SIKU za mwanzoni za Prince Dube ndani ya Yanga, kijiweni hapa na katika mitaa mingi tuligawanyika sana kuhusu mshambuliaji huyo kutoka Zimbabwe.
Mambo yalikuwa hayamuendei vizuri wakati hivyo kukawepo makundi mawili ambayo ni moja lililo nyuma ya mshambuliaji huyo na jingine likiwa na hisia tofauti juu yake.
Ambao walikuwa wamegoma kushuka kwenye basi la Dube walikuwa wanasisitiza kuwa jamaa ni mshambuliaji wa maana hasa na kwa kipindi kile hakuwa sawa tu kisaikolojia jambo ambalo lilimpunguzia hali yake ya kujiamini lakini anayo nafasi ya kuonyesha makali yake.
Upande mwingine wakawa wanajaribu kutuaminisha kuwa Dube alichokuwa anakionyesha ndio uwezo wake halisi na hakikuwa kinatokea kwa bahati mbaya kwani hata akiwa Azam hajawahi kuwa na muendelezo wa kufanya vizuri.
Kumbe jamaa alikuwa anasikiliza na kuona tulivyokuwa tunabishana kuhusu yeye na akapanga kutoa majibu ndani ya uwanja na hicho ndicho ambacho kinatokea hivi sasa ambapo amefanya wote kuwa upande mmoja.
Anaifanya safu ya ushambuliaji ya Yanga kuwa moto wa kuotea mbali hivi sasa kutokana na uwezo mkubwa ambao anauonyesha kwa kufunga mabao na kupiga pasi za mwisho tena kwa muendelezo bila kipengele chochote.
Katika Ligi Kuu yupo kileleni katika chati ya ufungaji bora akipachika mabao 10 sawa na mshambuliaji mwenzake wa Yanga, Clement Mzize na kiungo wa Simba, Jean Charles Ahoua. Kiujumla kwa sasa Dube ndiye mchezaji aliyehusika katika mabao mengi (17)kuliko mwingine yeyote katika Ligi Kuu Bara akifunga 10 na kutoa asisti 7.
Sasa hivi sote tumeungana, jamaa anajua.