Kocha Msaidizi wa Simba, Seleman Matola, amesema kupoteza tena mbele ya Yanga kumezidi kufanya safari ya ubingwa kuwa ngumu.
Akizungumza baada ya dakika 90 za mchezo wa Kariakoo Dabi kumalizika, Matola amekiri wamepoteza nafasi ya ushindani kuwania ubingwa msimu huu, lakini haina maana kwamba ndio mwisho wa msimu kwani bado wana mechi nyingine zilizobaki.
“Tulianza bila mshambuliaji, lakini mara baada ya kufungwa mabao mawili, tukamuingiza mshambuliaji ambaye amefunga bao la kufutia machozi,” amesema na kuongeza;
“Mabadiliko ya mapema pia tuliyoyafanya yametugharimu kwa sababu mchezaji aliyeingia kafanya makosa, wapinzani wakapata faida ya penalti kutokana na kosa alilolifanya ndani ya 18.”
Matola amesema walikuwa wanatambua jeraha alilokuwanalo, Henock Inonga na waliamini ataweza kumaliza dakika 90, lakini mambo yameenda tofauti, huku akiweka wazi kuwa, beki huyo kapata jeraha jipya.
Inonga alilazimika kufanyiwa mabadiliko dakika ya 12 na nafasi yake kuchukuliwa na Hussein Kazi ambaye muda mchache tangu kuingia kwake, akasababisha penalti iliyokwenda kufungwa na Stephanie Aziz Ki.
Katika hatua nyingine, Matola amezungumzia namna timu yao ilivyo na makosa katika eneo la ushambuliaji sambamba na ulinzi ambapo wameruhusu mabao kwenye kila mchezo.
“Tatizo la washambuliaji na wachezaji wanaopewa nafasi ya kucheza wamekuwa wakishindwa kutumia nafasi sawa na mabeki makosa yamekuwa yakijirudia na sisi hilo tumeliona tutaenda kulifanyia kazi,” amesema Matola.