TFF yafungia viwanja vitatu kwa kutokidhi vigezo

Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) limetangaza kufungia viwanja vitatu kutumika kwa michezo ya ligi kutokana na kukosa vigezo vya kikanuni na kisheria vinavyotakiwa kutumika kwa Ligi Kuu.

Viwanja vilivyokumbana na rungu hilo ni Jamhuri, Dodoma unautumiwa na Dodoma Jiji FC, CCM Kirumba, Mwanza unaotumiwa na Pamba Jiji FC, na Liti, Singida unaotumiwa na Singida BS.

Taarifa iliyotolewa leo Jumatatu Machi 10, 2025, na Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Cliford Mario Ndimbo imesema miundombinu ya viwanja hivyo haikidhi masharti yaliyowekwa katika Kanuni ya Leseni za Klabu.

Hivyo, timu zinazotumia viwanja hivyo kwa michezo yao ya nyumbani zitalazimika kutumia viwanja vingine vinavyokidhi vigezo hadi marekebisho yatakapofanywa na TFF kufanya ukaguzi upya.

TFF imezikumbusha klabu zote kuendelea kuboresha miundombinu ya viwanja ili kuhakikisha michezo inachezwa katika mazingira salama na yanayokidhi viwango vya kitaifa na kimataifa.

Related Posts