Aziz ni kijana wa miaka 24 wa Kipalestina aliyekimbia udhalilishaji kwao akaishia kudhalilika majuu.
Kisa hiki kinafikirisha, kusikitisha na kufundisha. Wapo wengi kama Aziz walioharibikiwa baada ya kuolewa wakidhani wameoa majuu.
Aziz, akiwa hajui hata Kiingereza, alijikuta akijiingiza kwenye ndoa ya mateso. Nkwazi alimjua Aziz. Alikuwa rafiki wa kaka yake aliyemlalamikia kuwa mdogo wake alikuwa akipoteza mwelekeo.
Kutokana na kuwajua wote wawili, Nkwazi aliamua kuingilia kati kusaidia. Kaka mtu alitukutanisha nyumbani kwetu walikozoea kuja kupoteza muda na kufundishwa Kiingereza.
Baada ya kaka mtu kueleza kisa kizima, kama marafiki na walezi, tulimuuonya Aziz asijiingize kwenye uhusiano ambao ungemletea majuto baadaye.
La kufa halisikii dawa. Aziz alichukia hadi kutuambia: “Hii ni Kanada na kila mmoja anaweza kufanya atakavyo.”
Kwa maneno mengine, alitaka tusimuingilie katika maisha na uhuru wake hasa ikizingatiwa kuwa hapa, vijana huweza kuamua kufunga ndoa hata bila kuwahusisha wazazi na ndugu japo si wote.
Ghafla, Aziz aliacha kuja kwetu. Tulijua sababu. Alikuwa kwenye mapenzi na mama aliyemzidi umri tutakayemuita Meg (si jina lake) aliyetaka wafunge ndoa.
Pamoja na kumuonya asisikie, tulijua ni haki yake kufanya hivyo japo tulimtahadharisha juu ya tofauti za mila na dini.
Mfano, tulimjua Meg kama mama aliyekuwa amempenda wakipanga kuoana. Meg alipenda sana kuongelea mbwa wake aliyekuwa akisema kuwa hula na hulala naye wakati mwingine.
Si ajabu huku kwa baadhi ya watu kula na mbwa kwa sababu kwao, mbwa ni sehemu ya familia. Hivyo, tuliona hatari itokanayo na kutofautiana kidini na kimila ambavyo vingemkwaza Aziz.
Baada ya kugundua kuwa Aziz alianza kutuchukia mbali na Meg aliyeambiwa juu ya ushauri wetu. Tukawaacha maana, ulikuwa ni uamuzi na maisha yao.
Hakika, Aziz na Meg walifunga safari kwenda kwenye visiwa vya Saint Lucia kufunga ndoa na kisha fungate ilifuatia.
Wawili haoa walirejea Kanada wakiwa mke na mume. Baada ya hapo, tuliamua kuhama mkoa tuliokuwa tunaishi na kusahau mambo ya Aziz na Meg.
Siku moja, Nesaa alikwama kwenye theluji usiku akitoka shule. Alijitokeza baba wa Kiarabu aliyekuwa na familia yake akamsaidia kwa kujaribu kulikwamua gari asifanikiwe.
Hivyo, alishauri ampe lift hadi nyumbani. Tuligundua kuwa kumbe aliishi mtaa wa pili toka kwetu. Alimsaidia Nkwazi kukwamua gari na tangu siku hiyo wakawa marafiki.
Baada ya miezi kupita, yule Mwarabu alikuja kutuaga kuwa alikuwa anahamia Toronto. Tulifurahi sana na kusikitika.
Hata hivyo, alituuliza kama tunamjua Aziz toka kule tulikokuwa tukiishi mwanzo. Alituelezea namna Aziz alivyomuomba atuombe msamaha kwa kudharau ushauri wetu.
Tulimuuliza yule Mwarabu sababu za Aziz kukimbia na kujutia ndoa yake. Alitwambia kuwa Meg hakuwa tayari kubadili dini wala kuheshimu mila ya Aziz mbali na kutokuwa tayari kuacha kufuga mbwa wake kipenzi pamoja na mambo mengine binafsi kama nani mwenye madaraka zaidi ya mwingine kati yake na mkewe.
Kwa ufupi, Aziz alijikuta kwenye ndoa ya mateso hadi akakimbilia Toronto kuepuka ndoa ya mateso. Tulifurahi kusikia kuwa Aziz alikuwa amegundua makosa yake na mchango wetu na kujutia.
Hata hivyo, maji yalikuwa yameishamwagika. Aziz, licha ya kuonja mateso na kuumia, alipoteza malengo na muda wake. Tulimshauri akasome kwanza akaghairi.
Sasa tujiulize. Kisa hiki kinafundisha nini? Mosi, usilolijua litakusumbua hata kukuuumiza. Pili, asiyesikia la mkuu huvunjika guu. Tatu, vijana waepuke kujiingiza kwenye makubaliano ya ndoa bila uzoefu wala ushauri.
Nne, tofauti za dini hata mila ni muhimu katika kufikia uamuzi wa kufunga ndoa. Mfano, Aziz, Muislam, asingeweza kuishi na hata kuchangia kitanda na vyombo na mbwa.
Tano, umri katika ndoa ni muhimu. Japo hatukatazi waliozidiana umri kuoana, kuna haja ya kulidurusu na kulijadili hili kabla ya kujifunga kwenye ndoa. Sita, si kila ving’aavyo ni dhahabu.
Mwisho, ingawa haya yanaweza kuchukuliwa kama masuala binafsi, yana somo kubwa kwa vijana wanaofikiri kuwa kuoa majuu ni kuukata.
Wakati mwingi na mwingine, kufanya hivyo si kuukata bali kukatwa kama ilivyo kwa Aziz na wengine kama yeye.