SINGIDA Black Stars inapiga hesabu kali za kumbeba winga wa Al Hilal, Jean Claude Girumugisha ili atue katika kikosi hicho kuchukua nafasi ya Victor Adebayor waliye mbioni kumsitishia mkataba alionao mwishoni mwa msimu huu.
Adebayor aliyeanza kuitumikia timu hiyo mara dirisha dogo la usajili lilipofunguliwa Desemba mwaka jana, ameshindwa kuonyesha makeke wala kupenya katika kikosi cha kwanza, jambo linalowafanya mabosi wa klabu hiyo kufikiria kumsitishia mkataba wa miaka miwili alionao kwa sasa.
Mwanaspoti linafahamu, sababu kubwa ya kutafutiwa mrithi ni matarajio makubwa waliyokuwa nayo mabosi hao kwa winga huyo kutokukamilika.
Ndio maana wakatafuta mbadala wake mapema ili kuona kama wanaweza kupata saini ya Mrundi huyo, mwenye mkataba wa miaka mitatu ya kuitumikia Al Hilal.
Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti kuwa; “Jina la winga huyo liko mezani likijadiliwa ili kuona jinsi gani tutamng’oa kwa Waarabu hao na kuwa naye msimu ujao.”
Winga huyo aliyeichezea Al Hilal kwa msimu mmoja, anaipa Singida kibarua cha kununua mkataba wa miaka miwili iliyosalia katika klabu hiyo ya Sudan inayotumia Mauritania kama nyumbani kwa sasa.
Ikumbukwe kuwa Al Hilal ilicheza na Yanga katika hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika zikiwa Kundi A na kila moja kupigwa nyumbani, Yanga ililala 2-0 na kwenda kushinda 1-0 ugenini.
Katika mechi ya kwanza ya jijini Dar es Salaam, Yanga ikilala 2-0, Jean Claude alicheza dakika 61 tu na alionekana kumpa wakati mgumu beki Kibwana Shomari aliyekuwa akikabana naye kwa muda wote.
Baada ya mechi hiyo Singida, ilimuona staa huyo ambaye amekuwa akipata muda mwingi wa kucheza katika kikosi cha kwanza tangu alipojiunga na timu hiyo ya Sudan.
Katika mechi sita ambazo Al Hilal ilicheza, amecheza tano huku akifisha dakika 294, katika mechi moja ambayo hakucheza dhidi ya Mazembe, kocha alipanga wachezaji ambao hawapati nafasi kwani tayari alishajihakikishia kutinga robo fainali ya michuano hiyo.
Singida inayosifika kwa kusajili mastaa wengi hadi wengine ikiwatoa kwa mkopo katika timu nyingine, inashika nafasi ya nne katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 44 kupitia mechi 23 ilizocheza.