NGULI wa zamani wa Taifa Stars, Jella Mtagwa alifariki dunia juzi jijini Dar es Salaam baada ya kuteseka kitandani kwa miaka 20. Tunarudia sehemu ya mahojiano yake na Mwanaspoti akiwa kitandani nyumbani kwake Mei 27, 2019. “Acheni Mungu aitwe Mungu.” Hiyo ni kauli ya aliyekuwa nahodha wa Taifa Stars, Mtagwa iliyoshiriki fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon) mwaka 1980.
Jellah anasema ameteseka kwa maradhi kwa miaka 15 mfululizo (hii ilikuwa mwaka 2019), mkewe Mboni Ramadhani na watoto wake walikata tamaa, lakini Mungu amemsimamia.
Anasema anatamani kunyanyuka na kutembea, lakini miguu haina nguvu siyo Jellah yule aliyekuwa beki na nahodha tegemeo wa Taifa Stars kwa miaka 10 mfululizo tangu mwaka 1974.
Mkewe anakumbuka ilikuwa mwaka 2004 ambapo waliletewa taarifa kuwa Jellah amedondoka barabarani.
“Mzee alikuwa na nguvu vizuri tu, aliondoka nyumbani kwenda Kisutu sokoni kwenye shughuli za kawaida,” anasimulia Mboni.
Anasema wakiwa katika hekaheka za kufuatilia, mara walimuona akiletwa nyumbani na watu waliomsaidia, lakini akionekana kuwa mgonjwa.
“Tulimpeleka hospitali ambako alipimwa na kugundulika ana presha na tatizo la kupooza mwili, alianza matibabu, lakini hali yake ilizidi kuwa mbaya, alipopimwa zaidi ikaonekana pia ana tatizo la kisukari,” anasema.
Wakati mkewe akisimulia hayo, Jellah alikuwa akimsikiliza kwa makini na kutikisa kichwa, huku akijitahidi kuonyesha tabasamu hafifu ambalo lilimezwa na hali ya ugonjwa unaomkabili.
Licha ya kuumwa kwa muda mrefu, Jellah hakupoteza kumbukumbu, alikumbuka namna alivyojitoa katika timu ya Taifa, anasema asilimia 80 ya maisha yake yalikuwa mpira, lakini haukumnufaisha.
“Hata wanangu walikuwa hawanifahamu wakati ule, sikupata muda wa kuwa nao, muda mwingi nilikuwa kambini ndani ya mwezi mmoja, kama nilikaa nyumbani sana basi ni siku tano, nyingine zote nakuwa kambini au katika mechi.
“Muda mwingi niliutumia kwenye mpira kama sio Stars, basi Yanga au Pan African ambako nilicheza baada ya kuondoka Yanga,” anasema.
Anasema maisha yake ya soka yalianzia Shule ya Msingi Mwembesongo mkoani Morogoro kisha akaendeleza kipaji chake akiwa Shule ya Sekondari Morogoro.
Akiwa Morogoro Sekondari ndipo alipokutana na Leodeger Tenga, rais wa zamani wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF – yuko naye kwenye picha kubwa) aliyekuwa akisoma Kibaha na walikutana kwenye mashindano ya shule.
Anasema alijiunga na Yanga baada ya kuonekana katika michuano ya Kombe la Taifa. “Kocha wa Yanga wakati ule (Tambwe Leah) alikuwa na nguvu, alitaka kuwafukuza wachezaji wanne, wengine tukagoma, hivyo sote tukaingizwa katika mkumbo ule. Siku tunafukuzwa, mashabiki walijaa Jangwani kuona kama ni kweli. Kocha akatamka kwamba tusipoondoka sisi basi yeye atarudi kwao Zaire (sasa DRC), alikuwa na nguvu hivyo tukafukuzwa na kwenda kuanzisha Pan African,” anasimulia.
“Kila mchezaji wa Taifa Stars aligangamala, kwani mmoja akicheza vizuri, wote wanacheza akiharibu basi ni wote, timu nzima ilikuwa na hamasa kutoka moyoni”.
Anasema walikwenda kuweka kambi Mexico kujiandaa na fainali hizo zilizofanyika Lagos, Nigeria.
Taifa Stars ilipangwa kundi moja na Nigeria, Ivory Coast na Misri timu ambazo zinafanya vizuri mpaka sasa Afrika. “Tungefika mbali kwenye yale mashindano, lakini tulifungwa kwa ushamba, pia kuna mmoja wetu (anamtaja jina) alituhujumu na nilimwambia,” anasema.
Anasema mechi na Nigeria walifungwa 3-1 lakini kwa tabu, ila baadae ikagundulika mmoja wao huyo aliwahujumu.
