BAADA ya JKT kuifunga Vijana ‘City Bulls’ kwa pointi 70-55, kocha wa timu hiyo, Chris Weba amesema pointi 25-13 walizopata katika robo ya tatu, ndizo zilizowapa ushindi.
Mchezo huo uliokuwa unasubiriwa na mashabiki wengi wa Ligi ya Kikapu Mkoa wa Dar es Salaam, ulipigwa kwenye Uwanja wa Donbosco Oster bay.
Akiuzungumzia mchezo huo, alisema ulikuwa mzuri na wa kupendeza katika robo zote nne.
Hata hivyo, alisema City Bulls ilicheza vizuri robo mbili za kwanza, licha ya wao kuongoza kwa pointi 10-8, 17-15.
“Baada ya kuona City Bulls inaweza ikatusumbua, tulibadilisha mfumo wa ufungaji kwa kufunga nje ya duara la eneo lao na tuliongoza kwa pointi 25-13 robo ya tatu,” alisema Weba.
Katika mchezo huo, Jonas Mushi alifunga pointi 15 akifuatiwa na Baraka Sadiki aliyefunga 13, huku kwa City Bulls, Fotius Ngaiza aliongoza kwa kufunga pointi 12.
Katika mchezo mwingine uliochezwa uwanjani hapo, Mchenga Stars iliifunga ABC kwa pointi 71-64, katika mchezo uliokuwa mgumu.
Mchenga iliongoza robo ya kwanza kwa pointi 19-15, 20-22, 10-16, 20-11.
Kwa wanawake, Tausi Royals iliichapa bila huruma Kurasini Divas vikapu 108 kwa 32.