Majaliwa awapa ujumbe viongozi wa dini

Manyara. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa amewasihi viongozi wa dini nchini waendelee kukemea vikali vitendo vyote ambavyo ni kinyume na maadili ya dini na utamaduni wa Mtanzania.

Majaliwa ametoa rai hiyo leo Jumapili Machi 9, 2025 alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan katika ibada ya kuwekwa wakfu na kutawazwa kwa Askofu wa Pili wa kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kiteto, Askofu Bethuel Mlula iliyofanyika Kanisa Kuu la Anglikana la Mtakatifu Mikaeli, Kiteto mkoani Manyara.

“Ninawaomba viongozi wetu wa dini tuendelee kuliweka suala la kuimarisha malezi na kidhibiti mmomonyoko wa maadili kuwa ajenda ya kudumu. Lazima tuwe na maadili mema ili Taifa liwe endelevu,” amesema.

Aidha, Majaliwa amesema pamoja na masuala ya kiroho amewaomba viongozi wa dini waendelee kuwahamasisha waumini kuunga mkono ajenda mbalimbali za kitaifa, ikiwamo ya uhifadhi wa mazingira, kampeni ya nishati safi na upandaji miti pamoja na kushiriki katika hatua zote za uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amempongeza Askofu wa kwanza mstaafu wa kanisa hilo Askofu Isaiah Chambala kwa kazi kubwa aliyoifanya katika kipindi cha uongozi wake, pia ametumia fursa hiyo kumhakikishia ushirikiano wa kutosha kwa masilahi mapana ya Wana-Kiteto na Watanzania kwa jumla.

“Nitumie nafasi hii kuwahakikishia viongozi wetu wa dini kwamba Serikali ipo pamoja nanyi, tutaendelea kuwa na vikao vya pamoja na sisi tunathamini sana namna ambavyo mmejitoa kuiunga mkono Serikali hii”

Kwa upande wake, Askofu Mlula ameipongeza Serikali kwa jitihada kubwa zinazofanyika ili kuwaletea Watanzania maendeleo katika sekta mbalimbali nchini ikiwamo ya afya na elimu.

Aidha, Askofu Mlula ameipongeza Serikali kwa kusimamia amani umoja na utulivu iliyoasisiwa na Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume.

New Content Item (1)
New Content Item (1)

 “Amani ni tunu ambayo Mwenyezi Mungu ametupatia, tuitumie amani hii kujiletea maendeleo,”amesema.

Naye, Askofu wa Tanga na Askofu Mkuu wa Kanisa Anglikana Tanzania, Maimbo Mndolwa ametoa wito kwa wakazi wa Kiteto kwenda kuhakiki majina yao katika daftari la kudumu la wapiga kura ili waweze kushiriki uchaguzi mkuu wa wabunge na madiwani.

“Haki ya jina kuwepo kwenye daftari ni yako ila unaweza kuipoteza usipoitumia vizuri, tushiriki katika michakato iliyoandaliwa na Serikali.”

Related Posts