KIPA Abuutwalib Mshery ameshindwa kuendeleza rekodi aliyokuwa nayo dhidi ya Coastal Union akikaa langoni dakika 270 bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa baada ya Miraji Abdallah kuvunja mwiko huo leo katika pambano la Kombe la Shirikisho (FA).
Yanga ikiwa nyumbani kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam kuvaana na Coastal Union katika mchezo wa hatua ya 32 Bora, ilipata ushindi wa mabao 3-1, huku la Wagosi likimtibulia Mshery ikiwa ni mara ya kwanza kwake kutungulia na timu hiyo tangu aanze kukutana nao.
Mechi ya leo ilikuwa inatimiza dakika 360 kwa Mshery akiwa langoni dhidi ya Coastal tangu ilipomsajili kutoka Mtibwa Sugar, huku akiwa na rekodi ya kuibania pia akiwa na timu hiyo ya Manungu inayoshiriki Ligi ya Championship kwa sasa.

Mshery aliyetua Yanga dirisha dogo la msimu wa 2021-2022 akitoka kuibania Coastal Mkwakwani kwa kuiwezesha Mtibwa kushinda bao 1-0 na kusajiliwa Yanga Desemba 29 ambapo alianza kukaa langoni dhidi ya Coastal ugenini wakati Yanga ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0 mchezo uliopigwa Mkwakwani Jan 16, 2022 yaliyowekwa kimiani na Fiston Mayele dk 41 na Saido Ntibazonkiza dk 90′.
Kisha kipa huyo katika mchezo uliokuwa muhimu kwa Yanga katika kuwania ubingwa, Mshery alikaa langoni Juni 15m 2022 na Yanga kushinda 3-0, mabao yakifungwa na Fiston Mayele dk 35′ na 68 na jingine la Chico Ushindi dk 52.
Kipa huyo alikaa tena dhidi ya Coastal Agosti 20, 2022 katika msimu wa 2022-2023 na Yanga kushinda mabao 2-0 yaliyowekwa kimiani, Bernard Morrison dk 4 na Fiston Mayele dk 68, na kulinda rekodi yake dhidi ya Wagosi akiwa langoni bila kutunguliwa ndipo leo mambo yametibukia.
Leo akiiongoza Yanga kwenye mchezo wa FA, Mshery ameruhusu nyavu zake kutikiswa dakika ya 18 ya mchezo baada ya shuti kali lililopigwa na Miraji Abdallah nje ya 18 na kukwama moja kwa moja nyavuni baada ya Clement Mzize kunyang’anywa mpira na kumfikia mfungaji huyo aliyekuwa nahodha.

Hata hivyo, Mshery huenda amejifariji kutokana na mabao na Maxi Nzengeli aliyefunga mara mbili dak ya 2 na 15 na lile la Mzize dakika ya 21 lililoivusha Yanga hadi hatua ya 16 Bora ikijiandaa sasa kuvaana na Songea United.
Ukiondoa mchezo huo Mshery tayari alikaa langoni kwenye mchezo dhidi ya Copco timu yake ikiibuka na ushindi wa mabao 5-0, ikiwa ni mechi ya hatua ya 64 katika msimu huu, ambapo Yanga inasaka ubingwa kwa msimu wa nne baada ya kulishikilia taji hilo kwa misimu mtatu mfululizo.