Shinyanga. Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga, imefuta mwenendo, kutiwa hatiani na adhabu ya kifungo cha maisha jela walichohukumiwa vijana wanne waliomlawiti kwa zamu mwanamke mwenye miaka 39 na kumpora simu.
Hukumu imetolewa Machi 12, 2025 na Jaji Ruth Massam baada ya kusikiliza rufaa iliyowasilishwa na vijana hao kupinga hukumu iliyowatupa maisha gerezani. Ameamuru kesi isikilizwe upya mbele ya hakimu mwingine.
Vijana hao, Said Abdallah, Nathania Simon, Masumbuko Jumapili na Samwel Robert, walikata rufaa wakiegemea sababu tatu, lakini iliyozingatiwa ni hoja kuwa Mahakama haikutilia maanani kuwa walikuwa na umri chini ya miaka 18.
Kupitia wakili wao, Emmanuel Sululu, warufani walidai hakimu aliyesikiliza kesi hiyo hakuzingatia utetezi waliouwasilisha kortini kuwa wana umri wa miaka 17 baada ya Jamhuri kupinga kupokewa vyeti vyao vya kuzaliwa.
Walitiwa hatiani na kuhukumiwa kifungo cha maisha jela kwa madai ya kumlawiti mwanamke huyo, tukio lililotokea Desemba 10, 2023 eneo la Mbezi katika Manispaa ya Shinyanga na kisha kumuiba simu ya kiganjani.
Walikana shtaka lakini baada ya Mahakama kusikiliza ushahidi wa pande zote mbili, iliwatia hatiani na kuwahukumu wote kifungo cha maisha jela kwa kosa la kwanza la kulawiti na kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la pili la wizi wa simu.
Baada ya hukumu iliyotolewa mwaka 2024 na Mahakama ya Wilaya Shinyanga, walikata rufaa wakidai hakimu alikosea kisheria kuwatia hatiani akiegemea ushahidi dhaifu wa Jamhuri ambao haukuthibitisha shtaka.
Sababu ya pili walidai hakimu alikosea kisheria alipokataa utetezi wa warufani kuwa walikuwa wadogo chini ya miaka 18 wala hakutoa sababu zinazokubalika na hapakuwa na uthibitisho simu ilipatikana kwa mrufani wa pili.
Wakati wa usikilizaji wa rufaa, wakili Sululu alijikita katika sababu ya pili pekee akisema hakimu alikosea alipowanyima fursa ya kujitetea kuwa wao ni chini ya miaka 18 licha ya kutoa vyeti kuonyesha wana umri wa miaka 17.
Alidai vyeti vyote vya kuzaliwa vilipelekwa mahakamani wakati wa usikilizwaji wa kesi, lakini upande wa mashtaka ulipinga ukidai warufani hawakuwa na mamlaka ya kisheria kuwasilisha vyeti hivyo kama vielelezo.
Jamhuri walipinga kwa sababu warufani hawakuwa wameijulisha Mahakama mapema kuwa wangekuwa na vielelezo hivyo. Ingawa Jamhuri iliweka pingamizi hilo, Mahakama ilivipokea lakini haikuvizingatia katika hukumu.
Hakimu katika hukumu alisema hakuvitilia maanani kwa kuwa viliwasilishwa katika hatua ya utetezi, hivyo wakili Sululu akadai hakimu alikosea kuwahukumu kwa sababu hapakuwa na uthibitisho kuthibitisha umri tofauti.
Akijibu hoja hiyo, Wakili wa Serikali, Goodluck Saguya aliunga mkono hoja za wakili Sululu akisema warufani walinyimwa haki ya kujitetea kuhusu umri na kwamba, walipotoa hoja hiyo, Mahakama ilipaswa kuchunguza umri wao.
Ni kutokana na dosari hizo za kisheria, wakili Saguya aliiomba Mahakama kubatilisha mwenendo wa shauri hilo, kufuta adhabu waliyopewa na kuamuru shauri lisikilizwe upya kwani ushahidi uliokuwa umetolewa ulikuwa ni mzito.
Alipinga ombi la wakili Sululu la kutaka Mahakama iwaachie huru wateja wake kutokana na dosari hizo za kisheria, badala yake akaiomba Mahakama ione kuwa ushahidi ulikuwa mzito na nafuu pekee ni kusikilizwa upya.
Katika hukumu iliyopatikana kwenye tovuti ya Mahakama leo Machi 13, 2025, Jaji Massam amesema baada ya kupitia kwa makini rekodi ya rufaa ya shauri hilo, amebaini warufani wanapinga utetezi wao kuhusu umri haukuzingatiwa.
Jaji amesema hoja ambayo inapaswa kuamuliwa na Mahakama ni kama kulikuwa na ukiukwaji wa taratibu za kuchunguza umri wa warufani na kama utetezi wao ulizingatiwa na Mahakama ya Wilaya Shinyanga iliyosikiliza shauri hilo.
Kwa mujibu wa jaji, ni msimamo wa sheria kuwa endapo kunakuwapo ukiukwaji wa taratibu, Mahakama inaweza kuamuru kuachiwa warufani au kuamuru kesi kusikilizwa upya na amri ya kusikilizwa upya huamriwa pale ushahidi unapokuwa mzito.
Jaji amesema katika shauri lililo mbele yake, hakuna ubishi kuwa katika hatua za mwanzo warufani hawakuibua utetezi kuwa wao ni chini ya umri wa miaka 18 bali waliibua wakati wa hatua ya utetezi na kuwasilisha vyeti vya kuzaliwa.
Mbali na kuwasilisha vyeti hivyo, lakini waliwasilisha kadi za kliniki na nyaraka zote zilipokewa na Mahakama kama vielelezo De 1, De 2, De 3 na De 4.
Jaji amesema Mahakama ina wajibu wa kuchunguza uhalali wa vyeti hivyo na kuamua endapo walikuwa chini ya miaka 18 au hapana, hivyo kushindwa kufanya hilo inabidi akubaliane na mawakili kuwa umri wao haukuchunguzwa.
“Napenda kueleza kuwa, hukumu ya kifungo cha maisha jela kwa walalamikaji (warufani) ni sawa na kusababisha dhuluma zaidi kwao chini ya mazingira ya kesi hii ambayo haikujengwa.
“Kwa hiyo, nakubaliana na wakili Saguya kuwa njia sahihi ya kufanya ni kubatilisha mwenendo wa mahakama ya chini na kuamuru kusikilizwa upya kwa kesi kwa kuwa kuna ushahidi mzito ulitolewa na mashahidi wa Jamhuri dhidi yao,” ameamuru jaji.
Katika usikilizwaji upya, aliamuru Mahakama itakayosikiliza kesi hiyo ni lazima izingatie taratibu na kanuni zilizopo katika kuthibitisha umri wa warufani wakati wanatenda kosa hilo, hivyo anafuta hukumu na adhabu, akiamuru kesi isikilizwe upya.