Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amefanya uteuzi wa viongozi mbalimbali wa wenyeviti wa bodi na kumuongezea muda Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (Tafiri).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Moses Kusiluka, Dk Ismael Aaron Kimirei ameteuliwa kushika wadhifa katika kipindi cha pili.
Naye Balozi Ernest Mangu ambaye ni Mkuu wa Jeshi la Polisi mstaafu ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kwa kipindi cha pili.
Kwa upande wake Mkurugenzi mstaafu wa Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Marina Njelekela ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOI), akichukua nafasi ya Profesa Charles Mkony ambaye amemaliza muda wake.
Uteuzi mwingine ni wa Juma Fimbo ambaye ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA).
Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Profesa James Mdoe ameteuliwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) akichukua nafasi ya Dk Andrew Kitua ambaye amemaliza muda wake.