Kinachofanyika udhibiti athari za tumbaku Tanzania

Dar es Salaam. Wakati kila mwaka watu 21,800 wakipoteza maisha nchini kwa maradhi yatokanayo na uvutaji wa tumbaku, Serikali imeeleza hatua zinazochukuliwa kudhibiti athari za zao hilo.

Kwa mujibu wa taarifa za uwekezaji na udhibiti wa tumbaku Tanzania (Investment Case for Tobacco Control in Tanzania), kila mwaka vifo vitokanavyo na matumizi ya tumbaku huchangia asilimia sita ya vifo vinavyotokea Tanzania.

Kwenye matibabu, kwa mwaka Sh110 bilioni hutumika kushughulikia maradhi yatokanayo na tumbaku huku hasara ya Sh337 bilioni ikipatikana eneo la kazi kwa kupoteza nguvu kazi, hiyo ni kwa mujibu wa ripoti hiyo ya tumbaku.

Tanzania ni mwanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO) na ilisaini mkataba wa kimataifa wa kudhibiti matumizi ya tumbaku (WHO FCTC) ambao unatazamwa kama chombo cha kimataifa kilichoainisha hatua za kisheria na wajibu wa nchi wanachama katika kukabiliana na tatizo la uvutaji wa sigara.

Mkataba huo wa WHO -FCTC ulilenga kuweka msingi kwa ajili ya hatua zote; kupunguza mahitaji na usambazaji wa tumbaku na ukaweka maelekezo ya kisera katika utekelezaji wake katika hatua zote.

Leo Jumatatu Machi 10, 2025, akizungumza na Mwananchi, Mkurugenzi wa Bodi ya Tumbaku Stanley Mnozya amesema Tanzania inafanya kazi kwa kushirikiana na WHO katika maeneo yenye madhara ya afya kwa binadamu katika sekta ya tumbaku.

Amesema msisitizo wanaoutoa kwa wakulima ni kutovuta tumbaku, bali zao hilo litumike kwa biashara.

“Tunalima ili kusafirisha kupata fedha za kigeni na sio kuvuta, kwa mwaka jana zao hili limeongoza kwa kuingiza fedha za kigeni, asilimia 98 ya tumbaku yetu tunasafirisha, inayobaki ni kwa ajili ya viwanda vyetu vya sigara na hata sigara zikitengenezwa zinasafirishwa kwenda nje,” amesema.

Kuhusu hatua za kulinda mazingira, Mnozya amesema Serikali imepiga marufuku matumizi ya miti kukaushia mkaa, akisema wakulima walikuwa wakikata misitu kupata kuni kukaushia tumbaku na kusambaza majiko ya kutumia majani ya tembo.

“Kwa Wilaya ya Chunya mkoani Mbeya pekee tumekausha tani zaidi ya milioni moja kwa kutumia majani ya tembo, tumepiga marufuku ukataji wa miti kukaushia tumbaku,” amesema.

Pia amesema Serikali imewekeza katika ujenzi wa majiko ya kukaushia tumbaku kwa kuwapatia wakulima hao majiko.

“Serikali imetoa ruzuku tunatengeneza majiko ambayo mkulima haingizi gogo bali matawi, katika kukausha tumbaku tutaanza kutumia makaa ya mawe pamoja na umeme. Zipo mbegu tumeingiza nchini ambazo haziitaji miti kwa ajili ya ukaushaji bali kutumia hewa na jua lengo kupoteza aina ya tumbaku inayokaushwa kwa kuni,” amesema.

Mkurugenzi huyo amesema Tanzania haipingani na matakwa yeyote ya WHO, lakini changamoto iliyopo ni shirika hilo kutoendana na nchi mbalimbali ya takwa la kushughulikia maeneo yenye changamoto kwa zao hilo pekee.

Amesema ni ngumu kufuta zao la tumbaku bila kuwapa zao mbadala wakulima, akisisitiza mbadala wa zao la tumbaku ni muhimu umpatie faida mkulima.

“Huwezi kufuta tumbaku bila kumpa njia mbadala mkulima, upatikane mbadala wa zao la tumbaku ambao umefanyiwa utafiti na unampa faida mkulima, kuna kikao cha nchi za Kusini mwa Afrika na Mashariki kuanzia Machi 18 tutafanya kikao na tutatoa msimamo wa Tanzania katika zao la tumbaku,” amesema.

Mnozya amesema kwa mwaka jana Serikali iliingiza fedha za kigeni (Dola milioni 484) huku wakulima wakipata Sh724 bilioni kwa kuuza zao hilo na halmashauri zikipata Sh23 bilioni kama ushuru.

Katika kulinda afya ya wananchi, Aprili mwaka jana Naibu Waziri wa Afya Dk Godwin Mollel alisema tayari bunge limepitisha Sheria ya Udhibiti wa Tumbaku “The Tobacco Products (Regulation) Act, 2003” ambayo imetoa katazo la uvutaji wa sigara hadharani.

Dk Mollel amebainisha Jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa Tumbe, Amour Khamis Mbarouk aliyeuliza ni lini Serikali italeta Sheria ya Kuzuia uvutaji wa sigara na mazao mengine hadharani.

Dk Mollel alisema sheria hiyo imezuia matangazo ya tumbaku na bidhaa zitokanazo na tumbaku kwenye maeneo ya umma, ikiwemo vyombo vya habari, billboards na kwenye matamasha.

Sheria hiyo inawataka wamiliki wa maeneo ya umma kutenga vyumba au maeneo maalum ya kuvutia ili kuwalinda wasiotumia bidhaa za tumbaku.

Mkulima wa tumbaku, Kisiriga Swalehe wa Malumba Amcos Kijiji cha Mabama wilaya ya Uyui mkoani Tabora amesema ukinzani uliopo wa sheria katika kilimo cha zao la tumbaku unapaswa kuangaliwa kwani wakulima wanalitegemea zao hilo.

“Kwa halmashauri ya Uyui zaidi ya Sh2 bilioni zilikusanywa kama ushuru wa zao la tumbaku, na ndio wananchi tunalitumia zao hili kukuza uchumi. Kwa sababu wanasema tumbaku inaharibu mazingira, Serikali ingetengeneza maeneo ya kukausha tumbaku kwa umeme na makaa ya mawe,” amesema.

Kwa takwimu za WHO, tumbaku husababisha nusu ya vifo kwa watumiaji wake.

Kutokana na uvutaji wa tumbaku kila mwaka watu milioni nane hufariki, ikikadiriwa watu milioni 1.3 hupoteza maisha wakiwa wavutaji wa pili.

Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC) kinaeleza athari zitokanazo na uvutaji wa tumbaku ni saratani, kiharusi, magonjwa ya moyo, magonjwa ya mapafu, kisukari aina ya pili na athari katika mfumo wa uzazi.

Related Posts