JK atoa angalizo jamii kumsahau mtoto wa kiume

Dar es Salaam. Rais Mstaafu wa awamu ya nne, Jakaya Kikwete ametoa tahadhari akisema wakati nchi ikifanikiwa kumnyanyua mtoto wa kike, muhimu ni kutomuacha nyuma mtoto wa kiume kielimu.

Amesema hatua hiyo itaisaidia nchi kusonga mbele katika ulimwengu wa sasa, kwani kumuacha nyuma mtoto wa kiume anaweza kuja kuwa tatizo katika jamii.

Kikwete ameyasema hayo leo Ijumaa, Mei 17, 2024 wakati wa mahafali ya 7 ya Shule ya Uongozi ‘Uongozi Institute’ ambayo jumla ya viongozi 198, kutoka programu tatu za uongozi katika ngazi ya cheti, diploma na uongozi kwa wanawake wamehitimu.

Amesema viongozi wanaohitimu wanawake pia ni wengi, hiyo inaonyesha namna ambavyo hata katika uongozi namba inaongezeka.

“Nchi imepiga hatua kubwa sana kumnyanyua mtoto wa kike kielimu, lakini wa kiume naye amezaliwa kutoka tumbo la mwanamke, huyu mwingine tunahangaika naye wa kiume hawa tunawaacha wanapaa samaki huko Pwani, lazima tuhakikishe tunaweka mzani sawa na kuwapa thamani nao,” amesema.

Kikwete ambaye ni Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) amesema kwa kipindi cha miaka miwili ameshuhudia chuo hicho kikitoa wahitimu ambao asilimia 52 hadi 53 ni wasichana.

“Ni sawa na inapendeza sana elimu kwa mtoto wa kike ni muhimu sana, lakini naanza kushtuka kidogo kuna uwezekano tunawasahau wa kiume tusimuache baadaye akaja kuwa tatizo katika jamii. Tuangalie tumetoka wapi, tutawaweka wanawake katika nafasi za uongozi wanaume nao wawe sambamba,” amesema Kikwete.

Katika mahafali hayo ambayo miongoni mwa wahitimu ni viongozi kutoka Nigeria, eswatin, Demokrasia ya Congo, Kenya na Malawi kiongozi huyo ameushauri uongozi wa taasisi hiyo kubadilisha jina ili kuendana na huduma wanayotoa ya mafunzo ya uongozi.

Kikwete ameelezea namna taasisi hiyo ilivyoanzishwa na kwamba lengo ilikuwa kutoa mafunzo kwa viongozi wa Afrika.

“Tanzania tumekuwa waanzilishi wa hii taasisi, tuifanye iwe yetu na tuipe jina linalohusudu bara la Afrika, ningeshauri iitwe ‘African Leadership institute’ kisha kwenye mabano tuandike ‘Uongozi Institute’ hili jina la uongozi linaleta shida kwa wengi katika kulitamka,” amesema.

Katika hatua nyingine, amewataka viongozi hao kuacha alama katika kila taasisi watakayoiongoza na kupenda kujisomea ili wawe na mawazo mapya.

“Ukipewa nafasi ya uongozi leo, anza kuchukua hatua mapema na kutafakari ukiondoka watu watakukumbuka kwa lipi. Acha alama zako pale, fikiria nikistaafu watu watanikumbukaje? Lazima uanze kujipanga namna gani utatekeleza majukumu yako, lakini ukizingatia kuacha alama,” amesisitiza.

Miongoni mwa vitu alivyosisitiza zaidi ni kuachana na mitandao ya kijamii, “Achaneni na mitandao. Wengi wanapoteza muda mwingi huko na wanasoma yasiyofaa udaku, vijembe na mengine mengi kama hutakuwa makini hata faili ofisini hutasoma, nashauri endeleeni kusoma vitabu mpate maarifa zaidi.”

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, George Simbachawene amewapongeza wahitimu hao kwa kufanikiwa kumaliza programu hiyo na kuwataka kwenda kuonyesha uwezo wa kile walichojifunza.

Naye Katibu Mkuu Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Injinia Zena Ahmed Said amesema mafunzo hayo yakifanywa kwa vitendo, yatasaidia kuboresha uongozi na kufikia malengo ambayo nchi imejiwekea.

Amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imekuwa ikishirikiana na Shule ya Uongozi kutoa mafunzo kwa viongozi wapya wakiwemo mawaziri, makatibu wakuu lakini pia wanasaidia kutoa ufadhili kwa wanafunzi wao.

Akizungumzia uongozi wa wanawake amesema, mafunzo hayo ni muhimu yanasaidia viongozi wanawake kukabiliana na changamoto zinazowakabili katika uongozi, itasaidia kuwapa uwezo na mbinu mpya kushika nafasi zao vizuri zaidi.

“Wataweza kuwa na mawazo mazuri na mawasiliano yaliyo bora, kama uwezo wako wa kuwasiliana uko vizuri itakuwezesha kufanya mawasiliano mazuri katika malengo kwa kusaidia na watu wanaokusaidia.”

Amesema Zanzibar ina wahitimu 15, ambao ni sawa na asilimia 7.5 ya wahitimu wote.

Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dk Moses Kusiluka amesema, Serikali ina jukumu la kuhakikisha viongozi wa umma wanajengewa uwezo ili kuwa na uongozi bora.

“Tumeweka uwekezaji kuhakikisha malengo haya yanafikiwa, Serikali imetenga fedha kuhakikisha hili linafanikiwa kwa watumishi wa umma na sekta binafsi,” amesema Balozi Kusiluka.

Related Posts