DHAMIRA YA RAIS SAMIA KUJENGA CHUO KIKUU SONGEA KUANZA KUTEKELEZWA

 

 

Na Albano Midelo,Songea

Meneja wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) Kampasi ya Songea, Dkt. Bakari Mashaka, amesema wanatarajia kuanza mradi mkubwa wa ujenzi wa chuo kitakachokuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 10,000 wa kozi mbalimbali katika kata ya shule ya Tanga Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma.

Dkt. Bakari Mashaka amebainisha kuwa chuo hicho kinaleta mradi Mkubwa wa bilioni 18.5 za Kitanzania ambazo ni fedha za Serikali kujenga Chuo Kikuu Katika Mtaa wa Pambazuko kata ya Tanga Manispaa ya Songea.

Amesema fedha hizo zimetolewa na serikali chini ya Uongozi wa Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye amedhamiria kila Mkoa hapa nchini uwe na Chuo Kikuu,hii ni ahadi ambayo aliitoa kwa wananchi na sasa anaitekeleza kwa vitendo kwa wananchi wa Mkoa wa Ruvuma’’,alisema Dkt.Mashaka.

Amesema kwa sasa, IAA Kampasi ya Songea inatoa huduma zake kwenye jengo la TTCL, ghorofa ya pili, mjini Songea, na Kozi zinazotolewa ni diploma ya Usimamizi wa Biashara, Uhasibu na TEHAMA, Fedha na Benki, pamoja na masomo ya ngazi ya uzamili (Masters) katika fani za Biashara, Fedha, TEHAMA, Uongozi, na Usimamizi wa Rasilimali.

Dkt. Mashaka amesema kuwa chuo hicho kinalenga kuhakikisha wanafunzi wanajifunza kwa vitendo, hasa namna ya kuanzisha na kuendesha biashara ambapo ameeleza kuwa wanataka wanafunzi wao wasitegemee ajira pekee, bali wawe na uwezo wa kujiajiri na kuendesha maisha yao.

Kwa upande wake, Afisa Uhusiano wa IAA Kampasi ya Songea, Nuru Meshack, ameelezea changamoto kubwa waliyoibaini katika Wilaya ya Songea ni wazazi wengi kuamini kuwa mtoto aliyepata daraja la nne hawezi kuendelea na masomo, hivyo amewahimiza wazazi na wanafunzi kuwa ufaulu wa D nne, isipokuwa kwa masomo ya dini, unaruhusu mwanafunzi kujiunga na chuo.

Amewakaribisha wanafunzi kujiunga na IAA Kampasi ya Songea, akisisitiza kuwa chuo hicho kimejikita katika kuwasaidia wanafunzi kujiajiri badala ya kutegemea kuajiriwa na mazingira ya kusomea ni mazuri na yanasaidia mwanafunzi kufanikisha malengo ya kielimu na kuendana na teknolojia.

Chuo cha Uhasibu Arusha Kampasi ya Songea kinapatikana katika jengo la TTCL, ghorofa ya pili, karibu na ofisi za Manispaa ya Songea. Kwa mawasiliano zaidi namba 0784-171-565 au kufika moja kwa moja kwenye ofisi zao.

Katikati ni Rais Dkt Samia Suluhu Hassan akiwa na wanafunzi wa sekondari ya wasichana ya Dkt Samia Suluhu Hassan iliyojengwa Wilaya ya Namtumbo mkoani Ruvuma,baada ya kuifungua rasmi,sekondari hiyo yenye uwezo wa kuchukua wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha sita

Related Posts