Safari ya benki ilivyomuacha na ulemavu wa kudumu mwalimu

Mufindi.  Aprili 21, 2019 inabaki kwenye kumbukumbu za mwalimu Silvester Lyuvale, siku aliyopata ajali iliyomsababishia ulemavu wa kudumu.

Lyuvale (52), mwalimu wa Shule ya Msingi Kinyanambo katika Halmashauri ya Mji Mafinga, wilayani Mufindi, mkoani Iringa baada ya ajali alikatwa miguu yote miwili. Alipopata ajali hiyo alikuwa Ofisa Elimu Kata ya Wambi.

Akizungumza na Mwananchi, anasema Aprili 21, 2019 alipotoka nyumbani kwenda benki kuchuka fedha za malipo ya wafanyakazi shambani kwake alipata ajali ya kugongwa na gari.

Anasimulia siku alipopata ajali alitoka nyumbani alikokuwa akinywa juisi ya embe iliyoandaliwa na mkewe, ambayo aliifunika akiamini muda si mrefu angerudi kuinywa, lakini ilibaki kwenye glasi kama ilivyo naye akaishia kupata ajali baada ya pikipiki aliyokuwa akiendesha kugongwa na gari.

Anasema baada ya ajali alihisi maumivu makali, lakini hakutambua kuwa atapoteza miguu yote miwili.

“Baada ya ajali nilipoteza fahamu, wasamaria wema walinipeleka Hospitali ya Mji Mafinga, siku hiyo-hiyo nilihamishiwa Hospitali ya Rufaa Iringa. Ilikuwa kati ya saa tatu na saa nne asubuhi,” anasema.

Anasema alipatiwa matibabu kwa mwezi mmoja, akakatwa mguu mmoja na hali bado haikuwa nzuri.

“Nilitakiwa kuhamishiwa hospitali nyingine, nikapelekwa Hospitali ya Ikonda wilayani Makete, mkoani Njombe. Nilitibiwa nikaambiwa natakiwa kukatwa mguu mwingine na ule uliokatwa katika Hospitali ya Rufaa ya Iringa nao unatakiwa kurudiwa kukatwa,” anasema.

Baada ya kukatwa miguu yote miwili anasema alipata nafuu akaruhusiwa kurudi nyumbani.

Anasema alipokatwa mguu wa kwanza hakuwa akijitambua lakini wa pili madaktari walimwambia ataweza kutembea kwa kutumia miguu ya bandia.

“Nilipokea hali hii kwa sababu tangu niliposema huu mguu wa pili pengine unaweza kunisaidia, walisema nao umeharibika mfupa, ulikuwa na ukungu mweusi ndani,” anasema.

“Kwa mapenzi nikasema Mungu kwa sababu umeniokoa siku ile, basi naomba hata huu ukatwe tu ilimradi niweze kuendelea vizuri. Nashukuru hadi sasa naendelea vizuri sijapata shida yoyote tangu nilipokatwa miaka sita sasa,” anasema.

Christina  Nyakunga mke wa mwalimu Lyuvale akimsaidia kuingia ndani akiwa katika kiti mwendo (wheeler chair). Picha na Mary Sanyiwa

Mwalimu huyo anasema alipopata ajali alikuwa Ofisa Elimu Kata ya Wambi, Halmashauri ya Mji Mafinga lakini kutokana na mazingira aliyokuwa nayo aliandika barua kwa mwajiri akiomba kurudi kufundisha katika Shule ya Msingi Kinyanambo.

Kwa mazingara ya sasa anasema ana faraja kwa sababu anaendelea na utendaji kazi ya kufundisha kama kawaida.

“Kwa mazingara ya sasa napata faraja, ombi langu nisaidiwe kitimwendo kinachotumia umeme ambacho kitanisaidia kufundisha kwa urahisi, kwani hiki ninachotumia ni mpaka nikisukume kwa mikono ndipo niandike,” anasema.

Anasema maisha yamebadilika, alikuwa akipata marupurupu lakini sasa hayapo.

