Mwambusi aitangazia vita Yanga | Mwanaspoti

KOCHA wa Coastal Union, Juma Mwambusi amesema wanahitaji nidhamu bora ya kiuchezaji wakati kikosi kikijiandaa kuivaa Yanga Machi 12, kwenye mchezo wa Kombe la FA hatua ya 32 utakaopigwa Uwanja wa KMC Mwenge.

Akizungumza na Mwanaspoti, Mwambusi alisema baada ya mchezo wao wa mwisho wa Ligi Kuu Bara waliolazimishwa suluhu dhidi ya Dodoma Jiji, tayari walianza maandalizi ya michuano hiyo kwa lengo la kuhakikisha wanasonga mbele hatua inayofuata.

“Hii ni michuano mingine na malengo pia ni lazima yawe na utofauti, mechi za mtoano siku zote huwa ni ngumu kwa sababu kila mpinzani unayecheza naye anakuwa na tahadhari anayoichukua, ni mchezo mgumu sana ila tumejipanga kuleta ushindani.”

Kocha huyo wa zamani wa Mbeya City, Yanga, Ihefu na Singida United aliyejiunga na kikosi hicho Oktoba 23, 2024 akichukua nafasi ya Mkenya David Ouma, alisema changamoto kubwa inayomkabili ni kushindwa kutumia vyema nafasi wanazotengeneza.

“Tunatengeneza nafasi nyingi ila tunashindwa kuzitumia vizuri, hii ni tatizo linaloweza kuitokea timu au washambuliaji wowote, kama nilivyosema hapo mwanzoni tunaenda kucheza na wapinzani waliokuwa bora ila tumejipanga kukabiliana nao.”

Timu hiyo inaenda kukabiliana na Yanga ikiwa haijashinda michezo sita mfululizo ya Ligi Kuu Bara tangu mara ya mwisho ilipoifunga JKT Tanzania mabao 2-1, mechi iliyopigwa kwenye Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha Februari 7, mwaka huu.

Katika michezo hiyo sita ambayo timu hiyo imecheza bila ya ushindi wowote, imetoka sare minne na kuchapwa miwili na safu yake ya ushambuliaji ya kikosi hicho haijafunga bao lolote, huku ikiruhusu nyavu zake kutikiswa wavuni mara tano.

Coastal inaingia katika mchezo huo baada ya kuitoa Stand FC ya Masasi hatua ya 64 bora kwa kuifunga mabao 4-0, huku kwa upande wa Yanga ambao ndio mabingwa watetezi wanakumbukumbu nzuri ya kuicharaza Copco FC ya jijini Mwanza kwa mabao 5-0.

Related Posts