HENOCK Inonga ameomba udhuru aende Ufaransa kupumzika, lakini kuna machale yanawacheza viongozi wa Simba juu ya uamuzi wa beki huyo kufosi kuondoka hasa wakikumbuka awali kabla ya kutua Msimbazi ilibaki kidogo atue Jangwani.
Mkongomani huyo ameomba kuondoka licha ya kwamba ana mkataba wa mwaka mmoja huku klabu inayohusishwa nae ikiwa ni FAR Rabat ya Morocco, lakini kuna watu wanahisi harufu ya Yanga hata Azam FC kwa mbaali, ndiyo maana wamechukua tahadhari kubwa.
Viongozi wamemsisitiza Inonga kama ana ofa yoyote na anataka kuondoka klabuni hapo asisite, aipeleke mezani watamaliza fasta dili hilo ili asepe lakini si yeye atake kulipa mwenyewe na kuondoka kimyakimya.
Inonga ambaye amebakiza mwaka mmoja kwenye mkataba wake na Simba, anataka kuachana na klabu hiyo mwisho wa msimu huu na Mwanaspoti linafahamu mabingwa wa Morocco FAR Rabat inataka kumchukua ikielezwa alishamalizana nao miezi kadhaa iliyopita, lakini hata Simba wenyewe kuna baadhi wanataka dili la FAR likija mezani litupwe kule kwa madai imeanza kumhadaa mchezaji na kumtoa mchezoni mapema.
FAR Rabat inataka kujenga ukuta wao mpya na hesabu zao Inonga ni beki ambaye atawapa ubora mkubwa baada ya kutamani kumsajili mara mbili kwa nyakati mbili tofauti bila mafanikio.
Mwanzoni mwa miaka ya 2000, aliyekuwa beki tegemeo wa Simba, Ramadhani Wasso aliwahi kuomba kutimkia Arabuni lakini akakunja kona kali na kuibukia Yanga jambo lililoibua tafrani klabuni.
Hivyo, Simba wanataka kujiridhisha ofa ambayo Inonga anayo ni ya nje ya nchi kweli na si ujanja ujanja na kushangaa anaibukia Yanga kuziba pengo la Bakari Mwamnyeto au Azam.
Taarifa kutoka ndani ya Simba ni kwamba mabosi wa Simba bado wanahisi kuna kitu kinaendelea chinichini kwani kiwango cha beki huyo kimeyumba sana tena katika michezo muhimu waliyokuwa wakimtegemea hadi kufikia hatua ya kuamua akae benchi kabisa.
Wanadhani alikuwa akipumzika kijanja kutokana na sababu anazozijua yeye ingawa wao wanahisi kuna kitu ambacho chanzo chake ni klabu za ndani ya nchi na si FAR Rabat.
Ingawa wapo ndani ya Simba wanaodai pia baada ya kutoka Afcon aliambiwa na ‘watu wake’ asikiwashe sana asije akapata majeraha yatakayoathiri anakokwenda.
Hata katika mchezo uliopita dhidi ya Yanga wa ligi waliofungwa mabao 2-1 wanadai hakucheza kwenye ubora wake na hata majeraha aliyoyapata hadi akatolewa ni ya kawaida ambayo kwa wanavyomjua angeweza kuendelea kukiwasha. “Hakuna shida Yanga inaweza kutufunga lakini kwa mechi ile kama tungekuwa kamili kama ambavyo mchezo ulivyoanza nadhani isingekuwa rahisi kupoteza na alipotoka Inonga tu mambo yakageuka. Jinsi anavyotaka kuondoka sasa, acha kwanza tujiridhishe juu ya ofa aliyonayo, mpira wetu tunajuana,” alisema bosi mmoja wa juu ndani ya Simba.
Taarifa zaidi kutoka Morocco zinasema safari ya Inonga kwenda Ufaransa ni anakwenda kukutana na mabosi wa klabu moja inayotaka kumsajili mwisho wa msimu huu.
Mabosi wa klabu hiyo ambao wanatoka Afrika Kaskazini wameshtukia mtego kama wakimwita beki huyo nchini kwao, basi Simba itanasa kila kitu juu ya safari hiyo kwa kutazama namna alivyoingia ndani ya nchi nyingine kupitia pasi yake ya kusafiria.
Hesabu za mabosi hao wanataka bora Inonga pasi yake ya kusafiria isome aliingia Ufaransa kama ambavyo ameomba ruhusa Simba kisha wakutane na kukubaliana namna ya kukamilisha dili hilo, pia pande hizo mbili iwe rahisi kwao kwa Inonga kutokea DR Congo huku Waarabu hao wakitokea nchini kwao.
Simba tayari wako mezani wakisaka kocha mpya pamoja na kuwasainisha wachezaji wachache wanaotaka kubaki nao msimu ujao, huku wakikimbizana pia na nafasi ya pili kuwania kufuzu Ligi ya Mabingwa Afrika.
Tayari kitakwimu Yanga ameshatawazwa bingwa mpya wa Ligi Kuu Bara msimu huu licha ya kwamba wana mechi tatu mkononi.
Huu ni msimu wa tatu Simba inaukosa ubingwa huku ikipambana kuwania nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi yenye timu 16.
Moja ya sababu zinazoelezwa kuiyumbisha Simba ni pamoja na usajili mbovu na kutokuwa na mipango thabiti ya ndani.
Mwenyekiti wa zamani wa Simba, Hassan Dalali alisema; “Plani za sasa ni kuzunguka Tanzania nzima, kuzungumza na wanachama ili turudishe umoja na kumaliza migogoro, Yanga inafanikiwa kwa sasa, wapo kitu kimoja, penye umoja pana baraka za Mungu.”
“Hakuna kitu kilichoniuma, kama kufungwa mabao 5-1 na Yanga, nilikaa uwanjani hadi saa 4:00 usiku, watu wakawa wananiuliza mzee Dalali vipi mbona upo hapa hadi muda huu, nikawa sielewi,” aliongeza Dalali.