Kimenya, Elfadhili wagoma, Juma arejea Prisons

MATOKEO mabaya inayopata Tanzania Prisons, yamewafanya viongozi warudi kwa wachezaji askari Jumanne Elfadhili, Salum Kimenya na Jeremiah Juma waliowaondoa kikosini na kuwapangia majukumu mengine, baada ya kuona uwepo wao utasaidia timu isishuke daraja.

Hata hivyo, inaelezwa wachezaji wawili miongoni mwao, wamegoma kurudi kikosini na kutaka msimamo wa awali uheshimiwe juu yao.

Katika msimamo wa ligi, Prisons ipo nafasi ya 15, imecheza mechi 23 imeshinda nne, sare sita na imefungwa 13 na ina pointi 18, jambo ambalo viongozi wameona hakuna namna zaidi ya kuwarejesha wakongwe hao.

Hadi sasa mchezaji aliyejiunga kambini ni Jeremiah ambaye alitajwa atakaa nje kwa muda mrefu kutokana na kusumbuliwa na majeraha, ingawa nyuma ya pazia ilikuwa hahitajiki kikosini, huku Elfadhili na Kimenya ikielezwa wameweka msimamo wa kuendelea na majukumu ya sasa na siyo kurudi kucheza.

Chanzo cha ndani kutoka Prisons kilisema kocha Amani Josiah alizungumza na viongozi ili kuwarejesha wachezaji hao aliowaona wana kitu cha kuisaidia timu isishuke.

“Kocha alisema matatizo baina ya wachezaji hao na viongozi hayamhusu, kikubwa kinachotakiwa ni kuinusuru timu isishuke daraja na alipitia rekodi za Juma akaona ni mshambuliaji ambaye ana uwezo wa kufunga,” kilisema chanzo hicho.

Alipotafutwa Jeremiah ambaye msimu wa 2016/17 alimaliza na mabao 13 ili kuthibitisha hilo, alisema hawezi kuzungumza chochote na kama yupo kambini ataonekana uwanjani.

Msimu kadha timu hiyo imekuwa ikiponea chupuchupu kushuka daraja ikiwamo wa 2021/22 na katika mechi 30 ilishinda saba, sare nane, ilifungwa 15, pointi 29 ilisalia Ligi Kuu kwa kucheza mtoano (playoff).

Prisons iliyong’olewa katika michuano ya Kombe la Shirikisho kwa penalti 3-2 na Bigman baada ya dakika 90 kumalizika kwa sare ya 1-1,  sasa imesaliwa na mechi saba za Ligi Kuu ambazo inapaswa kupata matokeo mazuri ili kujiokoa kwa mara nyingine kwenda Ligi ya Championship.

Related Posts