho kwenye msimamo sio ya kuichukulia poa ni timu ambayo inaingiza uwanjani wachezaji 11 kama sisi na wenye ubora na malengo tutakuwa wa mwisho kuamini kuwa tumemaliza tuna uhakika wa nafasi kwa pointi tulizonazo sasa,” alisema na kuongeza;
“Ubora wa mchezaji mmoja mmoja na kikosi chetu kwa ujumla ni mzuri lakini hata wapinzani wetu pia wana kikosi kizuri wanapambana kusaka nafasi ya kutwaa taji, wengine kucheza msimu ujao huu ni mzunguko wa lalasalama, ukidondosha pointi mwingine anasonga.”