Wanamitandao wavamia hospitalini wakisaka ukweli kuhusu alipo Papa Francis

Rome. Wakati Papa Francis alipokuwa akipokea matibabu ya nimonia kali katika mapafu yote mawili, mwanamitandao (TikToker) wa Italia anayeitwa, Ottavo aliingia katika wodi moja ya Hospitali ya Gemelli jijini Roma akiwa na kamera nyuma kwenye mwili wake.

Gazeti la The Guardian limeripoti leo Jumatano Machi 12, 2025, kuwa lengo la TikToker huyo ilikuwa ni kuthibitisha nadharia iliyokuwa ikisambaa mitandaoni kuwa Papa Francis (88) alikuwa amefariki.

“Hakuna ulinzi kabisa hakuna chochote,” amesikika Ottavo akiwaambia wafuasi wake takriban 10,000 katika video hiyo.

“Nisingeweza kufika hapa ikiwa angekuwepo. Kwa maoni yangu, Papa Francis amefariki,” amenukuliwa mwanamitandao huyo.

Hata hivyo, kwa kutambua changamoto ya usambaaji taarifa za uongo na upotoshaji kuhusiana mwenendo wa afya ya kiongozi huyo wa kiroho hususan kwenye mitandao ya kijamii, Vatican ilianzisha utaratibu wa kutoa taarifa ya mwenendo wa afya yake mara mbili kwa siku.

Kwa mujibu wa Vatican, Ottavo hakubaini wodi aliyovamia haikuwa aliyolazwa Papa Francis akitibiwa maradhi yanayomsumbua kwenye mfumo wake wa upumuaji.

Tangu Papa alazwe Hospitali ya Gemelli mjini Roma Februari 14, 2025, Vatican imekuwa ikipambana kimyakimya kukabiliana na habari za uongo, wanaopanga njama na picha za bandia zilizotengenezwa kwa teknolojia ya akili mnemba (AI).

CNN pia imeripoti leo Jumatano Machi 12, 2025, kabla ya Ottavo, TikToker mwingine aliyejiita, Er Bombolino alijaribu kuingia hospitalini siku chache kabla ili kuthibitisha kuwa Papa alikuwa hai ama amekufa. Naye pia aliishia katika wodi isiyo sahihi.

Februari 22, 2025, Papa Francis alipata changamoto ya upumuaji kwa muda mrefu iliyoambatana na makohozi yaliyokuwa yametuama kwenye mfumo wa hewa hata hivyo, hali hiyo ilidhibitiwa na madaktari wanaomtibu kuthibitisha kuwa afya yake imeimarika.

Jana Jumanne, Vatican iliripoti Papa Francis hakuwa tena katika hatari ya kifo na alikuwa akionyesha matumaini ya kurejea kiafya katika matibabu hayo hospitalini, lakini habari za uongo kuhusu hali yake ya afya zinaendelea kuenea mtandaoni.

Akaunti kadhaa za mitandao ya kijamii zimetangaza kwa uongo kifo chake mara nne tangu alazwe hospitalini na maelfu ya picha bandia zimeanza kusambaa mitandaoni, zikimuonyesha Papa akiwa katika hali mbaya, amevaa mavazi yake meupe ya kidini huku akiwa amelala kitandani hospitalini, akipumua kwa msaada wa barakoa ya oksijeni.

Alhamisi iliyopita, kwa mara ya kwanza tangu alipoingia hospitalini, Papa Francis alirekodi na kutoa ujumbe wa sauti kuwashukuru waliokuwa wakimwombea apone, sauti yake ikiwa nzito na dhaifu baada ya kukaa hospitalini kwa karibu wiki tatu akipambana na nimonia.

Akizungumza kwa Kihispania ambacho ni lugha yake mama, Papa Francis alisema katika ujumbe huo uliorushwa kwenye Uwanja wa Mtakatifu Petro: “Nawashukuru kwa moyo wangu wote kwa sala zenu kwa ajili ya afya yangu kutoka uwanjani, nami ninawaombea kutoka hapa (hospitalini).”

Ripoti za vyombo vya habari nchini Italia zimependekeza kuwa moja ya malengo ya ujumbe huo wa sauti lilikuwa ni kujibu habari za uongo kuhusu kifo cha Papa.

Avvenire ambalo ni gazeti la kitaifa linalohusiana na Kanisa Katoliki, liliandika: “Ujumbe wa sauti wa Papa uliopeperushwa usiku wa jana (Machi 6) ni ushahidi wa kwanza wa kupinga uvumi huo.

Hata hivyo, kutokana na kulazwa kwake hospitalini kwa muda mrefu kuna hatari kwamba habari za uongo zitaendelea kuenea.”

Mkurugenzi wa Ofisi ya Habari ya Vatican aliliambia Gazeti la The Guardian Jumanne: “Habari za uongo hujieleza zenyewe. Sisi tunatoa taarifa zetu kwa uwazi na mara kwa mara.

“Tulisema kuwa kwa ujumbe huo wa sauti, Papa Francis alitaka kuwashukuru waumini kwa sala zao katika wiki hizi. Ikiwa mojawapo ya malengo ya ujumbe huo lilikuwa pia ni kupinga habari za uongo kuhusu afya yake, basi kila mtu ana uhuru wa kufikia hitimisho lake.”

Polisi pia wanakusanya taarifa kuhusu upotoshaji huu na wanatafakari hatua za kisheria, ingawa Wizara ya mambo ya Ndani ililieleza The Guardian kuwa, “hakuna uchunguzi rasmi unaoendelea kwa sasa.”

TikTokers Ottavo na Er Bombolino, katika video ya pamoja ya Instagram, walijitetea dhidi ya tuhuma hizo, wakisema: “Sisi si watu wa kupenda njama. Tumejitoa kwa Papa Francis. Tunatafuta ukweli tu. Yuko wapi Papa Francis?”

Awali, Vatican ilibainisha kuwa uamuzi wa kutoonekana kwenye video ulifanywa na Papa Francis mwenyewe.

 “Kila mtu ana uhuru wa kuchagua lini na jinsi gani aonekane,” Ofisi ya Habari ya Vatican ilieleza.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.

Related Posts