Siku tano za Makalla kupoza joto la uchaguzi CCM Dar

Dar  es Salaam. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla ametumia ziara ya siku tano Mkoa Dar es Salaam kufanya mikutano ya ndani.

Hiyo ilikuwa ziara ya tatu ya Makalla kuifanya katika mkoa huo tangu kuchaguliwa kuwa mlezi wa mkoa huo kichama, ya kwanza aliifanya kwenye maandalizi ya kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa Novemba 2024, baadaye alifanya nyingine kuvunja makundi yaliyotokana na uchaguzi huo.

 Katika mikutano hiyo ambayo Makalla alikuwa mzungumzaji na kutoa maelezo ilikutanisha viongozi wa majimbo yote 10  ya uchaguzi ikiwamo Ilala, Kinondoni, Kawe, Ubungo, Kibamba, Segerea, Temeke, Mbagala, Ukonga, Kigamboni na kata 102 zinazounda mkoa huo wenye mitaa 564.

Kutokana na vurugu zinazoendelea kwa makada wa chama hicho, kila mmoja kutaka kujionyesha anahitaji nafasi, ilimlazimu kiongozi huyo kulipa msukumo jambo hilo huku akisema watakaobainika  chama hakitasita kuwachukuliwa hatua za kinidhamu ikiwamo kuwaengua watakapofanya mchujo.

Makalla aliyeambatana katika ziara hiyo na mwenyekiti wa CCM mkoa huo, Abbas Mtemvu na wajumbe wa halmashauri kuu ya chama hicho, Simba Gadafi na Dk Ibrahim Msengi alidai imefikia hatua watuhumiwa wanashtakiana wenyewe kwa wenyewe, jambo linaharibu taswira ya chama hicho tawala.

Aliwataka makada hao kuheshimu taratibu za chama kwa kuzingatia  kanuni walizojiwekea  na kuwataka wanaohitaji kugombea nafasi ya udiwani au ubunge kusubiri muda ufike.

Jambo hilo alikemea  katika wilaya zote ingawa Wilaya ya Kigamboni hoja hiyo aliizungumza zaidi.

Makalla alidai jimbo hilo limezidi na imefikia hatua hadi viongozi wa chama hicho waliopewa dhamana wanaandaa mikutano na kupita kutambulisha watu mbalimbali.

Chanzo cha vurugu hizo kushamiri Kigamboni  ni baada ya aliyekuwa mbunge wake Dk Faustine  Ndugulile na aliyekuwa Mkurugenzi Mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Kanda ya Afrika, kufariki dunia usiku wa kuamkia Novemba 27, 2024 nchini India alikokuwa akipatiwa matibabu.

Dk Ndugulile alipeperusha bendera ya chama hicho kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika mwaka 2020 na kushinda  baada ya kuvuka kiunzi cha kura za maoni zilizofanyika katika mchakato wa ndani, akipata kura 190 akimpiku Paul Makonda aliyeambulia kura 122

Makalla alidai viongozi hao wamekuwa wakiomba hadi bajeti ya fedha kwa makada kwa ajili ya kuandaa mikutano ya hadhara ili kuwauza wagombea huku akiwataka wajirekebishe.

Kutokana na uzito wa jambo hilo hasa wanapoelekea kupiga kura za maoni, aliagiza watendaji wa chama hicho kwa kushirikiana na kamati za siasa za wilaya kuwabaini ili muda wa mchujo ndani ya chama hicho ukianza, iwarahisishie kuwaengua wagombea hao.

 Pia, aligusia na kuonya mtindo wa kufanya uteuzi na utenguzi kwa mabalozi unaoendelea kufanyika wilaya mbalimbali, huku akikiri walishapokea malalamiko kutoka wilaya tatu na kutoa kalipio akisema wamegundua mchezo huo unalenga upangaji safu.

 Si hivyo tu, alitoa elimu ya mabadiliko madogo ya katiba ya chama hicho kupitia Mkutano Mkuu Maalumu uliofanyika jijini Dodoma kuanzia Januari 18 hadi 19, 2025 akisema yanayolenga kuboresha utendaji wa chama na kuongeza ushiriki wa wanachama katika michakato ya uteuzi.

Mabadiliko ambayo Makalla aliyapongeza  akidai yatakuza demokrasia, kuziba mianya ya rushwa, kuongeza ushiriki wa wajumbe katika mchakato wa kupendekeza majina ya wagombea, kuimarisha uwajibikaji na kudhibiti tabia ya kupanga safu za wajumbe.

Pia, alidai kutokana na mabadiliko hayo wanalenga kuwalinda madiwani na wabunge waliopo madarakani waweze kufanya kazi zao kwa uhuru, kwa kuwa, wamebeba maono na malengo ya wananchi katika utatuzi wa kero zao.

‘No reform no election’ ya Chadema

Katika hatua nyingine Makalla aliizungumzia kampeni ya “hakuna mabadiliko, hakuna uchaguzi” ya Chadema inayolenga kuishinikiza Serikali kuboresha mifumo ya uchaguzi akidai haina hoja.

Makalla alisema uchaguzi utafanyika na iwapo hawatashiriki uchaguzi ile dhana ya chama hicho kuitwa kikubwa cha upinzani itatoweka.

