Mwanakwaya auawa akienda kanisani | Mwananchi

Shinyanga. Mwanakwaya Agatha Daniel (32) ameuawa kwa kukatwa mgongoni na mkono wa kulia kwa kitu chenye ncha kali wakati akienda kanisani.

Mwanakwaya huyo, mkazi wa Mtaa wa Bugayambelele katika Manispaa ya Shinyanga, aliuawa jana, saa 12:30 alfajiri wakati akiwa njiani kuelekea kanisani.

Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kenedy Mgani, amesema mwanakwaya huyo alipatwa na mkasa huo Machi 9, 2025, katika eneo la Mtaa wa Sido, watu waliofanya tukio hilo walikimbia.

Kwa mujibu wa Kamanda Mgani, mwanakwaya huyo baada ya kushambuliwa alipewa msaada na wasamaria wema. Hata hivyo, alipoteza maisha wakati akipatiwa matibabu.

Kamanda Mgani amesema wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini aliyehusika na kitendo hicho cha kikatili, ambacho kimesababisha kifo cha mwanamke huyo, ili hatua kali za kisheria zichukuliwe.

“Wapo watu wanatiliwa mashaka, hatuwezi kuwataja kwa sasa, bado hatujawakamata na uchunguzi unaendelea ili kubaini nyuma ya hili tukio kulikuwa na nini, kutokana na kumfuatilia huyu mama wakati akienda kanisani,” amesema Kaimu Kamanda Mgani.

Mwenyekiti wa Mtaa wa Sido Buhangija, Emmanuel Kayange, amesema alipata taarifa za tukio hilo jana saa moja asubuhi kutoka kwa wapita njia, ambapo alifika kwenye eneo la tukio na baadaye kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi.

Amesema tukio hilo limewasikitisha kutokana na mwanamke huyo kufanyiwa ukatili mkubwa kwa kuchomwa kisu maeneo mbalimbali ya mwili wake.

Kayange amesema wanalaani tukio hilo na wameliomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina ili kubaini watu waliohusika na kuwachukulia hatua kali za kisheria, kukomesha matukio kama hayo.

Machi 7, 2025, Askofu wa Kanisa la AICT Shinyanga, Zakayo Bugota, akiwa kwenye kongamano la wanawake wa makanisa ya CCT, aliwaomba waumini waendelee kuliombea Taifa ili Mungu aliepushe na matukio ya kikatili, likiwemo la mtu mwenye ualbino aliyekutwa amefariki ndani na kufungiwa mlango kwa nje.

Related Posts