MECHI ya watani wa jadi, Yanga na Simba maarufu kama Dabi ya Kariakoo, imeota mbawa baada ya kuahirishwa na Bodi ya Ligi kwa sababu ya malalamiko ya Simba kuhusiana na sakata la kuzuiwa kufanya mazoezi ya mwisho kabla ya mchezo.
Mchezo huo ulipangwa kufanyika Machi 8 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ikiwa ni marudio katika duru la pili msimu huu baada ya awali timu hizo kukutana Oktoba 19 mwaka jana na Simba kulala 1-0 kwa bao la kujifunga la beki Kelvin Kijili katika dakika za lala salama.
Bodi ya Ligi imetangaza kuupangia tarehe nyingine mpya mchezo huo, huku Yanga wakitoa tamko la kukataa kucheza mechi hiyo.
Tukio kama hili lilitokea kwenye mechi baina ya mapacha hawa, mwaka 1965 katika msimu wa kwanza kabisa wa Ligi ya Taifa.
Naam, ni msimu wa kwanza kwa sababu kabla ya hapo hakukuwa na ligi moja ya kitaifa. Wakati wa ukoloni, ligi ilichezwa kwa ngazi ya wilaya tu, yaani kila wilaya ilikuwa na ligi yake, isipokuwa kwa wilaya chache zilizoshindwa kuandaa ligi zao basi zilishiriki ligi za wilaya za majirani zao.
Ligi ya kwanza ilikuwa ya wilaya ya Dar ya Dar es Salaam, iliyoanza mwaka 1929. Wakati huo Dar es Salaam ilikuwa wilaya ndani ya jimbo (mkoa) la Mashariki lililojumuisha wilaya za Morogoro pamoja na Bagamoyo.

Ligi iliyofuata ikawa ya Wilaya ya Iringa, mwaka 1931. Kwa hiyo hadi nchi inapata uhuru 1961, hakukuwa na ligi moja ya kitaifa.
Mwaka 1964 serikali ya awamu ya kwanza chini ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, ilileta kocha kutoka Yugoslavia, kwa ajili ya timu ya taifa.
Kocha huyu aliitwa Milan Celebic, alipokuja akagundua kuna wigo mdogo wa kuwaona wachezaji kutoka nchi nzima kwa sababu hakuna mashindano marefu ya kitaifa. Mashindano pekee ya kitaifa yaliyokuwapo ni Taifa Cup, ambalo lilishirikisha timu za mikoa.
Lakini tatizo lake ni kwamba mashindano haya yalikuwa ya mtoano, ukishatolewa ndiyo hadi mwakani…kwa hiyo kocha hapati nafasi ya kuona wachezaji wengi, mara nyingi.
Akashauri ianzishwe Ligi ya Kitaifa, ndipo mwaka 1965, Rais wa FAT wa wakati huo, Balozi J. Maggid, alipolipokea wazo hilo na kulifanyia kazi…ligi ikaanza ikiitwa mashindano ya kutafuta Klabu Bingwa ya Taifa. Ligi hiyo ilianza na timu sita za TPC-Moshi, Sunderland, Yanga na Tumbaku (Dar es Salaam), Coastal Union na Manchester United (za mkoa wa Tanga) na Ligi ilichezwa kwenye viwanja vya Ilala (sasa Karume) na Manispaa ya Tanga (sasa Mkwakwani). Hata hivyo, tatizo kubwa lililoikumba ligi hiyo na viongozi wa klabu, wachezaji na hata viongozi wa FAT (sasa TFF) ilikuwa ni kutozielewa vizuri kanuni na sheria za soka zilizosababisha Yanga kuigomea Simba na mwishowe kujitoa katika ligi.

Watani wa Jadi, Yanga na Simba (wakati ule ikiitwa Sunderland) walipangwa kukutana Juni 7, 1965 kwenye Uwanja wa Ilala (sasa Karume). Timu zikafika uwanjani, lakini Yanga wakamkataa mwamuzi aliyepangwa, pamoja na wachezaji fulani wa Simba.
Ikabidi vikao vifanyike kuokoa jahazi…mashabiki wameshaingia uwanjani wanasubiri mechi, lakini timu moja imekataa mwamuzi.
Baada ya vikao virefu na vizito, Rais wa FAT, Balozi J. Maggid akamteua kocha wa timu ya taifa, Milan Celebic, kuchezesha mechi hiyo.
Hapo Yanga wakakubali na kuingia uwanjani, lakini Simba nao wakagoma kisa kuna wachezaji wa Yanga walikuwa wamesimamishwa ila wakawemo kikosini. Wakati ule kulikuwa na chombo kama Bodi ya Ligi cha kusimamia ligi.
Mwenyekiti wake alikuwa, Abdu Hussein, yeye ndiye aliyeokoa jahazi baada ya kusema chombo chake hakikuwa na maandishi yoyote ya kusimamishwa kwao, hivyo hakitambui kama wamesimamishwa. Simba nao wakakubali, wakaingia uwanjani. Hata hivyo, muda mwingi ulipotea katika yale malumbano na kusababisha mechi kuchelewa kuanza.
Dakika ya 15, Yanga wakapata bao kupitia Mawazo Shomvi, hata hivyo mwamuzi Milan Celebic akamaliza mchezo katika dakika ya 80 kutokana na giza uwanjani. Na hii ni kwa sababu mchezo ulichelewa sana kuanza. Simba wakakata rufaa wakitaka mchezo urudiwe na FAT ikakubali. Yanga wakakataa kurudia wakisema Simba ndio walisababisha uchelewe kwa kuja na madai ya baadaye ya wachezaji kusimamishwa. Bila malalamiko yao mechi ingewahi kuanza kwa sababu malalamiko ya Yanga yalishamalizika mapema.
FAT ikasema kimsingi timu zote zilisababisha mechi kuchelewa kuanza hivyo zinawajibika kurudia. Yanga wakagoma kurudia na Simba wakapewa ushindi wa mezani. Hilo likawakera Yanga na kuamua kujitoa kwenye ligi. Hapo ndipo kaulimbiu yao ya DAIMA MBELE NYUMA MWIKO ilipoanza.

Kwa hiyo msimu wa kwanza wa ligi, 1965, Yanga hawakumaliza ligi kwa sababu walijitoa kugomea kurudia mechi yao dhidi ya Simba.
Miaka 60 baadaye, yaani 2025…mechi ya Yanga na Simba imeamuliwa kurudiwa, na Yanga tayari imeshatangaza mapema kwamba hawataicheza mechi hiyo. Je, Simba itapewa ushindi wa chee na Yanga itaamua kujitoa katika Ligi kwa mara nyingine? Je tutashuhudia tena DAIMA MBELE NYUMA MWIKO, au safari hii watalegea? Ni jambo la kusubiri kuona mara Bodi itakapotangaza tarehe mpya ya kupigwa dabi hiyo ya Kariakoo.