Wakongwe wakemea Kariakoo Dabi kuahirishwa kienyeji

HUKO mtandaoni bado mashabiki wa soka wana hasira kutokana na kuahirishwa kwa pambano la Dabi ya Kariakoo iliyokuwa ipigwe juzi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku baadhi ya wadau wakiwamo wakongwe wa soka waliwaka kwa waliokwamisha mechi kupigwa wakidai wamezingua.

Wapo wanaoamini Simba imezingua kwa upande mmoja kuamua kususia mchezo mapema kabla ya taarifa ya Bodi ya Ligi, huku wengine wakiona Yanga kupitia makomandoo waliingizwa kwenye mtego na watani wao na wakajaa mazima na mechi hiyo kuota mbawa ‘jiooooni’.

Lakini wapo wanaoamini Bodi ya Ligi imezingua kwa kushindwa kusimamia kanuni ambazo imekuwa zikizitumia kuziadhibu klabu na viongozi wake zinapokiukwa kwa kuahirisha mechi bila sababu za msingi zinazokubalika kulingana na kanuni hizo.

Ipo hivi. Pambano hilo la Ligi Kuu liliahirishwa saa chache kabla ya kupigwa Kwa Mkapa kwa kilichoelezwa ni kutokana na kitendo cha makomandoo wa Yanga kuizuia Simba kufanya mazoezi kwenye uwanja huo kama inavyotakiwa kwa mujibu wa kanuni, kabla ya Bodi ya Ligi kutoa taarifa iliyoainisha mechi hiyo itapangiwa tarehe nyingine ya kuchezwa.

Licha ya tangazo hilo, Yanga iliyokuwa wenyeji wa mchezo ilienda uwanjani na kupasha huku mashabiki wachache wakishuhudia.

Mechi hiyo ilitangazwa kuahirishwa huku mashabiki wakiwa wameshakata tiketi na maandalizi kwa jumla yakiwa yameshafanyika, ikiwamo Azam TV kujiweka tayari kurusha matangazo ya mechi hiyo kubwa nchini, kitu kilichofanya baadae watoe taarifa yao kusikitishwa na kilichofanyika.

Ukiacha Azam, wadau mbalimbali wamekuwa wakijadili uamuzi uliofanywa na Bodi ya Ligi inayodaiwa kujikanganya katika taarifa yao juu ya kuahirishwa kwani ilienda kinyume na kanuni zinazoainisha mambo yanayoweza kusababisha mechi kuahirishwa.

Kanuni namba 34: Kuahirisha Mchezo kifungu cha 1-5 kimeweka bayana mambo yanayoweza kuahirisha mchezo ikiwamo; Endapo timu ya Taifa ina mchezo, Endapo timu inashiriki katika mashindano ya Kimataifa na ina muda usiozidi siku tatu (3) kufikia mchezo wa Kimataifa.

Kifungu cha 1.3 kinasema; Sababu ya dharura au/na yenye msingi itakayokubaliwa na TFF au Endapo itatokea matukio yalio nje ya uwezo wa binadamu (force majure) yasiyotarajiwa wala kusababishwa na timu husika ama Endapo wachezaji wasiopungua watatu (3) wa klabu moja wataitwa kushiriki mchezo wa timu ya Taifa.

Kanuni hiyo inaweka bayana, Mchezo wowote ulioahirishwa chini ya kanuni 34(1.1 – 1.3) utapangwa tena katika tarehe itakayoamuliwa na TPLB isipokuwa kama utaahirishwa chini ya kanuni 34(1.4) utachezwa siku inayofuata au muda mwingine wa karibu zaidi kadiri ratiba inavyoruhusu.

Iwapo mchezo ulishaanza na kuvunjika kwa sababu ya matukio ya dharura yasiyotarajiwa wala kusababishwa na timu husika, utapangwa kuchezwa kwa muda uliosalia kuanzia dakika na tukio ulipovunjika ukiwa na wachezaji na waamuzi walewale. Mabao yaliyofungwa na kadi/adhabu walizoonyeshwa wachezaji katika mchezo uliovunjika zitaendelea kuhesabika. Muda wa kuanza mchezo huo na taratibu zitaamuliwa na TPLB.

