Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo amesema ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi ni muhimu katika kukuza uwekezaji pamoja na uchumi kupitia nyanja mbalimbali za maendeleo nchini.
Katika kuimarisha hilo, Balozi Kombo amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa Jukwaa la Wakurugenzi Watendaji (CEOrt -Roundtable) ambao ni kiungo muhimu cha ushirikiano kati yake na sekta binafsi.
Akizungumza jana Alhamisi Machi 12, 2025 wakati wa jukwaa la mazungumzo ya Iftar lililoandaliwa na CEOrt lenye kauli mbiu ‘Maadili ya Biashara kwa Ukuaji Jumuishi’ jijini Dar es Salaam, Waziri Kombo amesema jukwaa hilo limeifanya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwa karibu zaidi na sekta binafsi.
“Tunawapongeza sana CEOrt kwa kushirikiana na Serikali katika ajenda ya maendeleo ya nchi hii, mkiwa na mchango mkubwa katika kuajiri, kufanya uamuzi wa kulipa kodi kwa maendeleo ya nchi yetu kupitia wanachama wenu.
“Tunafurahia ushirikiano huu kati ya Serikali na sekta binafsi na jitihada zenu katika kuchochea maendeleo ya nchi yetu kupitia majukwaa mbalimbali na mafunzo,” amesema.
“Tanzania, kupitia taasisi mbalimbali kama vile Baraza la Biashara na kituo cha Uwekezaji imekuwa ikiweka mazingira bora ya kuvutia wawekezaji na miongoni mwa wawekezaji hao ni wanachama wa CEOrt,” amesema.
Balozi John Ulanga ambaye ni Mkurugenzi wa Biashara kimataifa na Diplomasia ya Uchumi kutoka Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje, amesema wanachama wa CEOrt wamekuwa mfano wa kuigwa kwa kufuata maadili ya kazi ikiwamo kuhimiza uwajibikaji, akiitaka jamii kufanya biashara kwa uaminifu ili kuvutia wawekezaji zaidi.
Amesema Tanzania ni kitovu kizuri cha kufanya biashara katika ukanda wote wa kusini mwa Jangwa la Sahara na Afrika, akiwataka wawekezaji kutumia amani na mazingira mazuri ya biashara yaliyopo ili kutanua wigo wa biashara zao.
Wadau mbalimbali wakiwemo mabalozi kutoka nchi za India, Uganda na maofisa kutoka idara mbalimbali za Serikali na wanachama wa CEOrt wameshiriki katika mazungumzo hayo yaliyohimiza uongozi wa kimaadili na uaminifu wa biashara katika kukuza imani, ustawi, na ustahimilivu wa kiuchumi wa muda mrefu wakati Tanzania ikitekeleza malengo ya maendeleo ya 2050.
Aidha akitoa neno la shukrani kwa Balozi Kombo, Mkurugenzi Mtendaji wa CEOrt, Santina Benson amesema wataendelea kufanya kazi na Serikali na wapo tayari kuendeleza ushirikiano uliopo.