Lyuvale anasema kutokana na hilo, ameamua kufanya kazi ya ziada ya kugonga kokoto ili kuongeza kipato na kupata fedha za kujikimu, ikiwamo nauli ya kwenda shuleni kufundisha.

“Nikitoka shuleni sina pa kwenda, naendelea kugonga kokoto na kuuza debe moja, ikitokea Toyo na nimegonga kwa muda mrefu nauza kokoto hizo,” anasema.

Anasema kuna wakati kokoto zikiwa nyingi huuza ujazo wa lori, kisha hununua mawe kwa ajili ya kugonga nyingine.

Anasema hutumia Sh6,000 kwa siku kwenda shuleni na kuna wakati hushindwa kwenda kwa kukosa nauli hiyo ambayo hukodi bajaji ya kumpeleka na kumrudisha nyumbani.

Anaiomba Serikali kuwaangalia watumishi wenye ulemavu kwa kuwawezesha kupata mikopo isiyo na riba ikiwamo inayotokana na asilimia 10 za kwenye halmashauri.

Anasema anapoandika chaki hummwagikia usoni kwa kuwa anaandika eneo la ubao ambalo limemzidi.

“Kutokana na mazingara hayo, sasa najifunga kitambaa eneo karibu na pua, nikishafikia urefu ambao nipo basi natoa kitambaa na kuendelea kufundisha kama kawaida,” anasema mwalimu huyo wa Kiingereza kwa darasa la tano.

Anasema ana uwezo wa kufundisha masomo yote.

Christina Nyakunga, mke wa Lyuvale ambaye kwa pamoja wana watoto watano anasema hapendi kukumbuka ajali iliyompata mume wake.

Anasema alipotoka hospitali na kurudi nyumbani, mazingara yalikuwa magumu kwa sababu alitoka akiwa anatembea na kurudi kwenye kitimwendo.

“Namshukuru Mungu kwa kuwa amemweka hai hadi leo hii tunajadili ya kufanya, hivyo namuomba Mungu  aendele kumweka katika hali hii kwa sababu kuna wengine wamepata ajali na kufariki dunia lakini mume wangu yupo hai, hilo ndilo nashukuru,”  anasema.

(kushoto) Mwalimu Sliveter  Lyuvale na mke wake Christina  Nyakunga wakiwa na yuso za furaha nyumbani kwao .Picha na Mary Sanyiwa

Anasema maisha yamebadilika kwa sababu mume wake alikuwa anafanya kazi, ikiwamo kwenda shambani kufanya miradi mbalimbali lakini kwa sasa hawezi.

Anaeleza akitoka kazini anakuwa sehemu hiyo na kugonga kokoto pekee.

Christina anasema ameweza kumudu hali hiyo kwa sababu ya kumuomba Mungu, akisema amekuwa jasiri akiendelea kupambana ili maisha yaendelee.

Amewataka wanawake kuwa na hofu ya Mungu na uvumilivu pindi wenza wao wanapopata matatizo, badala ya kuwakimbia.

Mwakilishi wa Chama cha Watu wenye Ulemavu Wilaya ya Mufindi, Chrisantus Bakana amesema wilaya hiyo ina walimu takribani 20 wenye ulemavu wa aina mbalimbali.

Anasema wanaendelea kuwatambua walimu wenye mahitaji muhimu kwa kuwapatia mahitaji.

“Walimu wenye ulemavu tayari tumewatambua kwa sababu wapo wenye kuhitaji viatu na fimbo nyeupe, hivyo tunaendelea kuweka jitihada kutatua changamoto zao. Tunaomba Serikali iendelee kutuunga mkono kwa ajili ya kuwasaida walimu wenye ulemavu kutimiza majukumu yao,” anasema.

Katibu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wilayani humo, Patrick Mlowe anasema wamekuwa wakiwasaidia walimu wenye changamoto kama hizo kwa kuwapatia kitimwendo ili kutekeleza majukumu yao.

Anaiomba jamii inayowazunguka walimu wenye mahitaji maalumu iwasaidie.

Related Posts