NHC yanunua eneo la Urafiki

Dar es Salaam. Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) limenunua eneo la Urafiki, zikiwamo mali zilizokuwa chini ya Kampuni ya Urafiki wa Tanzania na China.

Meneja wa Mawasiliano kwa Umma wa NHC, Muungano Saguya amesema hayo leo Mei 17, 2024 wakati wa ziara ya Mkurugenzi Mkuu wa NHC, Hamad Abdallah kutembelea miradi inayotekelezwa na shirika hilo jijini Dar es Salaam.

Hamad ametembelea miradi ya Samia Housing, Morocco Square, Shule ya Uchumi ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na eneo la Urafiki.

Saguya amesema eneo hilo linajumuisha nyumba, maghala, viwanja vya wazi, viwanda na mali nyinginezo.

Amesema eneo hilo lenye ukubwa wa zaidi ya ekari 50 limenunuliwa kwa mnada wa wazi kwa thamani ya zaidi ya Sh3 bilioni.

“Kupitia umiliki huu mpya, NHC limejipanga kuboresha maeneo haya ili kuendana na malengo yetu ya kutoa makazi bora na ya kisasa kwa wananchi. Tumeanza kwa kulipima na kutambua mipaka yote,” amesema.

Eneo la Urafiki lina historia ndefu ya kuwa kituo muhimu cha viwanda na makazi, kikitoa mchango mkubwa katika uchumi wa Tanzania.

Wabia wakuu wa kiwanda hicho ni Msajili wa Hazina na Kampuni ya Urafiki wa Tanzania na China.

Awali kulikuwa na mvutano kati ya kampuni iliyokuwa inamiliki kiwanda hicho na wafanyakazi hatua iliyofikia kupigwa mnada.

Related Posts