Taarifa ya maombi ya kawaida ya kuahirisha mchezo ni lazima itolewe kwa maandishi si chini ya siku kumi na nne (14) kabla ya siku ya mchezo, isipokuwa kwa sababu zilizo nje ya uwezo wa binadamu au dharura kubwa.

Ruhusa ya wachezaji wanaoteuliwa kuchezea timu za Taifa za nchi zao na kwa timu za Taifa za vijana chini ya miaka 23 (ishirini na tatu) na miaka 20 (ishirini) itatolewa kwa kufuata sheria za FIFA kwa muda kabla na baada ya mchezo husika.

Katika taarifa ya kuahirishwa kwa mchezo huo inasomeka; Baada ya kupitia taarifa mbalimbali zikiwamo za maofisa wa mchezo na vyanzo vingine, kamati ya saa 72 ilibaini kuwa, Simba wakati inaenda kutumia haki yake ya msingi ya kufanya mazoezi Kwa Mkapa, jaikuwasilina na ofisa yeyote, wala timu wenyeji au mamlaka ya uwanja kuhusu kufanya kwao mazoezi.”

Lakini taarifa hiyo inaeleza kamati ilibaini walinzi ambao baadhi wanafahamika kwa sura ni wa Yanga walizuia basi la Simba kuingia uwanjani kinyume na matakwa ya kanuni 17:45 na kuainishwa kwa Simba kushindwa kufanya mazoezi na matukio mengine ya kiuchunguzi ikazuia mechi.

Hata hivyo, kanuni za kuahirisha mechi na timu kutofanya mazoezi kwenye uwanja husika, kanuni na adhabu zake zimeainishwa, hivyio kuwachefua mashabiki na wadau wakiamini Bodi ya Ligi na TFF kwa jumla wamezingua kuwanyima uhondo wa kuziona Yanga na Simba juzi katika pambano hilo.

Wakili Alex Mgongolwa akizungumzia sakata hilo alisema alishangazwa na maamuzi ambayo Bodi ya Ligi imeyatoa kwani matukio yote mawili hatua stahiki zimejieleza kikanuni lakini zikashindwa kuchukuliwa.

Mgongolwa alisema mchezo huo haukupaswa kuahirishwa kama ilivyofanyika na klabu zilipaswa kuchukuliwa hatua huku akiyaita maamuzi hayo ni batili.

“Kanuni huwa zinatungwa ikiwa na dhamira ili mambo kama haya yanapotokea, ziweze kutoa tafsiri sahihi ya wapi taasisi isimame kwenye kufanya maamuzi na kanuni zina madhara yake,” alisema Mgongolwa na kuongeza;

“Tukirudi kwenye matukio ya jana, yote mawili yaliyotokea kanuni zetu hazikuwa bubu, zimeweka wazi nini tulipaswa kufanya katika kuweka usawa. Timu kufanya mazoezi hiyo ni haki yao na kama ikitokea imenyimwa hiyo haki kulikuwa na kanuni tulipaswa kuzichukua, zipo na zinajieleza.

“Vilevile timu inapogoma kucheza mechi kanuni zetu zinaeleza itachukuliwa hatua gani lakini haya yote mawili yameshindwa kufanyika, kwangu Mimi naona maamuzi yaliyochukuliwa ni batili kwa kuwa hayakuwa na baraka ya kanuni zetu.”

Kwa upande wa Katibu Mkuu wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Selestine Mwesigwa alisema tukio linaweza kutumika kama elimu kwa Bodi ya Ligi na TFF kujipanga na matukio ya namna hiyo yasiendelee kutokea.

“Kiukweli bado sijajiridhisha ni upande upi ulifanya makosa, unajua matukio yote yamekuwa ya haraka sana na maamuzi yamekuwa ya haraka pia,” alisema Mwesigwa na kuongeza;

“Ninachokiona kupitia haya yaliyotokea nadhani yanaweza kutumika kama elimu kwa Bodi ya Ligi na hata TFF kujua ni namna gani tunapaswa kuyaishi mambo kama haya yanapoweza kuja kutokea huko mbele.

