Dar es Salaam. Serikali ya Tanzania kupitia Waziri wa Afya, Jenista Mhagama imetangaza kumalizika kwa mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Marburg katika Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera.
Kupitia taarifa iliyotolewa leo Alhamisi Machi 13, 2025 Mhagama imeeleza kuwa mgonjwa wa mwisho aliyethibitika kuwa na virusi hivyo (MVD) aliripotiwa Januari 28, 2025 hivyo hadi kufikia Machi 11, 2025, ni siku 42 zinakuwa zimepita tangu kuwepo kwa mgonjwa huyo wa mwisho.
Serikali yatangaza kumalizika kwa Marburg Tanzania
“Kitaalamu na kulingana na kanuni na taratibu za Shirika la Afya Duniani (WHO), tumekidhi vigezo vya kutangaza rasmi kumalizika kwa mlipuko wa MVD. Hivyo basi, leo Machi 13, 2025, ninatangaza rasmi kumalizika kwa mlipuko wa MVD nchini,” amesema Mhagama.
Januari 20, 2025, Rais Samia Suluhu Hassan, alitangaza uwepo wa mlipuko wa ugonjwa wa Virusi vya Marburg katika Mkoa wa Kagera, ambapo wagonjwa wawili walithibitika kuwa na maambukizi.
“Kwa masikitiko makubwa, wote wawili walipoteza maisha wakiwa kwenye matibabu. MVD ni ugonjwa hatari unaoweza kusambaa kutoka mtu mmoja hadi mwingine kupitia mgusano wa moja kwa moja na majimaji ya mwili kutoka kwa mtu aliyeambukizwa,” amesema.
MVD ikiwa haitadhibitiwa kwa wakati inaweza kusababisha madhara makubwa ikiwa ni pamoja na vifo na athari za kijamii na kiuchumi.
Hata hivyo, tangu kutangazwa kwa mlipuko, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ilichukua hatua madhubuti kudhibiti na kuzuia kuenea katika halmashauri ya Biharamulo iliyoathirika ikiwemo kutoa taarifa za mara kwa mara kupitia vyombo vya habari na majukwaa mengine, hadi leo hii unapotangazwa kuisha.
“Nasisitiza kwa jamii yote kuendelea kuwa makini hata baada ya kutangazwa kumalizika kwa mlipuko huu, kwa kuzingatia hatua zote za kujikinga, ikiwa ni pamoja na kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni au kutumia vitakasa mikono (sanitizer), kutoa taarifa kwa wakati za uvumi au tukio lolote lisilo la kawaida katika jamii kupitia namba ya dharura 199, au kituo cha afya kilicho karibu.”