Tunataka Katiba lakini… | Mwananchi

Unguja. Ili kupata Katiba mpya, maendeleo ya demokrasia, chaguzi zenye haki na utawala bora, wadau wametoa mapendekezo wakitahadharisha madai yafanyike pasipo umwagaji damu.

Viongozi wa dini, asasi za kiraia na wanasiasa wamesema umefika wakati wa kushirikiana kama Taifa bila kujali tofauti za vyama au dini kuandamana kwa njia ya amani kudai Katiba mpya, vinginevyo itapita miaka mingine zaidi ya 20 bila hayo kufikiwa.

Akizungumza jana katika Jukwaa la Demokrasia Tanzania 2024, Abubakar Muhamed Ali, aliyekuwa mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, amesema kinachopaswa kufanyika ni kutumia elimu kwa mpigakura kama walivyofanya mwaka 2015.

“Tutumie njia hiyo tufanye kazi, Mungu atuepushe usitokee mvutano. Mara nyingi Katiba haipatikani mpaka damu zimwagike, lakini ni vyema kuendelea kuchimba kuna namna ya kupata Katiba mpya,” amesema.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maimamu Zanzibar, Sheikh Farid Ahmed, amesema ipo haja ya kuamini kwamba Katiba mpya itapatikana bila kukata tamaa, ila kinachotakiwa ni kuwashauri viongozi waliopo madarakani kuhusu umuhimu wake.

“Iwe ‘slogani’ yetu kuhakikisha tunapata Katiba bila kumwaga damu, kuleta vilema na mengine ikiwa wengine walipata Katiba kwa kumwaga damu lakini tusifike huko, tunazo njia nyingine,” amesema.

Ameongeza: “Maadamu wananchi wanataka Katiba, itafika wakati wataipata, kama tunavyokumbuka ilifika wakati watu walikuwa hawawezi kuzungumza Katiba, lakini sasa angalau kuna mazungumzo na watu wanaweza kuzungumza.’’

Amesema wamepita viongozi katika miaka tofauti na kufanya mabadiliko katika Katiba, hivyo wasijenge imani ya hofu kwamba hawatapata Katiba mpya, kwani kinachopangwa na Mungu hakiwezi kuzuiwa na binadamu.

Ili kuwashawishi viongozi hao, Sheikh Farid amesema ni vyema kuonyesha hatari na faida za kubadilisha Katiba, kwani Rais hawezi kufanya kila kitu, lakini asasi za kiraia zinaweza kuonyesha kwa maandishi.

“Tuonyeshe kwamba watu watafaidika vipi, wanyonge, watanufaika vipi, na wafanyabiashara watanufaika vipi. Iwapo wasipoona umuhimu wake, hawawezi kuona haja ya kushiriki hata katika mchakato wa kupata Katiba mpya,” amesema.

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza amesema kwa sasa baadhi ya chaguzi zinaonyesha ushiriki mdogo wa watu kwa hiyo utaratibu huo ukiachwa uendelee itakuwa hatari siku za mbele.

“Kwa sasa inaonekana watu wamekata tamaa katika chaguzi, ishara hiyo si nzuri…Kuna hatari ya siku moja kuwa na viongozi waliochaguliwa na wananchi wachache,” amesema.

Askofu Bagonza amesema Taifa la Tanzania lina historia iliyotukuka na ya kipekee katika ukanda wa Afrika, akisema lilipata uhuru na kustahimili vita baridi kati ya Mashariki na Magharibi bila kumwaga damu.

“Tuliingia mfumo wa vyama vingi bila kumwaga damu, tumeulinda Muungano wetu bila kumwaga damu, sasa tunahitaji Katiba mpya bila kumwaga damu. Viongozi wetu wasikie kwamba historia yetu ya kupata vitu bila kumwaga damu iendelee kutunzwa,” amesema Bagonza.

Naye Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo  (Chadema), Freeman Mbowe amesema kinachotofautisha Tanzania na nchi nyingine, zikiwamo Kenya na Afrika Kusini, hakuna ubaguzi na ukabila kama mataifa hayo yalivyo.

“Hakuna anayesema haitaki Katiba, kuna jambo linatuunganisha lakini miaka 30 ambayo tumepita bila kupata Katiba mpya lazima tuangalie njia tulizotumia kama bado zinatufaa,” amesema.

Mbowe amehoji kuendelea kutegemea kudra za Mwenyezi Mungu, huku akieleza hakuna maudhui yanayotoa tiba ya majeraha yanayotokana na ukosefu wa Katiba mpya.

Amesema Serikali inaelewa mahitaji ya Watanzania, hivyo ucheleweshaji unaotolewa ni wa makusudi.

Mbowe amesema sababu wanazijua wenyewe, kwani wamezungumza na Serikali kwa kipindi cha mwaka mmoja kuhusu umuhimu wake.

Kwa mujibu wa Mbowe, walijaribu kushirikisha umma mpana ili lisiwe la chama, hivyo wakapanga maandamano katika mikoa zaidi 16 ya Tanzania baada ya Serikali kuruhusu maandamano kufanyika.

“Tunachoshukuru Mungu hakuna aliyejeruhiwa wala kufanya vurugu na rika zote walishiriki, kwa hiyo hii inaweza kutusaidia kupata Katiba mpya tujenge msukumo kutokana na umoja wetu kwamba siku moja tuandamane kama Taifa kudai Katiba bila kuangalia nani,” amesema.

Ameongeza: “Kwa sasa tufike wakati tukatembee kwa pamoja bila kujali dini zetu, vyama vyetu wala watu gani, badala ya kutembea watu wachache wa Chadema, nina hakika tukifikia hatua hiyo watawala wataona umuhimu huo,” amesema.

Mbowe alisema huenda Rais akawa anaambiwa Katiba ni dai la  chama kimoja, lakini iwapo akiona mshikamano,  itampa nguvu na kuruhusu mchakato uendelee na kujenga umoja wa kitaifa.

Amesema iwapo wakiendelea kukaa katika mikutano na kujifungia itafika miaka 20 bila kupata Katiba.

Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa-ZNZ), Dk Mzuri Issa amesema wadau wana nafasi kubwa kuongeza msukumo wa kudai Katiba na uchaguzi ulio huru na haki.

Amesema Azaki  zikiendelea kuwa na imani mambo yatakuwa mazuri, japo inawezekana yasipatikane matarajio yanayolengwa.

Related Posts