Makalla alidai wanachosimamia Chadema hawakijui, akijenga  hoja kwa kudai mabadiliko tayari yalishafanyika na hakuna mtu kupita bila kupingwa, wakurugenzi hawatasimamia uchaguzi  na wafungwa ambao kifungo chao hakizidi miezi sita, watashiriki shughuli ya upigaji kura.

Kampeni ya Chadema ya ‘No reform no election,’ ni msimamo wa chama hicho uliopitishwa na wajumbe wa kamati kuu ya chama hicho ulifanyika  Januari 21,2025 Ukumbi wa Mlimani City na unatakiwa kusimamiwa na Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu kuhakikisha unatekelezwa.

Wachambuzi wanavyoizungumzia ziara hiyo,  Dk Conrad Masabo  amesema kila chama kina mtazamo wake wanapouangalia  uchaguzi na  CCM inatofautiana na vyama vingine vya upinzani.

“Vyama havina uwanja sawa, katika medani za kisiasa jambo linaloona CCM ni tatizo, vyama vya upinzani huenda wasione tatizo kwa sababu CCM uwanja wao ni tofauti, Makalla anaongea anatoka upande unaonufaika na mfumo uliopo,”amesema.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Dk Ponsian Ntui amesema CCM imekuwa na mbinu yao kila tume inapoenda mkoa fulani wanaenda kutoa elimu kuhakikisha watu wao wanajitokeza.

“Nijambo linalopaswa kufanywa na vyama vyote, inaonekana tume haina nguvu ya kuhamasisha, kwa kutoa elimu ya uraia na kuwaeleza kwa nini wanapiga kura na ukiangalia maeneo mengi hakuna hamasa,”amesema Dk Ntui.

Kuhusu vurugu kabla uchaguzi Dk Masabo amesema ni hoja ambayo haina mashiko kwa sababu kama mgombea wa chama hicho kwa ngazi ya urais ameshatoka, kwanini makada wasijipange, inakuwaje wanataka nafasi moja ijulikane mapema na zingine zisubiri?

“Labda waje kutuambia kilichosababisha CCM wakafanya mapema kupata wagombea wa urais lakini wanaona mapema, lakini wanaona ni shida kwa wagombea wa udiwani na ubunge kupatikana sasa, kuna kukosekana kwa hadi ndani ya CCM kwani nafasi fulani zinaonekana ni sahihi zikipata wagombea mapema,”amesema.

Dk Masabo amesema kuna mkanganyiko, mwaka huu wanakwenda kwenye uchaguzi mkuu unaohusisha Rais, wabunge na madiwani huku akisema alikuwa anafikiria ni vizuri wangeruhusu na nafasi zingine wapatikane wagombea.

“Naona kama wamewanyima wanachama wao haki ambayo wanachama wengine wamepewa wagombea nafasi za juu za urais Tanzania Bara na Zanzibar,” amesema. 

Kwa upande wake Dk Ntui amesema makundi hayaepukiki na hawawezi kuzuia kwenye michakato ya uchaguzi na njia inayotumika dunia nzima ni kuvunja makundi baada ya uchaguzi.

“Nafikiri alitakiwa kujielekeza makundi hayo yasitumie lugha ambazo zitaleta ugumu katika kuvunja makundi baada ya uchaguzi, watu wasikosoane nidhamu ili iwe rahisi hata kumuunga mkono aliyeshinda,” amesema.

Kuhusu kusema hakuna anayeweza kusimamisha uchaguzi, Dk Masabo amesema  si dhana sahihi kwa sababu mwaka 2005 kuna mgombea wa urais alifariki dunia na uchaguzi ulisogezwa mbele inakuwaje haiwezekani kubadilisha siku ya uchaguzi?

“Unayepinga haiwezekani kubadilisha tarehe unakuwa hauko sawa, tunachopaswa kujiuliza hoja zinazozungumzwa kweli zinakidhi sifa uchaguzi? Unaweza kuahirishwa au kusogezwa mbele, lakini ukirudi kwenye Katiba wanasema Serikali itapata madaraka kutoka kwa wananchi,”amesema.

Kuboresha daftari la mpigakura

Shughuli ya uboresha wa daftari la kudumu la mpigakura inayosimamiwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kwa mkoa huo wenye idadi kubwa ya wapigakura inatarajiwa kuanza Machi 17 hadi 23, 2025 na itakuwa hitimisho baada ya kazi hiyo kufanyika mikoa yote Tanzania kujiandaa na uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.

Kwa mujibu wa INEC, mkoa huo unatarajiwa kuwa na wapigakura 4,071,337 baada ya uboreshaji kufanyika kuanzia mwaka huu, ikiwa ni ongezeko la wapigakura wapya 643,420, sawa na asilimia 18.7, kutoka idadi ya wapigakura 3,427,917 waliopo baada ya uboreshaji uliofanyika mwaka 2019/20.

Ujumbe mkubwa uliwataka viongozi kuanzia ngazi ya mashina ya chama hicho, matawi, kata na wilaya kila mmoja kuhamasisha watu wake kwenda kuboresha taarifa zao muda ukifika huku akieleza shabaha yao ni kutetea dola na bila kuwa na uhakika wa wapigakura hawawezi kufanikiwa.

Related Posts