Dodoma. Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Dk Festo Dugange wa amewaagiza wakurugenzi (DED), wenyeviti na mameya wa halmashauri nchini kufanya tathimini juu ya mianya ya upotevu wa mapato na kuchukua hatua za kisheria haraka.
Dk Dugange ameyasema hayo jana jioni Jumatano, Machi 12, 2025 wakati akifunga mkutano wa 39 wa Jumuiya ya Serikali za Mitaa Tanzania (ALAT) jijini Dodoma.
Dugange amewataka kwenda kufanya tathimini katika halmashauri zao juu ya ukusanyaji wa mapato na kama kuna mianya ya upotevu wachukue hatua za kisheria za haraka kwa kujiridhisha kama wamehusika na upotevu wa mapato na kisha kuwapeleka mahakamani.
“Mkajiridhishe kama wataalamu wamehusika na upotevu wa mapato kwa kutumia risiti feki au kwa utaratibu wowote. Tunataka kuona hatua za kisheria zinachukuliwa haraka iwezekanavyo na zionekane kupitia vyombo vya habari kuwa wamepelekwa mahakamani na Tamisemi tuipate taarifa hiyo,” amesema Dk Dugange.
“Tuhakikishe sheria inachukua mkondo wake kama kuna mkuu wa idara, mkuu wa kitengo ama mtaalamu aliyehusika kupoteza mapato yetu katika halmashauri tuhakikishe tunaona kupitia vyombo vya habari wako katika mikono ya sheria na hatua stahiki za kisheria zichukuliwe dhidi yao,” amesisitiza Dk Dugange kwa niaba ya waziri mwenye dhamana Mohamed Mchengerwa.
Amesema kutokana na unyeti wa kazi zao ni lazima wadhibiti upotevu wa mapato ya ndani ya halmashauri na kuna maeneo ambayo ufujaji wa mapato upo kwa kutumia risiti feki.
Ametoa mfano wa Halmashauri ya Meatu mkoani Simiyu ambapo kuna watu wanatumia flashi inayotengeneza risiti na kuunganishwa katika mfumo wa risiti za kielektroniki za Pos ili kukidhi matakwa ya wanaotengeneza.
Amesema jambo hilo halikubaliki na kumtaka Mkurugenzi na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Meatu kwenda kulidhibiti jambo hilo haraka.
Agizo hilo ni kuitikia wito uliotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan, Machi 11, 2025 alipokuwa akifungua mkutano huo alipompata Waziri Mchengerwa kushughulikia kikamilifu wabadhirifu akishindwa atachukua hatua dhidi yao na yeye (Mchengerwa) mwenyewe.
Rais Samia alisema bado kuna changamoto katika ukusanyaji wa mapato, akifichua licha ya kuwepo kwa mifumo halali, bado kuna watu wasio waaminifu wanaounda mifumo ya pembeni inayokusanya fedha matokeo yake haziingii serikalini.
“Waziri na wakurugenzi, nataka muwe macho katika hili, kwa sababu fedha hizi zikikusanywa zitaingia katika mfumo halali na zitakwenda kufanya maendeleo. Tukiachia zikaenda mikono mingine, maendeleo yetu yatadorora,” alisema Rais Samia na kuongeza:
“Mheshimiwa Waziri (Mchengerwa), kama mmewabaini hawa watu, tafadhali sana… lile jicho lako la huruma hapa hapana… Ukishindwa kuwachukulia hatua, nitakuita na kukuuliza umefanya nini? Hukufanya kitu? Mimi nitafanya kwako na kwao, wao uliowasamehe na wewe uliyewasamehe,” alisema Rais Samia.
Katika hatua nyingine, Dk Dugange amesema eneo la ukusanyaji kodi ya majengo na ushuru wa mabango bado halmashauri hazijafanya vizuri, ambapo ni asilimia 38 hivyo kuwataka kufanya tathimini ni kwa nini hawajafika malengo kusudiwa na ifikapo Juni mwaka huu wawe wamefikia asilimia 90.
Pia, amewataka kusimamia utoaji huduma kwenye sekta za afya ili kuondoa malalamiko ya wananchi kwa Serikali kuhusu huduma na lugha mbaya kwa wateja na kuweka mikakati ya kudhibiti fedha za uchangiaji huduma za afya.
Awali, Naibu Katibu Mkuu Tamisemi, Atupele Mwambene amesema katika Tamisemi imetumia mkutano huo kujua changamoto za kiutendaji ili kuzitatua.