Dar es Salaam. Makamu Mwenyekiti Chadema-Bara, Tundu Lissu amekabidhiwa gari lake aina ya Toyota Land Cruiser V8, VXR na Jeshi la Polisi, jijini Dodoma, ikiwa ni takriban miaka saba tangu aliposhambuliwa.
Gari hilo alilokabidhiwa leo, Mei 17, 2024 lilikuwa limehifadhiwa katika yadi ya Kituo Kikuu cha Polisi Dodoma tangu Septemba 7, 2017 aliposhambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana nyumbani kwake Area D, jijini humo.
Lissu alishambuliwa muda mfupi baada ya kuwasili akitoka kushiriki mkutano wa Bunge uliokuwa unaendelea.
Tangu siku hiyo, gari hilo lilitolewa Area D na kupelekwa kituoni hapo.
Baada ya kukabidhiwa gari hilo, Lissu amesema atalitengeneza ili alitumie kwa shughuli zake za kisiasa mpaka pale litakaposhindwa kutembea.
Amesema anakwenda kuweka milango mingine na iliyopo yenye matundu ya risasi ataihifadhi.
Kwa mujibu wa Lissu, baada ya gari hilo kufikia tamati kutumika, atairejesha milango hiyo na kufanya utaratibu wa kulipeleka makumbusho.
Mwanasiasa huyo amewashukuru Polisi kwa kulihifadhi gari hilo kwa kipindi chote, akimwomba mtu anayetumia namba zake za gari hilo kuzirejesha, akisema amefuatilia na kubaini zinatumika.
Hii ni mara ya pili kwa Lissu kwenda Polisi Dodoma kulifuatilia baada ya Mei 9, 2023 alipoonyeshwa gari hilo kwa mara ya kwanza tangu aliposhambuliwa.
Akizungumza baada ya kuliona siku hiyo, Lissu alisema: “Hili gari limekuwa chini ya Polisi kwa muda wote huu na mimi binafsi nilikuwa sijawahi kuliona kabisa, nilikuwa nasikia tu kwamba nilipigwa risasi nyingi, leo wameniwezesha nimeona lina matundu 30 ya risasi na imenipa shida sana, nashukuru kwa kulilinda gari hii,” alisema.
Alieleza kushangaa kuona risasi zote kuelekezwa kwenye mwili wa mtu mmoja na kwamba baada ya kuliona gari hilo angefanya mawasiliano na Jeshi hilo ili aende kulichukua.
“Wanikabidhi (gari) na maisha mengine yaendelee, nafikiri kwa sababu kumekuwa na maneno maneno mengi, kwamba Polisi gari wanaikatalia, naomba niseme hapa wazi polisi hawajawahi kuwa na wazo la kunikatalia kuchukua gari langu,” alisema.
Alisema kilichokuwa kinatokea alipokuwa akienda kulitazama gari hilo, watendaji wa jeshi hilo walikuwa na shughuli nyingi.
“Ni Jamhuri na vyombo vyake vya ulinzi na usalama, ikiwemo Jeshi la Polisi wana maamuzi. Kielelezo (gari) wamekaa nacho zaidi ya miaka sita, kama ni picha wamepiga na kuangalia risasi ilipita wapi watakuwa wamefanya,” alisema.
Hata hivyo, Lissu wakati huo, alilitaka Jeshi la Polisi kuwatafuta waliofanya tukio hilo washughulikiwe kwa mujibu wa sheria.
“Mimi ningependa huyo aliyepiga hizo risasi zote hizo, atafutwe na ashughulikiwe kwa mujibu wa sheria,” alisema.
Lissu alishambuliwa kwa risasi akiwa kwenye maegesho ya magari nje ya nyumba yake Area D, jijini Dodoma.
Baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana, alipelekwa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Dodoma, kisha usiku wa siku hiyohiyo alihamishiwa Hospitali ya Nairobi nchini Kenya hadi Januari 6, 2018 alipopelekwa nchini Ubelgiji kwa matibabu zaidi.
Kwa mujibu wa Lissu, watu wawili wenye bunduki za kivita waliruka ghafla kutoka kwenye gari lililokuwa likimfuata kwa nyuma na kuanza kumshambulia.
Alieleza kati ya risasi zaidi ya 30 zilizoipiga gari, 16 zilimpiga katika sehemu mbalimbali za mwili wake. Wakati wa tukio hilo, Lissu alikuwa na dereva wake, Adam Bakari.