Al Ahly yatanguliza mguu fainali ya CAFCL

Sare isiyo ya mabao iliyopata watetezi wa Ligi ya Mabingwa Afrika, Al Ahly ya Misri ikiwa ugenini dhidi ya TP Mazembe ya DR Congo, imeiweka pazuri timu hiyo ya Misri katika na nafsi ya kutinga fainali ya 17 tangu mwaka 1987.

Katika mechi ya mkondo wa kwanza ya nusu fainali iliyopigwa jioni ya leo Jumamosi kwenye Uwanja wa TP Mazembe uliopo jijini Lubumbashi, Al Ahly iliwabana wenyeji wao walitwaa taji hilo mara tano ikiwa ni moja ya klabu mbili zinazoshika nafasi ya pili nyuma ya Wamisri hao waliotwaa mara 11.

Al Ahly imeshacheza fainali 16 hadi sasa, zikiwamo tano ilizopoteza na 11 ilizotwaa taji ikiwamo ya msimu uliopita na sasa inahitaji ushindi ikiwa nyumbani ili kutinga fainali ya 17 na kusibiri kujua itcheza na nani kati ya Esperance ya Tunisia na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini zitakazovaana usiku huu katika pambano jingine la nusu fainali jijini Tunis, Tunisia.

Pambano la Lubumbashi limekuwa ni la tano kwa Mazembe na Al Ahly kukutana katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika tangu mwaka 2000, huku rekodi zikiwabeba Wamisri wakicheza nyumbani kwani mechi zote mbili zilizopita kati ya nne za awali walizokutana imeshinda.

Al Ahly ilishinda nyumbani mechi ya kwanza kwa bao 1-0 mchezo uliopigwa Sept 01, 2002 kisha kurudia tena July 08, 2012 kwa mabao 2-1.

Katika mchezo huo wa Lubumbashi, timu zote zitajilaumu kwa kushinda kutoka na mabao kwani, kila moja zilitengeneza nafasi nyingi zilizoshindwa kukwamisha wavuni, lakini imekuwa faida zaidi kwa Al Ahly ambao walionekana kushangilia sana mara baada ya filimbi ya mwamuzi Pacifique Ndabihawenimana kutoka Burundi.

Saa 4:00 usiku utapigwa tena mchezo mwingine wa nusu fainali kati ya Esperance na Mamelodi.

Mechi hiyo ya Tunisia itakuwa ni ya saba kwa timu hizo kukutana tangu 2000, huku wenyeji wakibebwa na rekodi tamu za nyumbani mbele ya wageni wao, walioitoa Yanga kwenye robo fainali kwa penalti baada ya mechi mbili za awali kumalizika bila ya bao.

Katika mechi tatu za awali za nyumbani, Esperance imeshinda moja kwa mabao 3-2 mwaka 2000, huku nyungine mbili za mwaka 2001 na 2017 zikiisha kwa suluhu, huku ugenini ikipasuka mara moja mbele ya Wasauzi walipofungwa 2-0 mwaka 2000, na kushinda moja kwa mabao 2-1 mwaka 2017 na ile ya mwaka 2001 ililazimisha suluhu.

Kama ilivyokuwa kwa mechi ya Lubumbashi, hata mchezo huu wa Tunisia sio mwepesi, licha ya wageni kupewa nafasi kubwa ya kuibuka na ushindi kutokana na aina ya kikosi ilichonacho kilichoruhusu bao moja tu hadi sasa katika mechi nane zilizopita za michuano hiyo kwa msimu huu kuanzia makundi hadi robo fainali.

 Itakuwa bonge la burudani kwa mashabiki wa soka nchini ambao watazifuatilia mechi hizo za nusu fainali sambamba Kariakoo Dabi itakayopigwa Kwa Mkapa ikiwa ni mechi ya marudiano ya Ligi Kuu Bara baada ya awali Yanga kushinda 5-1 katika mechi ya mkondo wa kwanza iliyopigwa Novemba 5 mwaka jana.

Zilizopita Mazembe Al Ahly

Related Posts