Vatican yatoa mwenendo afya ya Papa Francis

Roma. Vatican imesema Papa Francis anaendelea vyema na matibabu ya nimonia katika mapafu yote mawili huku akionesha maendeleo katika afya yake.

Taarifa hiyo ya Vatican iliyotolewa leo Jumapili Machi 9, 2025, inaeleza kuwa, madaktari wake wameamua kuendelea kuwa waangalifu kuhusu hali yake, wakimaanisha bado hajaondoka kwenye hatari ya kiafya inayosababishwa na maambukizi hayo.

Papa huyo mwenye umri wa miaka 88, ambaye ana ugonjwa sugu wa mapafu uliosababisha sehemu ya pafu lake kuondolewa alipokuwa kijana, ameendelea kuwa thabiti kwa siku kadhaa.

Madaktari wanasema hana homa na kiwango cha oksijeni kwenye damu yake ni cha kuridhisha.

Madaktari hao wamesema uthabiti huo unathibitisha mwitikio mzuri kwa matibabu anayopewa kiongozi huyo wa kiroho.

Hiyo ni mara ya kwanza kwa madaktari kuthibitisha kwamba, Papa Francis anaitikia vyema matibabu dhidi ya maambukizi hayo ya mapafu, ambayo yaligunduliwa baada ya kulazwa hospitalini Februari 14, 2025.

Francis aliendelea na kazi zake na kupumzika jana Jumamosi, akiingia wiki ya nne katika Hospitali ya Gemelli huko Roma huku hali yake ikiwa imetulia baada ya kukumbwa na matatizo ya kupumua wiki iliyopita.

“Ili kuhakikisha maendeleo haya ya awali yanaendelea siku zijazo, madaktari wake wameamua kuendelea kuwa waangalifu,” inaeleza taarifa hiyo.

Licha ya kutokuwepo kwa Papa, shughuli za kila siku za Vatican zinaendelea.

Kardinali, Pietro Parolin aliendesha Misa katika Kanisa la Mtakatifu Petro. Misa hiyo ilikuwa maalumu kwa ajili ya kundi la wanaopinga utoaji mimba.

Parolin alisoma ujumbe wa Papa kutoka hospitalini, akisisitiza umuhimu wa kulinda maisha kutoka kwa kuzaliwa hadi kifo cha kawaida.

Baadaye Jumamosi, Kardinali mwingine wa karibu na Papa, Michael Czerny kutoka Canada, aliendesha maombi ya kila usiku kwa ajili ya Papa.

Leo Jumapili, Czerny pia ataongoza Misa ya Mwaka Mtakatifu kwa ajili ya wahudumu wa kujitolea misa ambayo Papa Francis alipaswa kuongoza.

Papa Francis amekuwa akitumia oksijeni ya kiwango cha juu kumsaidia kupumua.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaasa wa Mashirika.

Related Posts