Amenufaika vipi na mpira?
Pamoja na kujitoa kwa asilimia kubwa ya maisha yake katika kuitumikia Stars, Yanga na Pan African, Jellah anasema alicheza kwa mapenzi na hakupata fedha ambayo leo anaweza kujivunia kuwa imetokana na kipaji chake cha mpira.
Maisha ya Jellah ni ya kawaida ambayo hata nyumba aliyoishi eneo la Manzese, Dar es Salaam, mvua ikinyesha maji yalikuwa yanajaa ndani.
“Natamani kujenga nina kiwanja Mkuranga, lakini kabla ya kuanza ujenzi ndipo nikaanza kuugua, hivyo sijaweza kufanya jambo lolote.”
Miongoni mwa mastaa ambao picha zao zilitumika kwenye stempu ni Jellah ambaye anasema hakujua hata mkataba au makubaliano ya picha yake kutumika kwenye stempu yalifanywa na nani.
“Nilistukia tu picha yangu iko katika stempu, nilianza harakati za kufuatilia kujua, nilikwenda ofisi za FAT (sasa TFF) mara mbili bila mafanikio,” anasema.
Anasema Mwenyekiti wa FAT wakati ule, Said El-Maamry mara ya kwanza alimueleza kwamba, picha yake imetumika kwenye stempu kwa sababu ya kipaji chake.
“Niliondoka lakini sikuridhika, nikarudi tena mara ya pili mwenyekiti akaniambia hulipwi na hakuna chochote unachopewa eti kwa kuwa picha yako imetumika kwenye stempu. Sikunufaika na chochote mpaka leo,” anasema.
Nyumbani kwa Jellah, watoto wake wote wanne wanafuatilia mpira hadi mama yao huku mtoto pekee wa kiume kwenye familia hiyo akifuata nyayo za baba yake.
Familia hiyo yenye haiba ya ucheshi, imehifadhi kumbukumbu za baba yao enzi akiwa mchezaji nyota, lakini wanapata simanzi wanapokumbuka namna walivyopambana kama familia katika kupigania afya ya baba yao.
Binti wa Jellah, Mariam Mtagwa anasema ilifikia mahali walikata tamaa ya kuendelea kumuona mzee wao akiwa hai.
“Baba hakuwa na bima ya afya kwa muda mrefu tangu apatwe na maradhi, miaka minne iliyopita ndipo tulipofanikiwa kumpatia bima ya afya,” anasema.
Anasema mwanzoni alipoanza kuugua, kuna msamaria mwema ambaye hawakumtaja jina alijitolea kugharamia matibabu yake katika Hospitali ya Agha Khan.
“Afya ya mzee ilianza kuimarika, lakini siku moja ilibadilika ghafla, familia hatukuweza kumpeleka Agha Khan, hivyo tukampeleka Mwananyamala.
“Ilikuwa siku ngumu mno kwetu, baba alikuwa haelewi chochote, tulihangaika usiku kucha, hadi asubuhi ilitugharimu Sh600,000 za matibabu, alfajiri saa 11 ndipo kwa mbali akaanza kuonyesha matumaini.
“Hali ile ilitufunza jambo kwamba, kama tusingekuwa na kiasi kile cha fedha, huenda leo tungekuwa tunazungumza mengine,” anasema.
Anasema familia ilikuwa ikimhudumia baba yao kwa kujichangisha ili kupata matibabu kwani kwa miaka 11, matibabu ya Jellah yalikuwa ya kulipia fedha taslimu.
“Tulipambana hadi hapa mzee alipofikia. Mbali na presha na kiharusi, kisukari nacho kikaanza kumtesa zaidi, hasa kwenye vyakula, ilitubidi kuwa makini sana ili kumuona mzee anaendelea kuishi,” anaeleza.
“Simba na Yanga ilikuwa kama dini. Ilikuwa ngumu kutoka huku kuhamia huku.” Jellah anasema katika maisha yake ya mpira alimpenda sana mshambuliaji nyota wa Simba enzi zao, Zamoyoni Mogella. “Mogella alikuwa na akili ya mpira, nakumbuka kuna bao alitufunga katikati ya uwanja wakati ule nacheza Pan.”
Alivyodumu miaka 10 akiwa nahodha
Jellah anasema alijitunza kwa kuepuka anasa akiwa na Stars, Yanga na Pan. “Starehe yangu ilikuwa kwenda Makwizi (bendi ya muziki) na mke wangu basi, lakini kipindi kingine chote nilikuwa mazoezini na kambini.” Apumzike kwa amani Jella Mtagwa ambaye jana jioni alipumzishwa mjini Morogoro.