M23, Rais Tshisekedi uso kwa uso Angola Machi 18

Luanda. Mazungumzo yanayolenga kurejesha amani Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kati ya viongozi wa Muungano wa Waasi wa Alliance Fleuve Congo (AFC/M23) na Rais Felix Tshisekedi yatafanyika Machi 18,2025.

Taarifa ya kufanyika mazungumzo hayo, ilitolewa na Ikulu ya Angola jana jioni kuwa mazungumzo hayo yatafanyika Jijini Luanda nchini humo ambapo viongozi wa pande hizo watakutanishwa kwa mara ya kwanza nchini humo.

Juzi (Jumanne), marais  Felix Tshisekedi na Joao Lourenço walikutana mjini Luanda katika kile kinachotajwa ni kutafuta mwarobaini wa mzozo huo.

 Angola ambayo ni mpatanishi katika mgogoro unaoendelea Mashariki mwa DRC, ilitangaza nia yake ya kuanzisha mazungumzo kati ya Serikali ya Rais Tshisekedi na kundi la waasi la AFC/M23.

Hata hivyo, tangazo hilo linazua maswali miongoni mwa jamii ya kimataifa japo Ofisi ya rais wa DRC ilithibitisha Jumatano jioni kwamba tayari imepokea mwaliko.

Jitihada za awali za mazungumzo ya amani yaliyosimamiwa na Angola yameshindwa kusitisha mapigano kati ya Jeshi la Ulinzi la DRC (FARDC), katika eneo lenye hali tete la DRC linalokabiliwa na mapigano kati ya makundi mbalimbali yenye silaha.

Lakini siku ya Jumanne, Angola ilisema pande hizo mbili zilikubaliana kuja kwenye meza ya mazungumzo, baada ya Rais wa DRC, Felix Tshisekedi kujadili mzozo huo na mwenzake wa Angola, Joao Lourenco.

“Kufuatia hatua zilizochukuliwa na upatanishi wa Angola, wajumne kutoka DRC na M23 wataanza mazungumzo ya moja kwa moja ya amani mnamo Machi 18, 2025 katika mji wa Luanda,” ofisi ya rais wa Angola ilisema katika taarifa yake jana jioni.

Tshisekedi hapo awali alikataa kufanya mazungumzo na M23 inayodaiwa kuungwa mkono na Serikali ya Rwanda ambayo imefanya mashambulizi makubwa mashariki mwa DRC.

Rwanda imekanusha kila mara kuhusiana na madai hayo ya kuifadhiri M23, huku Rais Paul Kagame alidai hana taarifa za uwepo wa vikosi vya Jeshi la Rwanda (RPF) Mashariki mwa DRC.

Tangu mapema Januari, M23 waliiteka miji mikubwa ya Mashariki mwa DRC hususan  makao makuu ya Jimbo la Kivu Kaskazini, Goma na Bukavu ambayo ni makao makuu ya Kivu Kusini huku hofu ikitanda wakati huu ambao wanatajwa kusonga mbele kuelekea Uvira.

Katika chapisho lake kwenye mtandao wa X kiongozi wa M23, Bertrand Bisimwa alijigamba kwamba wamefaulu kumlazimisha Tshisekedi kwenda kwenye meza ya mazungumzo, na kuliita “chaguo pekee la kistaarabu la kutatua mgogoro uliopo”.

Hayo yanajiri wakati viongozi wa jumuiya ya SADC wakitarajiwa kukutana leo Alhamisi Machi 13,2025, h kujalidi mgogoro huo wa DRC.

Serikali ya Rais Tshisekedi imesema takriban watu 7,000 wamefariki kutokana na mgogoro huo tangu Januari.

Wiki iliyopita, Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa liliripoti kuwa karibu watu 80,000 wamekimbia nchi hiyo kutokana na mapigano.

Tangu Januari, watu 61,000 wamewasili nchi jirani ya Burundi, kulingana na Naibu Mkurugenzi wa Ulinzi wa Kimataifa wa shirika hilo, Patrick Eba.

M23 ni mojawapo ya makundi karibu 100 yenye silaha yanayopigania kudhibiti rasilimali mashariki mwa DRC, eneo lenye hifadhi kubwa za madini ya kimkakati kama vile Coltan, Cobalt, Aluminum, na Lithium.

Majirani wa DRC, wakiwemo Burundi na Uganda wana majeshi yao mashariki mwa DRC, hali inayoongeza hofu ya vita vya kikanda ambavyo vinaweza kufanana na vita vya DRC vya miaka ya 1990 na mapema 2000 vilivyoua mamilioni ya watu.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.

Related Posts