Mwanaidi Sarumbo: Simulizi ya miaka tisa ya huduma zahanati ya kijiji

Morogoro/Dar. Mwanaidi Sarumbo ni miongoni mwa watumishi wa afya wachache, waliojitolea kuishi maeneo yasiyofikika kirahisi wakitoa huduma kwa wananchi saa 24, siku saba za wiki.

Kwa zaidi ya miaka tisa sasa, Mwanaidi (29) ambaye ni daktari wa binadamu amekuwa akihudumia wananchi wa vijiji vinne vya Mhale, Chowelo, Mngoo na Chitengu katika zahanati ya Mhale iliyopo Kata ya Mgeta, wilayani Morogoro Vijijini.

Kijiji cha Mhale kinapatikana umbali wa kilomita 53 kutoka Morogoro mjini. Ili kukifikia usafiri pekee ni wa bodaboda ambayo pia itakulazimu kutembea kwa miguu umbali mrefu kutokana na changamoto ya miundombinu ya barabara isiyoruhusu dereva na abiria kupita pamoja.

Mhudumu wa afya ngazi ya jamii, Gairos James

Vijiji viko milimani ili kufikia kaya moja hadi nyingine utalazimika kuvuka mito na mabonde.

“Mara ya kwanza nilipofika kijiji hiki, niliwaza kuacha kazi. Nilihamia kutoka kituo cha Dakawa Wami. Nimeishi hapa miaka tisa, changamoto nyingi lakini nimekabiliana nazo kwa kuwa niliapa kuwasaidia wananchi, nina muda mrefu watumishi wengi wamekuja wameniacha,” ndivyo anavyoanza kusimulia Mwanaidi.


Mwanaidi Sarumbo Simulizi ya miaka tisa ya huduma zahanati ya kijiji

Anasema mazingira yalimshtua, hapakuwa na nyumba ya yeye kuishi, kwa siku kadhaa aliishi kwa mwenyeji wake, kabla ya kutafuta nyumba ya kupanga.

Mwanaidi anasema changamoto kubwa ni barabara na hakuna mawasiliano ya intaneti. “Sehemu kubwa huku hazishiki mtandao, ukija hapa mawasiliano ya kawaida utafanya, lakini kuingia online ni changamoto. Hata ninavyofanya kazi inabidi niandike kwenye karatasi kisha niende mjini ambako nitapata mtandao, ninafanya kazi mara mbili,” anasema.

Anasema inamlazimu kwenda kuingiza taarifa mtandaoni kila mwisho wa mwezi na hutumia siku nzima kwenda na kurudi kutokana na umbali.

Mwanaidi katika mahojiano na Mwananchi yaliyofanyika Oktoba 28, 2024 anasema watumishi wanaopelekwa katika zahanati hiyo hawakai, wengi hufika na kuondoka baada ya muda mfupi.

Anasema wapo wanaoomba kuondoka kwa kigezo cha kwenda masomoni.

“Tulikuwa wawili, mwenzangu kwa sasa amekwenda masomoni, sina msaidizi hapa zaidi ya watumishi wa afya ngazi ya jamii.

“Inaniwia vigumu, muda mwingine changamoto leba kuna mzazi, mgonjwa anakusubiri kwa hiyo unakuta muda mwingine unashindwa lakini unapambana kuokoa maisha,” anasema na kuongeza:

“Kazi yangu haina off (mapumziko) wala usingizi wa usiku. Sina mapumziko muda wote unakuwa ‘bize’ haina Jumamosi wala Jumapili kwa sababu unakuwa peke yako. Ikitokea dharura wewe ndiye unahusika. Wanakufuata nyumbani inabidi utoke, kwa hiyo muda wa kazi unaisha lakini ikitokea dharura inabidi uache kila kitu unachofanya unaondoka kwenda kusaidia mgonjwa zahanati.”

Hata hivyo, Machi 11, 2025 Mwanaidi akizungumza na Mwananchi amesema wamepelekwa watumishi wengine wawili.

