Na Seif Mangwangi, Arusha
SERIKALI imesema itaendelea kuweka wazi taarifa ya uwekezaji na mapato yanayopatikana katika sekta ya madini, gesi na mafuta nchini kama sheria inavyotaka.
Hayo yameelezwa leo Machi 13, 2025 na Mawaziri Innocent Bashungwa Waziri wa Mambo ya ndani ya Nchi na Waziri wa Madini, Anthony Mavunde walipokuwa wakifungua mkutano wa 62 wa bodi ya kimataifa ya uwazi na uwajibikaji (EITI), ulioanza leo jijini hapa.
Waziri Bashungwa amesema wananchi wanapaswa kufuatilia na kujua mambo yanayoendelea katika sekta ya madini, gesi na mafuta hivyo Serikali itaendelea kufuatilia mapato hayo ili kuweka wazi na kuleta uaminifu kwa wananchi.
” Kwa kuzingatia Tanzania ni mwanachama wa bodi ya EITI inayosimamia uwazi na uwajibikaji, Mwaka 2015 Serikali ilitunga sheria ya kusimamia uwazi na uwajibikaji katika rasilimali madini, mafuta na gesi asilia, sura 447, ” amesema.
Waziri wa madini Anthony Mavunde, amesema taasisi ya TEITI inayosimamia uwazi na uwajibikaji nchini, imekuwa ikifanya vizuri kazi yake ambapo taarifa ya mwisho imeonyesha Serikali imeendelea kufanya vizuri katika kuweka uwazi na uwajibikaji wa taarifa za mapato yanayopatikana katika sekta hizo.
“Watu wengi wamekuwa wakitamani kuona nchi yetu inanufaikaje na rasilimali zilizopo kwenye madini, gesi na mafuta , kwa kupitia utaratibu huu wa uwazi na uwajibikaji ambao nunawekwa kwenye taarifa za mapato ndipo wananchi wetu wanaweza kufahamu jinsi rasilimali hizo zinavyoweza kututajirisha, ” amesema.
Amesema chini ya Serikali ya awamu ya sita ya Rais Samia Suluhu Hassan sekta ya mafuta, gesi asilia na madini zimekuwa zikifanya vizuri na hivyo kuvutia wawekezaji wengi zaidi nchini.
Mwenyekiti wa Kamati ya usimamizi wa shughuli za Taasisi ya uwazi na uwajibikaji nchini (TEITI), Ludovick Uto amesema bodi hiyo inakutana kwa mara ya kwanza Tanzania tangu Tanzania kujiunga mwaka 2009.
Taasisi ya kimataifa ya uwazi na uwajibikaji (EITI), yenye makao yake makuu Oslo nchini Norway ina wanachama 57 Duniani.