“Ligi yetu kufikia hadhi iliyonayo Sasa inatokana na mambo mengi wakiwemo wadhamini lakini pia wakati mwingine tuje kufanya maamuzi kwa kuangalia ustawi wa mashabiki wetu ambao wanaumizwa kwa kuwa walijiandaa kwa muda mrefu kuja kutazama mchezo mkubwa kama huu.”

Hata hivyo, Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia akizungumza kwa kifupi na Mwanaspoti kwa njia ya simu akiwa Misri alisema: “Nipo safarini huku Misri, nisingependa kuingilia maamuzi ya vyombo ambavyo tumevipa mamlaka, lakini maamuzi ya Kamati ni vyema yakaheshimiwa,” alisema Karia.

Mastaa wa zamani wa Simba na Yanga, wamekemea kilichotokea na kuitaka Bodi ya Ligi (TPLB) na Shirikisho la Soka (TFF) na kutaka kuangalia upya kanuni zitakazotoa adhabu kali dhidi ya watu wanaolitia doa soka.

Kiungo mshambuliaji wa zamani wa Tukuyu Stars, Yanga na Taifa Stars, Sekilojo Chambua alisema Bodi na TFF zikae chini kuzipitia baadhi ya kanuni ili kuzifanyia marekebisho ya kulinda hadhi ya ligi.

“Kilichotokea sijakipenda kabisa kwanza kimeumiza mioyo ya wapenzi wa mchezo huo kutoka ndani na nje, ulitarajiwa ungekuwa mchezo mgumu na burudani kwa sababu mbili ya kwanza Simba ilitaka kufuta uteja wa kufungwa mara nne kitu ambacho si cha kawaida kwa hizo timu, la pili zimepishana pointi chache za kuwania ubingwa, hivyo kila timu ingekuwa inapambania pointi tatu,” alisema Chambua na kuongeza;

“Vitu hivi vinatakiwa kukemewa katika klabu hizo ni makomandoo wasiwe na nafasi ya kuingilia vitu ambavyo haviwahusu, huwezi kukutana Manchester United  ikicheza na Liverpool makomandoo wanaingilia mchezo, wanawaachia wahusika, pia Simba kama Kwa Mkapa wanaujua sio mgeni kwao kwa nini wagomee mechi badala yake wangeacha adhabu iwahusu waliofanya ujinga wa kuwazuia.”

Mkongwe mwingine wa Simba, Yanga na Stars, Zamoyoni Mogella alisema jambo la kwanza Bodi na TFF iwaombe radhi mashabiki waliopoteza muda na gharama zao pia ziwekwe adhabu kali za kuepusha ujinga unaofanyika, vinginevyo itakuwa ngumu kukomesha vitendo hivyo.

“Kama tunahitaji soka la kisasa hatuwezi kuendeshwa na imani za kiswahili hiyo ndio sababu ninayoiona kutochezwa kwa mechi hiyo kwa timu zote mbili, pia kama kutakuwepo na kanuni za adhabu kali zitaondoa ujinga huo, vinginevyo hayo mambo yataendelea kujirudi,” alisema Mogella na kuongeza;

“Mechi imeahirishwa kirahisi, ifikie hatua mambo ya  makomandoo wa hizo klabu hizo yawe na mipaka yasiende sehemu ambazo hawatakiwa kuingilia maamuzi yasiyo wahusu na kanuni zielekeze hayo yote.”

Kipa wa zamani wa Yanga, Benjamin Haule alisema:

“Kinachofanyika Simba na Yanga ni cha kukemea hakileti afya ya mpira wa miguu nchini, TFF na bodi ya ligi zithamini mashabiki ambao wana mchango mkubwa wa kuifanya ligi iwe na thamani mbele ya mataifa mengine.”

Beki wa zamani wa Simba na Yanga, Amir Maftah alisema: “Kilichofanyika ni kuwaumiza mashabiki ambao wanapaswa kuombwa radhi, Simba na Yanga kama kioo cha soka, kuna haja ya kutathimini.

Related Posts