WHO yaonesha hofu juu ya ukosefu wa misaada Gaza – DW – 17.05.2024

Shirika hilo limeeleza kuwa operesheni ya kijeshi katika mji wa Rafah unayaweka hatarini maisha ya watu wengi hasa wagonjwa. 

Msemaji wa WHO Tarik Jasarevic amesema hatua ya Israel kufunga kivuko cha mpaka wa Rafah cha kuingiza msaada ndani ya Gaza kumesababisha kile alichokiita “hali ngumu.”

Soma pia:  Misaada ya kiutu itaanza kuingia tena Gaza

Jasarevic ameeleza kuwa, vifaa vya mwisho vya matibabu walivyovipokea ilikuwa kabla ya Mei 6. Ameongeza kuwa wasiwasi mkubwa hasa ni kuhusu ukosefu wa mafuta yanayohitajika ili kuhakikisha vituo vya afya vinavyotoa huduma za matibabu na hospitali zinafanya kazi bila kikwazo.

“Usipokuwa na mafuta, jenereta haziwezi kufanya kazi, na usipokuwa na umeme, watu ambao wanahitaji uangalizi maalum hospitali watakuwa katika hatari. Huwezi pia kuwafanyia wanawake wajawazito upasuaji, huwezi kufanya upasuaji wowote na huwezi pia kuwahudumia watoto wachanga.”

Idadi ya vifo na majeruhi yaongezeka Ukanda wa Gaza

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Hospitali za Gaza zinahitaji hadi lita milioni 1.8 ya mafuta kila mwezi ili kuziwezesha kuendelea kufanya kazi.

Msemaji huyo wa WHO amesema kiasi lita 159,000 za mafuta ndio zimeingia Rafah tangu kufungwa kwa mpaka huo kati ya Gaza na Misri na kwamba hospitali 13 tu kati ya 26 katika eneo zima la Palestina ndizo zinazofanya kazi.

Wanajeshi wa Israel walichukua udhibiti wa mji wa Rafah mnamo Mei 7 kama sehemu ya oparesheni yao dhidi ya kundi la wanamgambo la Hamas.

Jeshi hilo lilifunga kivuko cha mpaka cha Rafah ambacho kinatajwa kuwa muhimu kwa usafirishaji wa bidhaa na misaada ya kibinadamu ndani ya Gaza.

Waandamanaji washambulia malori ya kubeba misaada Gaza

Wapalestina waliojeruhiwa katika shambulio la Israel wakitibiwa kwenye hospitali ya Al-Shifaa
Wapalestina waliojeruhiwa katika shambulio la Israel wakitibiwa kwenye hospitali ya Al-ShifaaPicha: Mahmoud Essa/AP/picture alliance

Wakati hayo yanaripotiwa, jeshi la Israel limesema leo kuwa raia kadhaa wa nchi hiyo wameliteketeza moto lori lililokuwa limebeba msaada katika eneo la ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu.

Vyombo vya habari vya ndani vimeripoti kuwa walowezi wa Israel ndio waliohusika na shambulio hilo dhidi ya lori, na kwamba dereva pamoja na wanajeshi kadha wa Israel walijeruhiwa katika mshikemshike huo.

Shambulio hilo dhidi la lori la msaada limetokea karibu na Kokhav Hashahar, makaazi ya walowezi wa kiyahudi katikati mwa ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu na Israel tangu mwaka 1967.

Soma pia:  Israel yajitetea mbele ya mahakama ya haki ICJ

Mnamo siku ya Jumatatu, mamia ya watu walizuia na kuharibu msafara mwengine wa malori yaliyokuwa yamebeba msaada kuelekea Gaza.

Licha ya tahadhari iliyotolewa na Umoja wa Mataifa kuhusu kitisho cha njaa, mamlaka ya Israel imezuia kuingizwa kwa misaada ya kibinadamu ndani ya Gaza katika kipindi cha zaidi ya miezi saba ya vita kati yake na Hamas.

Kiwango kidogo tu cha msaada ndio kimeingia kupitia kivuko cha Kerem Shalom kusini mwa Gaza huku kivuko cha Rafah kikifungwa kabisa tangu jeshi la Israel lilipochukua udhibiti wa eneo hilo wiki iliyopita.

 

 

Related Posts