Kaya maskini Dar zapewa kodi, Chalamila atia neno

Dar es Salaam. “Umaskini sio ugonjwa wa kudumu’. Haya ni maneno aliyoyarudia mara kadhaa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila wakati akizindua mpango wa ruzuku ya kodi kwa kaya maskini zinazoishi kando kando ya barabara za mwendo wa haraka.

Mkuu huyo wa mkoa ameeleza kushangazwa na watu wanaokumbatia umaskini kama kitu cha kujivunia badala ya kutafuta namna ya kujikwamua kutoka kwenye hali hiyo.

Akizungumza leo Machi 12, 2025 wakati akizindua mpango wa ruzuku ya kodi kwa kaya maskini amesema Serikali inafanya jitihada mbalimbali kuwakwamua wananchi wake, lakini hiyo haipaswi kuwa sababu ya wao kuendelea kuwa wanyonge.

“Unaposaidiwa onesha jitihada za kutoka hatua moja kwenda nyingine, sio kila siku kilio chako ni umaskini. Umaskini sio ugonjwa wa kudumu unapaswa kupambana kutoka hapo ulipo, kukaa barabara sio kuangalia magari yanayopita na kuyahesabu.

“Tumia fursa zilizopo kwenye mazingira yako kujitafutia kipato halali, kuishi Dar es Salaam kama huna kipato ni kasheshe, jiji hili kila kitu unanunua hivyo ni lazima kupambana usione sifa kukaa kinyonge na kujizungumzia kwamba wewe ni maskini kila siku,” amesema na kuongeza.

“Tatizo letu Watanzania hatutaki kuambiwa ukweli na tunataka kuvisikia vile vinavyotufurahisha ila uhalisia ni kwamba wengi tunaukumbatia umaskini kwa sababu ya uvivu. Hapa Dar wanakuja watu wa mikoa mingine wanazitumia fursa zilizopo na wanafanikiwa wewe unabaki na umaskini,”.

Katika mpango huo Serikali imetenga Sh479.5 milioni katika utekelezaji wa mpango wa ruzuku ya kodi za nyumba kwa kaya maskini 999 zinazoishi kwenye nyumba za kupanga kando ya barabara za mwendo kasi.

Fedha hizo zimetolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) ikiwa ni awamu ya kwanza ya utekelezaji wa mpango wa majaribio wa kunusuru kaya maskini zilizo hatarini kushindwa kumudu kuishi karibu na njia ya BRT kutokana na kupanda kwa gharama za maisha, ikiwemo kodi ya nyumba.

Katika awamu hiyo ya kwanza kila kaya imepata Sh480, 000 kama kodi ya miezi sita ambayo ni sawa na Sh80, 000 kwa mwezi.

Meneja wa miradi ya ajira za muda na uendelezaji miundombinu wa Tasaf, Paul Kijazi amesema mpango huo, unaofadhiliwa na Benki ya Dunia kupitia Dar es Salaam Urban Transport Improvement Program (DUTP), unalenga kusaidia kaya hizi kumudu gharama za maisha na kunufaika na fursa za kiuchumi na kijamii.

Amesema licha ya mpango huo kuzisaidia kaya hizo kuendelea kuishi kwenye maeneo hayo, pia unalenga kuwawezesha wakazi wa mijini wenye kipato cha chini kunufaika na fursa za kiuchumi zinazotokana na mfumo wa BRT.

“Ili kufanikisha hili, wanufaika hupokea ruzuku ya kodi ya nyumba, mafunzo ya ujasiriamali, ushauri wa kibiashara na mwongozo wa mabadiliko ya kitabia. Hatua hizi zinawawezesha kuendelea kuishi katika makazi yao licha ya kupanda kwa gharama za maisha na kunufaika na fursa za BRT.

Jumla ya kaya 1,535 zinatarajiwa kunufaika katika mpango huo katika Halmashauri tatu za jiji la Dar 437 za Ubungo , 504  Kinondoni na  594 za halmashauri ya Ilala.

Akizungumza baada ya kupokea ruzuku hiyo,  Amina Ally amesema atazitumia fedha hizo kuboresha biashara yake ili kujiondoa kwenye orodha ya kaya maskini.

“Hizi fedha naenda kuziweka kwenye biashara nina uhakika miezi sita ijayo nitakuwa nimepiga hatua, sitakuwa tena kaya maskini,” amesema Amina.

Kwa upande wake Fatuma Mfaume amesema ni fursa kubwa kwao kukumbukwa na Serikali kwa kuwa ni ukweli kuwa hali ya uchumi imebadilika kwenye maeneo yao.

“Ni kweli maisha kwenye maeneo yetu yamebadilika, kodi zimepanga bei hata maeneo ya biashara gharama zake ziko juu, kwa hiki kilichofanyika itakuwa imetusogeza katika hatua nyingine,” amesema Fatuma.

Related Posts