Unguja. Ofisi ya Rais, Ikulu, kwa mwaka wa fedha 2024/25 imepanga kutekeleza miradi mitatu ya maendeleo, ukiwamo wa uimarishaji wa mfumo wa ulinzi na usalama katika majengo ya Ikulu na makazi Rais.
Akisoma hotuba ya bajeti Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Ikulu, Ali Suleiman Ameir, amesema mradi mwingine ni uimarishaji wa mfumo wa ulinzi na usalama katika nyumba za viongozi wa Serikali.
Ameliomba Baraza la Wawakilishi kuidhinisha Sh24 bilioni, akisema miradi imetengewa Sh4.5 bilioni.
Ofisi hiyo pia imepanga kuimarisha mawasiliano ya Mfumo wa Sema na Rais Mwinyi (SNR).
Kwa kipindi cha Julai hadi Machi 2023/2024, kitengo cha Sema na Rais Mwinyi kimepokea malalamiko 2,713 kutoka kwa wananchi.
Kati ya hayo, malalamiko 1,460, sawa na asilimia 53.8 yamepatiwa ufumbuzi na mengine 1,253 sawa na asilimia 46.2 yanaendelea kufuatiliwa kwa hatua mbalimbali ili kupatiwa ufumbuzi.
Kwa kutambua umuhimu na michango inayotolewa na Wazanzibari wanaoishi nje ya nchi (Diaspora) kwa nchi yao ya asili, wizara imekamilisha kanuni za usajili wa wanadiaspora wa Zanzibar na kutiwa saini na waziri.
Amesema kanuni hizo zitawezesha mfumo wa usajili wa wanadiaspora wa Zanzibar kuanza kutumika.
Hadi sasa mfumo huo umeshakamilika na kufanyiwa ukaguzi wa usalama na Wakala wa Serikali Mtandano (EGAZ) ambao umeruhusu mfumo huo kuanza kutumika.
“Ofisi imeendelea na utaratibu wa kuwasajili wanadiaspora wanaofika katika Ofisi za Diaspora. Kwa kipindi cha Julai 2023 hadi Machi 2024 jumla ya wanadiaspora 51 wamesajiliwa kupitia fomu maalumu,” amesema.
Wanadiaspora hao ni kutoka Oman, Uingereza, Burundi, Kenya, Falme za Kiarabu, Luxembourg, Uholanzi, Ukraine, Denmark na Yemen.
Katika kipindi hicho, ofisi imewaombea wanadiaspora vibali vya kazi 22 na vibali vya ukaazi 23 ili waweze kukaa nchini na kuendelea na shughuli za kiuchumi.
Amesema ofisi imefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuratibu na kusimamia mapokezi ya wageni waliofika kuonana na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Amesema ofisi hiyo imeratibu na kuwapokea wageni 1,105 waliotembelea na kukutana na Rais kati yao, 953 walikuwa ni raia wa Tanzania na 152 walitoka nje ya mipaka ya nchi.
“Ziara za wageni hawa zilikuwa ni sehemu muhimu katika kukuza uhusiano wa karibu na wananchi na kushirikiana katika kuleta maendeleo ya Zanzibar. Hatua hii inaonyesha umuhimu wa uwazi, uwajibikaji na uhusiano wa karibu kati ya viongozi na wananchi pamoja na watu wa mataifa mengine duniani waliopo Zanzibar,” amesema.
Miongoni mwa wageni hao ni Rais wa Poland, Andrzej Duda na mabalozi wanaowakilisha nchi zao Tanzania.
Katika mazungumzo yao walijadili masuala muhimu yanayohusu vipaumbele vya maendeleo, ikiwa ni pamoja na uchumi wa buluu, elimu, afya, na miundombinu.
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Baraza la Wawakilishi ya Kusimamia Ofisi za Viongozi Wakuu wa Kitaifa, Machano Othman Said amesema ipo haja ya Serikali kuiangalia taasisi ya utunzaji wa nyaraka na kumbukumbu kwa matumizi ya Serikali na umma, ili nyaraka hizo ziwe na mchango mkubwa katika sekta ya elimu na utamaduni.
“Kupitia bajeti hii kamati inaishauri Serikali kuzitatua changamoto zinazowakabili za upungufu wa vifaa vya kisasa ambavyo vinahitaji fedha nyingi na wataalamu katika kuendeleza uhifadhi wa nyaraka za muda mrefu,” amesema.