Kocha wa timu ya Vijana Queens, Kabiola Shomari, amesema kuondoka kwa wachezaji wake, Happy Danford na Tumaini Ndossi kujiunga na timu ya Tausi Royals, timu yake haitatetereka.
Usajili wa timu ya Tausi Royals kwa wachezaji hao kutoka Vijana Queens, ni wa pili kwao, mwaka jana iliwasajili Diana Mwendi, Tukusubira Mwalusamba na Asumpta.
Kwa mujibu wa kocha huyo, timu ya Vijana Queens haiwezi kumzuia mchezaji yeyote kujiunga na timu anayoipenda.
“Kikubwa zaidi timu inayomuhitaji mchezaji, inatakiwa ifuate taratibu za uhamisho, na sisi tuweze kumruhusu,” alisema Shomari.
Alisema baada ya kuondoka wachezaji hao, wanategemea kuwapandisha wachezaji kutoka kikosi cha pili cha City Queens kuziba nafasi hiyo.
Hata hivyo, alisema watakaowapandisha ni wachezaji walioonyesha kiwango kizuri katika ligi ya mkoa wa Dar es Salaam (BDL) mwaka jana.
“Huu ndiyo utaratibu wetu, hatuchukui mchezaji kutoka nje, tunakuza sisi wenyewe,” alisema Shomari.
Shomari anayefundisha pia timu ya chuo cha IFM, alisema kwa upande wa timu Vijana ‘City Bulls’ imekuwa pia ikikuza vijana chipukizi.
Alitaja timu zilizoundwa na chipukizi hao ni Jogoo ya pili kwa Vijana ‘City Bulls’ pamoja Yellow Jacket.
“Tunakuza wachezaji, na wachezaji wamekuwa wakichuliwa kila mwaka na timu nyingine, kama Jonas Mushi, Romaldnado waliohamia JKT na Baraka Sabibi aliyehamia UDSM Outsiders,” alisema Shomari.