“Nimeletewa watumishi wawili wiki iliyopita sasa nitakuwa na ahueni. Wamesaini na kuondoka kwenda wilayani kufuatilia uhamisho,” amesema.

Anasema kinachowakimbiza watumishi eneo hilo ni barabara mbovu na ukosefu wa mtandao.

Changamoto nyingine anasema ni wananchi kutoelewa au kuzingatia maelekezo wanayopewa, wakiwamo wajawazito ambao baadhi hujifungulia nyumbani na wanapopata shida hulazimika kumuita kwenda kuwasaidia.

“Kuna muda wanakijiji wanakuwa haelewi hata ukielekeza wengi wanachoka. Mazingira ya huku hata nikiondoka sitasahau kila siku nitakuwa nakumbuka, kwanza sikutarajia kama kuna watu wanaishi huku hata nilivyofika nilishangaa mno,” anasema.

Anasema ili huduma itolewe na muhudumu apate muda wa kupumzika, wanapaswa wawe watatu. Uwepo wa idadi hiyo ya watoa huduma anasema itaepusha zahanati kufungwa.

Anasema ili kupata huduma ya mtandao wa kasi hulazimika kwenda eneo la Mzumbei, hivyo kunakosekana mtu wa kutoa huduma.

“Kama mpo wawili au watatu hata akitoka  mmoja kwenda kufanya mambo mengine mmoja anabaki kituoni, mgonjwa wa dharura akifika anapewa huduma, bila hivyo muhudumu unateseka, wagonjwa nao wanateseka kwa kukosa huduma ukiondoka kituoni. Hali hii hunilazimu nitoke mara moja pekee kituoni kwa mwezi,” anasema.

Mwanaidi anasema vijiji vyote vinne vinatumia shule moja pekee ya msingi iliyopo ya Chowelo. Anasema hutumia huduma Mkoba kwenda kutoa chanjo kwa watoto na wajawazito kwa tarehe inayopangwa kila mwezi.

Anasema amekuwa akitoa ushauri kwa kina mama kujiunga na uzazi wa mpango, huduma za lishe kwa watoto na masuala ya afya kwa ujumla.

Anasema kwa kushirikiana na mtoa huduma ngazi ya jamii, Gairos James kabla ya kwenda kwa wananchi huwasiliana na mwenyekiti wa kijiji ambaye naye huwataarifu mwenzake wa karibu kwamba tarehe fulani kuna chanjo za watoto, hivyo huweka kambi eneo moja.

Mwanaidi anasema kunapokuwa na mgonjwa mwenye rufaa, hushirikiana na wanakijiji kumsafirisha kutokana na miundombinu isiyo rafiki.

Anasema iwapo atatokea mjamzito mwenye uzazi pingamizi anayehitaji upasuaji, humsafirisha kwa machela mpaka Kituo cha Afya Mgeta wakitembea kwa miguu kwa takribani saa 2.30 ili kuifikia barabara ambako atachukua usafiri mwingine.

“Usafiri unapatikana mbali, ni lazima utoke hapa Mhale ufike barabarani eneo la Nyandira, ni mbali ni takribani saa 2:30 kwa mwendo wa miguu. Pale ndipo unapata gari, bajaji au bodaboda kukifikia Kituo cha Afya Mgeta,” anasema.

Anasema: “Unaweza ukamwambia mjamzito kwamba wewe hutakiwi kujifungulia hapa, unatakiwa kwenda kituo cha afya lakini anafika zahanati tayari ana uchungu, hawezi kusukuma mtoto hapo ni lazima apelekwe kituo cha afya kwa machela,” anasema.

Hata hivyo, anasema hakuna mjamzito aliyewahi kupoteza maisha katika zahanati, hufanikiwa kuwafikisha kituo cha afya isipokuwa mmoja aliyefariki dunia jirani na kituo cha afya.

