Jeki ilivyomsababishia ulemavu utingo | Mwananchi

Musoma. Hujafa hujaumbika! Ni msemo unaoeleza maisha ya sasa ya Jackson Hamisi aliyepata ulemavu akiwa anatengeneza gari.

Hamisi (26), mkazi wa Kijiji cha Masurura wilayani Butiama, Mkoa wa Mara anasema Aprili 29, 2021 saa 12:00 jioni ni siku ambayo kamwe hataisahau maishani mwake. Ni siku iliyobadilisha maisha kutoka alivyokuwa mwenye viungo kamili hadi kuwa mwenye ulemavu, asiyeweza kutembea.

Katika mahojiano na Mwananchi, Hamis anasimulia kuwa, akiwa chini ya gari akiendelea na matengenezo, ghafla alipigwa na kitu kizito kwenye nyonga, hali iliyosababisha apoteze fahamu.

Anasimulia alipozinduka alijikuta katika kitanda cha Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando jijini Mwanza.

Hamisi anasema muda mfupi kabla ya kufika mwisho wa safari kwa siku hiyo, ghafla basi alilokuwa akifanya kazi akiwa utingo, lilipata hitilafu kwenye Kijiji cha Idindo, hivyo akashuka kuangalia tatizo lilikuwa ni nini.

“Kwa sababu nilikuwa utingo ikabidi nishuke kuangalia kuna shida gani, nikabaini propela ilikuwa imekatika. Nikaanza mchakato wa kufanya matengenezo ili tuendelee na safari,” amesema.

Anasimulia akiwa amepandisha basi juu kwa kutumia jeki na kuanza matengenezo, ghafla jeki ilifyatuka, gari likateremka likamuangukia eneo la nyonga.

“Nilijua tumemaliza safari kwa siku hiyo, kwani kilikuwa kimebaki kijiji kimoja tu tufike mwisho wa safari. Kumbe Mungu naye alikuwa amepanga ya kwake, safari yangu ya uzima ikaishia pale na kuwa mwanzo wa maisha haya yaliyojaa upweke, mateso na maumivu makubwa,” anasema.

Akizungumza nyumbani kwa mama yake mdogo Mtaa wa Nyabisare, nje kidogo ya mji wa Musoma, Hamisi anasema alikuwa akifanya kazi kwenye basi lililofanya safari kati ya Jiji la Mwanza na Kijiji cha Maligisu wilayani Kwimba, mkoani Mwanza.

Anasema kazi hiyo iliyokuwa na ujira kati ya Sh7, 000 na Sh10, 000 kwa siku na aliifanya kwa miezi minne tu. Aliipata baada ya kumaliza mafunzo ya ufundi kwenye gereji iliyopo jijini Mwanza.

Hamisi anasema malengo yake ilikuwa kuwa na maisha bora, ikiwa ni pamoja na kumjengea nyumba mama yake na kumpa mtaji wa kutosha kufanya biashara, hivyo kuboresha kipato.

Hamisi ambaye sasa analazimika ama kujivuta au kutambaa kutoka eneo moja kwenda lingine, anasema matibabu yalishindikana baada ya mama yake kukosa Sh2.5 milioni ili afanyiwe upasuaji.

Anasema alipofikishwa hospitalini alipewa huduma za awali, baada ya vipimo madaktari walimweleza ili apone na kurejea katika hali ya kawaida anahitaji kufanyiwa upasuaji.

Hamisi anasema aligundulika uti wa mgongo ulipata shida kutokana na ajali hiyo. Ukosefu wa fedha ulisababisha asifanyiwe upasuaji, akarudi nyumbani baada ya siku kadhaa za kukaa hospitalini.

Anasema waliporejea nyumbani, wana-ukoo walichanga fedha ili akapatiwe tiba lakini zilipatikana Sh500, 000 kiasi ambacho kisingetosha kugharimia upasuaji.

Anasema mmiliki wa gari alimpeleka hospitalini na tangu hapo hakuwasiliana naye tena wala kugharamia matibabu.

Anasema ajali imesababisha apooze kuanzia kwenye nyonga hadi miguuni, hivyo hawezi kusimama wala kutembea.

Hata hivyo, anasema hajakata tamaa ya kupona, anaamini akipata fedha na kufanyiwa upasuaji ataweza kuendelea na maisha yake kama kawaida.

Anasema hali aliyonayo ni ya mateso na majonzi, katika umri wake alitarajia makubwa kutokana na bidii aliyoiweka kwenye kazi, akiwa mtoto pekee kwa mama yake.

“Nilikuwa na ndoto nyingi, niliamini ipo siku ningebadilisha maisha yangu na ya mama yangu, kila siku nilifanya kazi kwa bidii na kwa kujituma kutokana na mazingira ya kwetu, kwani umaskini wetu ulisababisha nishindwe kumaliza shule, niliishia kidato cha pili baada ya mama kukosa fedha kwa ajili ya mahitaji ya shule,” anasema na kuongeza:

“Nimekuwa mpweke, kila nikiangalia vijana wa rika langu wanavyojituma kwenye utafutaji najikuta nalia, sina wa kuongea naye nimekuwa wa kukaa ndani tu nasubiri kuhudumiwa kwa kila kitu, hii inaniumiza.”

Anasema ajali imemwongezea umaskini kwenye familia baada ya mama yake kumaliza mtaji aliokuwa nao kwa ajili ya matibabu yake.

Kwa mujibu wa Hamisi, mama yake alikuwa akijishughulisha na biashara ya kukaanga samaki na kusafirisha kwenda Dar es Salaam.

Baada ya ajali, anasema fedha alizokuwa nazo pamoja na mtaji alizitumia kuhakikisha anapata tiba.

Anasema hakuwahi kumuona baba yake tangu azaliwe ingawa wamekuwa wakiwasiliana kwa njia ya simu, mawasiliano anayosema yalikoma baada ya kumweleza kuhusu ajali na hali aliyonayo.

Hamisi ameiomba Serikali na wadau wamsaidie apate matibabu arejee katika hali ya kawaida na kuendelea na shughuli zake.

Pili Chacha, mama mdogo wa Hamisi anasema amamchukua na kuishi naye kutokana na changamoto zilizomkabili kijijini.

“Alikuwa akiishi na mama yake ambaye ni dada yangu, hali ilikuwa mbaya zaidi maisha ni magumu inafika hatua wanakosa chakula kwa sababu dada yangu hana biashara yoyote, pesa yote iliishia kwenye matibabu,” anasema.

Pili ambaye ni msusi, anasema ameacha kazi hiyo ili aweze kumhudumia kijana huyo kutokana na hali yake.

“Imebidi niache kwenda saluni niweze kumhudumia, kwa hali yake si vizuri kumuacha peke yake kwa muda mrefu kwani anazidi kuwa mpweke,” anasema.

Anawaomba wadau wamsaidie aweze kufanyiwa upasuaji kama madaktari walivyoelekeza.

Related Posts