Presha, sukari, moyo vilivyoondoa uhai wa mbunge wa kwanza Moshi

Moshi. Wakati mamia ya waombolezaji wakifurika kwenye maziko ya aliyekuwa mbunge wa kwanza wa CCM  Moshi mjini, Mkoa wa Kilimanjaro, John Mwanga (78), familia imeeleza kuwa baba  yao alikuwa akisumbuliwa na shinikizo la damu na kisukari.

Mwanga ambaye alikuwa mbunge wa kwanza wa Moshi mjini mwaka 1990-1995 kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), alifariki dunia Machi 4, 2025 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Misheni ya Selian iliyopo mkoani Arusha. Mwanga, ambaye ameacha wajukuu 30, watoto tisa na vitukuu watano, amezikwa leo Machi 12, 2025 katika makaburi ya familia yaliyopo Kijiji cha Sisamaro, kata ya Okaoni, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Akisoma historia ya marehemu,  Imani Mwanga amesema baba yao alikuwa akisumbuliwa na shinikizo la damu na kisukari, ambapo mwaka 2023 na baadaye mwaka 2024 alipata changamoto ya moyo na kufanyiwa upasuaji katika Taasisi ya Magonjwa ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), jijini Dar es salaam.

Watoto wa marehemu John Mwanga, wakiwa mbele ya jeneza lenye mwili wa baba yao nyumbani kwao katika Kijiji cha Sisamaro, Kibosho, Wilaya ya Moshi Mkoani Kilimanjaro. Picha na Omben Daniel

“Baba yetu alikuwa akisumbuliwa na shinikizo la damu, sukari na ugonjwa wa moyo kiasi cha  kufanyiwa upasuaji mkubwa JKCI, upasuaji ulifanyika vizuri na akaendelea na matibabu  na baadaye alifanyiwa upasuaji mkubwa wa mguu,  na  aliendelea na matibabu hospitali mbalimbali,” amesema Imani ambaye ni mtoto wa marehemu.

Amesema ilipofika Februari 27, 2025 hali ya baba yao ilibadilika ghafla na kupelekwa Hospitali ya Selian, ambako aliendelea na matibabu mpaka alipofariki Machi 4, mwaka huu.

Aidha, amesema familia imepoteza mtu muhimu, aliyekuwa kiongozi dhabiti, kiunganishi wa familia.

“Tunamshukuru Mungu kwa kutujalia baba wa kipekee mno, sio rahisi kutaja sifa zake tukamaliza, Mungu alitupa baba na kiongozi dhabiti, tutajitahidi kuyaenzi yale mema aliyotuachia,” amesema mtoto huyo wa marehemu.

Akihubiri katika ibada ya maziko, Paroko wa Parokia ya Mtakatifu Fransisco Xavery Mkombole, Paroko Padri Evarist Kawau, ametoa pole kwa familia na kuwataka waumini kutumia kipindi hiki cha Kwaresma kusimama imara katika maombi.

“Tuendelee kumuombea baba yetu pumziko jema tukiamini ipo siku tutakutana naye huko mbinguni, lakini niwaombe waumini wenzangu mtumie kipindi hiki cha Kwaresma kusimama imara kwenye maombi,” amesema Padre Kawau

Mke wa marehemu John Mwanga, akiwa na watoto wake mbele ya jeneza lenye mwili wa mume wake. Picha na Omben Daniel

Akitoa salamu za pole kwa niaba ya Mbunge wa Moshi mjini, Priscus Tarimo, Katibu wa Mbunge, Said Mndeme amesema wataendelea kumuenzi kama mwana mageuzi wakati Bunge lililopitisha mabadiliko ya Katiba yaliyosababisha kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi.

“Mzee wetu alikuwa mbunge 1990 -1995 kwa hiyo alishiriki kwenye mchakato wa kidemokrasia kwenye masuala ya Katiba, hivyo ni lazima tumuenzi kama mwana mageuzi kwa sababu Bunge lao ndio lililopitisha mabadiliko ya Katiba na nchi kuingia kwenye mfumo wa vyama vingi, hivyo tunamkumbuka nalo,” amesema Mndeme .

Related Posts