“Tangu nimeanza kazi ni mara moja pekee, nilipambana lakini alifia karibu na kituo cha afya, huyu alipata changamoto baada ya kuzalia nyumbani. Kwa hiyo mpaka wanamfikisha hapa kufanya huduma ya kwanza, tukatoka hapa kwa machela alishapoteza damu nyingi,” anasema.

Mwanaidi anasema mara nyingi huwashauri wajawazito kujifungulia zahanati na wenye changamoto kwenye kituo cha afya Mgeta.

Daktari Mwanaidi Sarumbo akizungumza na Mwananchi katika zahanati ya Mhale, iliyopo iliyopo katika Kata ya Mgeta Wilaya ya Morogoro Vijijini

“Changamoto wanaume si waelewa. Unamwagiza mama aje na kanga, vitenge na hela ya akiba akienda kumwambia baba anasema kila kitu ni bure, hawajui kwamba vitu vingine inabidi mama awe navyo binafsi,” anasema.

Changamoto ufikishaji dawa, vifaatiba

Anasema licha ya uwepo wa changamoto katika utoaji huduma, kukusanya na kuweka kumbukumbu za nyaraka, ufikishwaji wa dawa na vifaatiba katika zahanati ya Mhale ni jambo lingine.

Kwa mujibu wa Mwanaidi, Bohari ya Dawa (MSD) hushusha dawa katika zahanati ya Luwale ambako hupokewa na watoa huduma.

Baada ya hapo, anasema hupelekwa zahanati ya Mhale kwa mtu kubeba kichwani au kwa pikipiki.

“Kama bodaboda anakuja huku wanalipia MSD wenyewe, kwa mfano wanaweza kumpa Sh10,000 au Sh15,000 kulingana na maboksi yaliyoshushwa kwa mfano kama ni boksi moja wanaweza kumwambia Sh10,000, jinsi yanavyoongezeka inakuwa vivyo hivyo,” anasema.

Anasema hufanya maoteo ya kiasi cha dawa zinazohitajika kwa mwaka na mara nyingi hajawahi kukosea.

“Mara nyingi maoteo ninayoyafanya kila mwaka huwa naotea vizuri, haijawahi kutokea zikaisha,” anasema.

Anasema anapofanya maoteo hayo, huangalia magonjwa yanayowasumbua watu wengi ambayo ni homa, vifua na nimonia kutokana na hali ya baridi iliyopo eneo hilo, hivyo amekua akiagiza zaidi antibiotiki.

Mwanaidi anasema anapofanya hivyo huangalia ni nini kimepungua na kipi kinahitajika kupitia mfumo.

“Huko nyuma tulikuwa tunahangaika kutoa chanjo, lakini tangu tumepata friji kwa sasa wanapata muda unaotakiwa hakuna changamoto hiyo,” anasema.

Kuhusu magonjwa yasiyoambukiza, anasema ni nadra, na akitokea huwaelekeza kwenda kituo cha afya.

Muhudumu wa afya ngazi ya jamii, Gairos James anasema amekuwa akimsaidia Mwanaidi kutekeleza majukumu yake katika vijiji vya Mhale na Chowelo.

Katika vijiji hivyo kuna vitongoji vya Kisulu, Kipondwa, Kizagila, Chowelo, Kiyala, Vumi na Bondeni.

“Changamoto hapa ni mtumishi mmoja, ukifika mwisho wa mwezi anaondoka kwenda mjini kuingiza takwimu mtandaoni, inabidi nibaki kuhudumia wagonjwa wa dharura hasa watoto.

“Kutokana na wagonjwa wengi namsaidia na kama kuna dawa ya kufuata chumba cha dawa na kama zimeisha naenda zahanati zingine za Nyandila, Lushungi nafuata huko,” anasema Gairos aliyeanza kazi katika zahanati hiyo mwaka 2017.

Habari hii imeandikwa kwa msaada wa Taasisi ya Gates Foundation

Related Posts