UNAWEZA kusema Yanga Princess chini ya kocha Edna Lena ‘ Mourinho’ imeanza kujipata kutokana na muendelezo na ubora wanaouonyesha msimu huu.
Mwanzoni mwa msimu Yanga ilianza vibaya Ligi Kuu (WPL) kwa mfululizo wa matokeo ikianza na sare ya 1-1 na Bunda Queens, 1-1 na Alliance Girls, 2-2 na Mashujaa na kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Simba.
Dirisha dogo ikafanya usajili kwa baadhi ya maeneo ikiwamo eneo la ushambuliaji ikimuongeza Mrwanda, Jeaninne Mukandasyenga akitokea Rayon Sports na hadi sasa kwenye mechi nne amefunga mabao matano, kiungo Aregash Kalsa kutoka C.B.E, golikipa Zubeda Mgunda na mabeki Protasia Mbunda, Diana Mnally.
Ongezeko la nyota hao kwa kiasi kikubwa limeongeza ari ya upambanaji katika kikosi hicho kinachopambania nafasi ya ubingwa.
Akizungumzia juu ya mabadiliko ya kikosi hicho, Mourinho alisifu juhudi za wachezaji kwenye kikosi hicho akitaja uzoefu wa nyota wapya.
“Ingawa watu wanaona kuna mabadiliko makubwa lakini kwangu naona bado kidogo, nafikiri wachezaji wakipata mechi nyingi mtaona ubora wao na naamini wataleta mabadiliko makubwa, “ alisema Mourinho.