Simanjiro. Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amekemea kitendo cha wazazi na walezi wanaowazuia watoto wao wa kiume kwenda shule, badala yake kuwageuza wachungaji wa mifugo.
Amesema nyakati hizi si za wazazi kupuuzia elimu kwa watoto wao badala yake wawe mstari wa mbele kuwahimiza kuipenda.
Sendiga amesema hata watoto wa kike nao wananyimwa fursa ya kupata elimu na badala yake huozeshwa na wazazi wao kwa lengo la kujipatia mahali.
Ameyasema hayo leo Ijumaa Mei 17, 2024 katika Kijiji cha Emboreet wilayani Simanjiro baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa kituo cha mafunzo, ujuzi na malezi kwa wasichana.
Kituo hicho kinajengwa kwa ufadhili wa taasisi ya ECLAT Foundation ikishirikiana na taasisi ya Upendo kutoka Ujerumani.
Ujenzi huo unaoanza kesho, utagharimu Sh1.6 bilioni hadi kukamilika kwake.
“Watoto wa kiume wapatiwe elimu wasichungishwe mifugo wangali wadogo na watoto wa kike wasiozeshwe wangali wadogo ila wapatiwe elimu,” amesema Sendiga.
Mkuu huyo wa mkoa pia amekemea vitendo vya ukatili ambavyo vinaendelea kuripotiwa kutokea wilayani humo ikiwemo ukeketaji, ubakaji, ulawiti na vipigo kwa wanawake na watoto.
Lakini ameipongeza familia ya Peter Toima kwa uzalendo walioufanya na kuwa mfano wa kuigwa kwa kutoa eneo kwa ajili ya ujenzi wa chuo hicho, kinachokwenda kuwa mkombozi kwa wahitaji.
Kwa upande wake, Toima ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Manyara, amesema ECLAT imetengeneza miundombinu mbalimbali katika sekta ya elimu.
Hivyo, amesema shirika hilo limejenga na kukarabati shule za msingi na sekondari kwenye wilaya za Simanjiro na mikoa ya Arusha, Mtwara na Lindi.
Mkazi wa Emboreet ambaye ni mfugaji, Naishok Mollel amesema Toima amekuwa alama kubwa ya elimu katika Wilaya ya Simanjiro.
Amesema jamii ya wafugaji wamekuwa na mwamko mkubwa wa kupenda elimu kutokana na miundombinu inayotengenezwa na Toima.